Masomo ya Misa Feb 21 Leave a comment

IJUMAA: JUMA VI LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA I
I

Mt. Petro Damiani, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Kuzaliwa: Mwaka 1007.
Utume: Aliishi maisha ya kitumwa nyumbani kwa ndugu zake. Akawa mkuu wa watawa na akajenga monasteri. Aliwasaidia mapapa wa Roma kwa maandishi juu ya teknolojia na sheria za Kanisa.
Kufariki: Mwaka 1072.

SOMO 1 Mwa 11:1-9
Nchi yote ilikuwa na lugha moja na usemi mmoja. Ikawa watu waliposafiri pande za mashariki waliona nchi tambarare katika nchi ya Shinari; wakakaa huko. Wakaambiana, Haya, na tufanye matofali tukayachome moto. Walikuwa na matofali badala ya mawe, na lami badala ya chokaa. Wakasema, Haya, na tujijengee mji, na mnara, na kilele chake kifike mbinguni, tujifanyie jina; ili tusipate kutawanyika usoni pa nchi yote. Bwana akashuka ili auone mji na mnara waliokuwa wakiujenga wanadamu. Bwana akasema, Tazama, watu hawa ni taifa moja, na lugha yao ni moja; na haya ndiyo wanayoanza kuyafanya, wala sasa hawatazuiliwa neno wanalokusudia kulifanya. Haya, na tushuke huko tuwachafulie usemi wao ili wasisikilizane maneno wao kwa wao. Basi Bwana akawatawanya kutoka huko waende usoni pa nchi yote; wakaacha kuujenga ule mji. Kwa sababu hiyo jina lake likaitwa Babeli; maana hapo ndipo Bwana alipoichafua lugha ya dunia yote; na kutoka huko Bwana akawatawanya waende usoni pa nchi yote.

WIMBO WA KATIKATI Zab 33:10-15

  1. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
    Huyatangua makusudi ya watu.
    Shauri la Bwana lasimama milele,
    Makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi.

(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.

  1. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao,
    Watu aliowachagua kuwa urithi wake.
    Toka mbinguni Bwana huchungulia,
    Huwatazama wanadamu wote pia. (K)
  2. Toka mahali pake aketipo,
    Huwaangalia wote wkaao duniani.
    Yeye aiumbaye mioyo yao wote
    Huzifikiri kazi zao zote. (K)

INJILI: Mk. 8: 34 – 9: 1
Yesu aliwaita mkutano pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, Mtu ye yote akitaka kunifuata na ajikane mwenyewe, ajitwike na msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza, na mtu atakayeiangamiza nafsi yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya Injili, huyu ataisalimisha. Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake? Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu. Akawaambia, Amin, nawaambia, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapouona ufalme wa Mungu umekuja kwa nguvu.


HUWEZI KUPAMBANA NA MUNGU: Tumeona katika somo la kwanza, wahusika wanakubaliana wajenge mnara kuelekea juu ili kufika mbinguni, hii ni sawa na kupambana na Mungu, kumsahihisha Mungu kwamba amefanya kosa kutuumba na kutuweka duniani. Tumeona jinsi Mungu alivyowasambaratisha. Na hata katika Injili, Kristo anasema, kuwa mfuasi wake lazima kujikana, kubeba msalaba na kumfuata na si vinginevyo, kinyume na hili ni kupambana na Mungu. Tumeshashuhudia watu walioumbwa kama wanaume wanataka kujibadili na kuwa wanawake na wanawake kuwa kama wanaume, walio na rangi ya maji ya kunde wanataka wawe weupe zaidi, walio na makalio au maziwa/matiti ya kawaida, wanataka eti yawe makubwa kwa kujidunga sindano au kumeza vidonge (maendeleo ya sayansi yametufikisha hapo). Huko ni kupambana na Mungu, ni kutomfuata Yesu bali kufuata vionjo vyetu.


Sala: Baba wa Mbinguni, tunaomba utujalie tuweze kujikubali na kufanya mapenzi yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *