Masomo ya Misa Februari 10 Leave a comment

JUMATATU: JUMA V LA MWAKA
RANGI: NYEUPE
KUMBUKUMBU
ZABURI: JUMA I

Mt. Skolastika, Bikira (480-547)
Alikuwa pacha na Mt. Benedikto walizaliwa huko Norsia (Italia)
Utume: Mt. Benedikto na Mt. Skolastika walijitolea kwa Mungu. Mt. Benedikto alijenga monasteri ya Monte Kasino.

SOMO 1. Mwa 1:1-19
Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji. Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru. Mungu akaiona nuru ya kuwa ni njema; Mungu akatenga nuru na giza. Mungu akaiita nuru mchana, na giza akaliita usiku. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku moja. Mungu akasema, na iwe anga katikati ya maji, likayatenge maji na maji. Mungu akalifanya anga, akayatenga yale maji yaliyo juu ya anga na yale maji yaliyo chini ya anga; ikawa hivyo. Mungu akaliita lile anga mbingu. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya pili. Mungu akasema, maji yaliyo chini ya mbingu na yakusanyike pamoja, ili pakavu paonekane; ikawa hivyo. Mungu akapaita pale pakavu Nchi. Na makusanyiko ya maji akayaita Bahari; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Mungu akasema, nchi na itoe majani, mche utoao mbegu na mti wa matunda uzaao matunda kwa jinsi yake, ambao mbegu zake zimo ndani yake, kwa jinsi yake; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya tatu. Mungu akasema, na iwe mianga katika anga la mbingu ili itenge kati ya mchana na usiku; nayo iwe ndio dalili na majira ya siku na miaka; tena iwe ndiyo mianga katika anga la mbingu, itie nuru juu na nchi; ikawa hivyo. Mungu akafanya mianga miwili mikubwa, ule mkubwa utawale mchana, na ule mdogo utawale usiku; akafanya na nyota pia. Mungu akaiweka katika anga la mbingu, itie nuru juu ya nchi na kuutawala mchana na usiku kutenga nuru na giza; Mungu akaona ya kuwa ni vyema. Ikawa jioni ikawa asubuhi, siku ya nne.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 104:1-2, 5-6, 10, 12, 24. 35

  1. Ee Nafsi yangu, umhimidi Bwana,
    Wewe, Bwana, Mungu wangu, amejifanya mkuu sana.
    Umejivika heshima na adhama,
    Umejivika nuru kama vazi.

(K) Bwana na ayafurahie matendo yake.

  1. Uliiweka juu ya misingi yake,
    Isitikisike milele,
    Uliifunika kwa vilindi kama kwa vazi,
    Maji yalikuwa yakisimama juu ya milima. (K)
  2. Hupeleka chemchemi katika mabonde;
    Zapita kati ya milima,
    Kando kando hukaa ndege wa angani,
    Kati ya matawi hutoa sauti zao. (K)
  3. Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
    Kwa hekima umevifanya vyote pia,
    Dunia imejaa mali zako.
    Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. (K)

INJILI. Mk 6:53-56
Yesu na wanafunzi wake walipokwisha kuvuka, walifika nchi ya Genezareti, wakatia nanga. Nao wakiisha kutoka mashuani, mara watu walimtambua, wakaenda mbio, wakizunguka nchi ile yote, wakaanza kuwachukua vitandani walio hawawezi, kwenda kila mahali waliposikia kwamba yupo. Na kila alikokwenda, aliingia vijijini, au mijini, au mashambani, wakawaweka wagonjwa sokoni, wakamsihi waguse ngaa pindo la vazi lake; nao wote waliomgusa wakapona.

TAFAKARI
MSAADA KWA MWINGINE NI BARAKA KWAKO PIA: Upendo, huruma na msaada wa Yesu ulikuwa huwezi kujificha, hata alipotaka kuwa faragha ilimwia vigumu. Watu walikuwa na shida nyingi na zilitatuliwa na Yesu. Tunaona watu wanawapeleka wagonjwa kwa Yesu ili awaponye. Ni jambo la kujiuliza, nilishawasaidia wangapi kupata msaada au huruma ya Kristo? Tuko ambao tunawakimbia wenye shida, tunaona kuwasaidia ni kupoteza muda, tunatumia misemo wasemao vijana wa siku hizi “apambane na hali yake.” Tunaona kama vile ni makosa yao kuwa katika shida na kwamba sisi hatutakaa tupate shida. Waswahili wanasema ‘leo kwangu kesho kwako’. Kumbe Ukristo wetu una maana pale tunaposaidiana.

Sala: Mungu Baba tupe neema ya kuwahurumia na kuwasaidia wenzetu walio katika taabu na dhiki.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *