JUMAMOSI: JUMA VI LA MWAKA
RANGI: NYEUPE
SIKUKUU
ZABURI: JUMA II
UKULU WA PETRO, MTUME
Utume: Wamewekwa mawakili wa Yesu Kristo hapa duniani. Hulinda na kueneza mafundisho ya Kristo alivyoagiza Kanisa lake. Petro ni mkubwa wa Mitume, Kanisa linaloongozwa na Mungu hata leo ili mahalifa wa Mt. Petro wasidanganyike wafundishe imani yetu kwa ushirikiano duniani.
SOMO 1: 1 Pet 5:1-4
Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye; lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiyari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo. Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi. Na Mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.
WIMBO WA KATIKATI: Zab. 23
- Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
(K) Bwana ndiye Mchugaji wangu, sitapungukiwa na kitu.
- Hunihuisha nafsi yangu, na kuniongoza,
Katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
Naam nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana wewe upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K) - Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K) - Hakika wema na fadhili zitanifuata,
Siku zote za maisha yangu,
nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
INJILI: Mt 16:13-19
Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.
MAMLAKA YOTE YATOKA KWA MUNGU: Leo Kanisa linaadhimisha sikukuu ya ‘Ukulu wa Petro’ hiki ni cheo alichopewa mtume Simoni baada ya kujibu kwa ufasaha swali la Yesu kuwa wanamwita yeye kuwa nani? Kwa sasa cheo hiki kinarithiwa na Baba Mtakatifu. Ni vizuri nasi tujiulize, tunamkiri Yesu kuwa nani? Je, tunakubali kuongozwa na uongozi halali wa Kanisa? Katika somo la kwanza, Petro anawasihi wale waliopewa jukumu la kusimamia taifa la Mungu wafanye kazi hiyo kwa upole, unyenyekevu, haki bila shuruti wala kulazimishwa wakijua wazi kuwa kazi hiyo ni ya majitoleo na si ya mshahara kama inavyodhaniwa. Tunaalikwa kuheshimu uongozi halali wa Kanisa kama mitume wengine walivyotoa heshima kwa Petro ili awajibie swali la Yesu. Kila mmoja wetu kuheshimu mipaka yake.
Sala: Bikira Maria Mama wa Kanisa, uwaombee viongozi wetu.