Masomo ya Misa Februari 8 Leave a comment

JUMAMOSI: JUMA IV LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA I
V

Mt. Hieromino Emiliano Padri
Utume: Alifundisha Filosofia na alijifunza sheria za kanisa. Alihubiri kwa uhodari mkubwa na kufundisha watu huko Hispania kwenye mchanganyiko wa Waarabu na Waislamu. Wakristo waliimarishwa imani zao na maadili yaliyowaongoza Waislamu.
Kufariki: Mwaka 1275.

SOMO 1. Ebr 13:15-17, 20-21
Kwa njia yake Yesu tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake. Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu. Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi. Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu, awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake; naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 23:1-6

  1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
    Sitapungukiwa na kitu.
    Katika malisho ya majani mabishi hunilaza,
    Kando ya maji ya utulivu huniongoza,
    Huniuhisha nafsi yangu.

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu sitapungukiwa na kitu.

  1. Aliniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake.
    Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
    Sitaogopa mabaya,
    Kwa maana Wewe upo pamoja nami.
    Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K)
  2. Waandaa meza mbele yangu
    Machoni pa watesi wangu.
    Umenipaka mafuta kichwani pangu,
    Na kikombe changu kinafurika. (K)
  3. Hakika wema na fadhili zitanifuata
    Siku zote za maisha yangu;
    Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

INJILI. Mk 6:30-34
Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya, na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.

TAFAKARI
MAPUMZIKO NI MUHIMU: Ukisoma kitabu cha Mhubiri sura ya 3 anasema vizuri kuwa ‘kila jambo na wakati wake’. Miili yetu tumeumbwa kwa namna ambayo nayo inachoka na inahitaji mapumziko wakati mwingie. Yesu kwa kutambua hili anawaelekeza mitume wake wapate muda wa kupumzika baada ya uchovu wa kazi ili kupata nguvu mpya, kupata muda wa kujiandaa tena vizuri, Waingereza wanasema ‘refreshing the mind’ kupumzisha ubongo upumue, hata computer kuna wakati isipopumzishwa inagoma. Kuna wakati unakuta mtu anazama kwenye utume hivyo kwamba hana muda wa kupumzika wala kula hadi afya inadorora, anadhani kuwa bila yeye labda utume huo hutaenda na kutokana na kuchoka haraka anajikuta anafanya utume wake muda mfupi kuliko ilivyotarajiwa, anachoka mapema na hata kupelekea kufa. Tuone leo umuhimu wa mapumziko, sio ya kupitiliza bali ya kiasi. Tuwe na faragha na Yesu pia.

Sala: Yesu mpole, tuwezeshe kutumia vyema muda wetu wa utume.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *