Masomo ya Misa Alhamisi 6 Leave a comment

JUMATANO: JUMA IV LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA I
V

Wat. Paulo Miki na Wenzake, Mashahidi
Utume: Alikuwa padre wa Shirika la Majesuiti, alihubiri injili kwa bidii na ufanisi. Alikamatwa 1596 na wenzake 26 Wakatoliki na kuteswa.

SOMO 1. Ebr 12:18-19, 21-24
Ndugu zangu hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lo lote lingine. Na hayo yaliyoonekana jinsi yalivyokuwa ya kutisha, hata Musa akasema, nimeshikwa na hofu na kutetemeka. Bali ninyi mmeufikilia mlima Sioni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 48:1-2, 8-10

  1. Bwana ndiye aliye mkuu,
    Na mwenye kusifiwa sana,
    Katika mji wa Mungu wetu.
    Katika mlima wake mtakatifu.
    Kuinuka kwake ni mzuri sana,
    Ni furaha ya dunia yote.

(K) Tumezitafakari fadhili zako,
Ee Mungu, katikati ya hekalu lako.

  1. Mlima Sayuni pande za kaskazini,
    Mji wa mfalme mkuu.
    Mungu katika majumba yake
    Amejijulisha kuwa ngome. (K)
  2. Kama tulivyosikia, ndivyo tulivyoona,
    Katika mji wa Bwana wa majeshi,
    Mji wa Mungu wetu,
    Mungu ataufanya imara hata milele. (K)
  3. Tumezitafakari fadhili zako, Ee Mungu,
    Katikati ya hekalu lako.
    Kama lilivyo jina lako, Ee Mungu,
    Ndivyo na sifa yako hata miisho ya dunia,
    Mkono wako wa kuume umejaa haki. (K)

INJILI. Mk 6:7-13
Siku ile Yesu aliwaita wale Thenashara, akaanza kuwatuma wawili wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu; akawakataza wasichukue kitu cha njiani isipokuwa fimbo tu; wala mkate, wala mkoba, wala pesa za bindoni; lakini wajifungie viatu, akasema, Msivae kanzu mbili. Akawaambia, Mahali po pote mtakapoingia katika nyumba, kaeni humo hata mtakapotoka mahali pale. Na mahali po pote wasipowakaribisha ninyi wala kuwasikia, mtokapo huko, yakung’uteni mavumbi yaliyo chini ya miguu yenu, kuwa ushuhuda kwao. Wakatoka, wakahubiri kwamba watu watubu. Wakatoa pepo wengi, wakapaka mafuta watu wengi waliokuwa wagonjwa, wakawapoza.

TAFAKARI
JUKUMU LA KILA MKRISTO: Ukisoma sheria za Kanisa (Canon Law) namba 222 kifungu (a) inaeleza wazi kuwa, ni wajibu wa waamini kuhakikisha kuwa wanajitolea kwa sadaka zao ili Kanisa lisimame na mahitaji ya Kanisa na wahudumu wake yawepo. Hii ndio maana ya Kristo kuwakataza mitume wake “msichukue kitu cha njiani, wala mkate, wala pesa, wala kanzu mbili…” hii ina maana kuwa vitu hivyo vyote mtavikuta huko huko kwa wenyeji watakaowapokea, vitaandaliwa na wakaaji wa huko, msihangaike, nyie jiandaeni kuwahubiri watu Neno la Mungu. Leo wapendwa waamini tunakumbushwa wajibu wetu kwa Kanisa, hii inasaidia wahudumu wa Kanisa kutojishughulisha na mambo mengine kama biashara, ufugaji na kilimo na hivi kupelekea hata wao kusahau lile jambo msingi la kuwa wahubiri wa Neno. Kwa kusema hivi namaanisha kuzama hadi kukosa muda wa kulieneza Neno ni mbaya.

Sala: Ee Yesu uwajalie waamini wako neema ya kutimiza vyema wajibu wao wa kulitegemeza Kanisa lako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *