Masomo ya Misa Feb 20 Leave a comment

IJUMAA JUMA VI LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA II

Mwenyeheri Yasinta
Kuzaliwa: Mwaka 1910.
Utume: Alikuwa ni mmoja kati ya watoto wa 3 wa Fatima, ambao walisema waliona matamshi matatu ya Malaika wa Amani. Alijiamini sana juu ya haja ya kuokoa wenye dhambi kwa njia ya uhalifu na dhabihu kama Bikira Maria alivyowaambia watoto kufanya.
Kufariki: Mwaka 1920.

SOMO I: Mwa. 9:1-13
Mungu alimbariki Nuhu na wanawe, akawaambia, zaeni, mkaongozeke, mkaijaze nchi. Kila mnyama katika nchi atawaogopa ninyi na kuwahofu, na kila ndege wa angani; pamoja na vitu vyote vilivyojaa katika ardhi, na samaki wote wa baharini; vimetiwa mikononi mwenu. Kila kiendacho kilicho hai kitakuwa chakula chenu, kama nilivyowapa mboga za majani, kadhalika nawapeni hivi vyote. Bali nyama pamoja na uhai, yaani, damu yake, msile. Hakika damu yenu ya uhai wenu nitaitaka; na kwa mkono wa kila mnyama nitaitaka; na kwa mkono wa mwanadamu, kwa mkono wa ndugu ya mtu nitataka uhai wa mwanadamu. Atakayemwaga damu ya mwanadamu, damu yake huyo itamwagwa na wanadamu; maana kwa mfano wake Mungu alimfanya mwanadamu. Nanyi zaeni, mkaongezeke; zaeni sana katika nchi, mkaongezeke ndani yake. Mungu akamwambia Nuhu, na wanawe pamoja naye, akisema, mimi, tazama, nalithibitisha agano langu nanyi; tena na uzao wenu baada yenu; tena na kila kiumbe kilicho hai kilichoko pamoja nanyi, ndege, na mnyama wa kufugwa, na kila mnyama wa mwitu katika nchi pamoja nanyi; wote wanaotoka katika safina, hata kila kilicho hai katika nchi. Na agano langu nitalithibitisha nanyi; wala kila chenye mwili hakitafutwa tena kwa maji ya gharika; wala hakutakuwa tena na gharika, baada ya hayo, kuiharibu nchi. Mungu akasema, hii ndio ishara ya agano nifanyalo kati yangu nanyi, na kila kiumbe hai kilichoko pamoja nanyi, kwa vizazi vyote hata milele; mimi nauweka upinde wangu winguni, nao utakuwa ni ishara ya agano kati yangu na nchi.

WIMBO WA KATIKATI Zab. 102: 15-20, 28 ,21-22

  1. Mataifa wataliogopa jina la Bwana
    Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
    Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni,
    Atakapoonekana katika utukufu wake,
    Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa,
    Asiyadharau maombi yao.
    (K) Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi.
  2. Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo,
    Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
    Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu,
    Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi
    Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa,
    Na kuwafungua walioandikiwa kufa. (K)
  3. Wana wa watumishi wako watakaa,
    Na wazao wataimarishwa mbele zako.
    Watu walitangaze jina la Bwana katika Sayuni,
    Na sifa zake katika Yerusalemu.
    Pindi mataifa watakapokusanyika pamoja,
    Falme nazo ili kumtumikia Bwana. (K)

INJILI: Mk. 8:27-33
Siku ile Yesu alitoka kwa wanafunzi wake, wakaenda kwenye vijiji vya Kaisaria-Filipi; na njiani akawauliza wanafunzi wake, akasema, watu huninena kuwa mimi ni nani? Wakamjibu, Yohane Mbatizaji, wengine Eliya; wengine, Mmojawapo wa manabii. Naye akawauliza, Na ninyi mnasema ya kuwa mimi ni nani? Petro akamjibu, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo. Akawaonya wasimwambie mtu habari zake. Akaanza kuwafundisha kwamba imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa na baada ya siku tatu kufufuka. Naye alikuwa akinena neno hilo waziwazi. Petro akamchukua, akaanza kumkemea. Akageuka, akawatazama wanafunzi wake, akamkemea Petro, akasema, Nenda nyuma yangu, Shetani; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu.


UHAI NI WA MUNGU MWENYEWE: Mungu baada ya kuumba vyote na mwanadamu, alimpa mwanadamu mamlaka ya kutawala vyote na kuzaa ili kuijaza dunia. Katika vitu alivyomsisitizia mwanadamu ni kutomwaga damu ya binadamu mwenzake. Tunaposhuhudia umwagaji damu sehemu mbalimbali duniani, ni kuwa mwanadamu amesahau sharti hili na imeleta madhara makubwa duniani. Katika Injili, Yesu anapowauliza mitume wake wanasema kuwa yeye ni nani, tunaona wanaacha jukumu hilo kwa Petro kujibu badala yao kwa vile ndo alikuwa kiongozi wao. Kuheshimu mamlaka halali ni jambo la heri. Tunapomchagua kiongozi tuamini kuwa anatuwakilisha vizuri kwa niaba yetu na tumpe ushirikiano na mazingira mazuri ya yeye kutimiza wajibu huo. Kuna wengine tunaingilia majukumu ya viongozi na kuleta vurugu katika jamii.
Sala: Tunawaombea viongozi wetu wa Kanisa na Serikali ili watimize wajibu wao kwa haki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *