Masomo ya Misa Februari 3 Leave a comment

JUMATATU: JUMA IV LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA IV

Mt. Blasi
Utume: Alikuwa Askofu wa Sebaste huko Armenia (Uturuki). Blasi alikuwa imara katika imani na alikufa kwa kukatwa kichwa. Alikufa shahidi wa dini.
Kufariki: Mwaka 316.

SOMO 1. Ebr 11:32-40
Ndugu zangu niseme nini tena? Maana wakati usingenitosha kuleta habari za Gideoni na Baraka na Samsoni na Yeftha na Daudi na Samweli na za manabii; ambao kwa imani walishinda milki za wafalme, walitenda haki, walipata ahadi, walifunga vinywa vya simba, walizima nguvu za moto, waliokoka na makali ya upanga. Walitiwa nguvu baada ya kuwa dhaifu, walikuwa hodari katika vita, walikimbiza majeshi ya wageni. Wanawake walipokea wafu wao waliofufuliwa. Lakini wengine waliumizwa vibaya hata kuuawa, wasikubali ukombozi, ili wapate ufufuo ulio bora; wengine walijaribiwa kwa dhihaka na mapigo, naam, kwa mafungo, na kwa kutiwa gerezani; walipigwa kwa mawe, walikatwa kwa misumeno, walijaribiwa, waliuawa kwa upanga; walizunguka- zunguka wakivaa ngozi za kondoo na ngozi za mbuzi; walikuwa wahitaji, wakiteswa, wakitendwa mabaya; (watu ambao ulimwengu haukustahili kuwa nao), walikuwa wakizunguka-zunguka katika nyika na katika milima na katika mapango na katika mashimo ya nchi. Na watu hao wote wakiisha kushuhudiwa kwa sababu ya imani yao, hawakuipokea ahadi; kwa kuwa Mungu alikuwa ametangulia kutuwekea sisi kitu kilicho bora, ili wao wasikamilishwe pasipo sisi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab. 31:19-23

  1. Jinsi zilivyo nyingi fadhili zako
    ulizowawekea wakuchao;
    ulizowatendea wakukimbiliao
    mbele ya wanadamu.

(K) Iweni hodari, mpige moyo konde,
nyinyi nyote mnaomngoja Bwana.

  1. Utawasitiri na fitina za watu
    Katika sitara ya kuwapo kwako;
    Utawaficha katika hema
    Na mashindano ya ndimi. (K)
  2. Bwana ahimidiwe;
    Kwa maana amenitendea fadhili za ajabu
    Katika mji wenye boma. (K)
  3. Nami nalisema kwa haraka yangu,
    Nimekatiliwa mbali na macho yako;
    Lakini ulisikia sauti ya dua yangu wakati nilipokulilia. (K)
  4. Mpendeni Bwana, ninyi nyote mlio watauwa wake.
    Bwana huwahifadhi waaminifu,
    Humlipa atendaye kiburi malipo tele. (K)

INJILI. Mk 5:1-20
Yesu na wanafunzi wake walifika ng`ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi. Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu; makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo; kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda. Na siku zote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe. Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia; akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese. Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu. Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi. Akamsihi sana asiwapeleke nje ya nchi ile. Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha. Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao. Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini. Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashamba. Watu wakatoka walione lililotokea. Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa. Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe. Wakaanza kumsihi aondoke mipakani mwao. Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye; lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu. Akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu.

TAFAKARI
UTU NI BORA KULIKO MALI: Huyu Mgerasi mwenye pepo anatukumbusha matokeo ya kumwabudu Yesu kwa imani. Tumeelezwa kuwa alipomwona Yesu alimkimbilia na kumsujudia. Mimi na wewe mara ngapi tunatenga muda na kuwa mbele ya Yesu wa Ekaristi na kumweleza shida zetu? Wengi wetu hata tukipatwa na shida hatuanzi na Yesu, tunahangaikia kwingineko kwanza ndio mambo yakienda mrama tunarudi kwa Yesu. Tumeona leo, Yesu anaupa utu hadhi yake. Kitendo cha kuruhusu pepo kuwaingia nguruwe haimaanishi wale nguruwe sio muhimu, bali utu kwanza. Kwa mfano, kuna watu wanaojali mali kuliko utu, yuko tayari hata kumtumikisha mwenzie kazi kutwa nzima bila kujali kama anachoka, ana kiu, au njaa, yeye anachojali ni kazi yake iende. Hata akisikia kuwa gari yake imepatwa na ajali, anachouliza kwanza, ‘gari yangu imeumia?’ na sio ‘wamepona waliokuwepo?’


Sala: Yesu wa Huruma, tunaomba utusamehe pale tuliposhindwa kuwahurumia wenzetu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *