IJUMAA: JUMA III LA MWAKA
RANGI: NYEUPE
KUMBUKUMBU
ZABURI: JUMA III
Mt. Yohani Bosko Padre
Utume: Watu wengi wanamfahamu kwa jina lake la kipadre DON BOSKO maana yake Padre Bosko. Alipata upadre mwaka 1841. Ni mwanzilishi wa shirika la Wasalesiani wa Don Bosko na shirika la Masista wa Maria, Msaada wa Wakristu.
SOMO 1. Ebr 10:32-39
Zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu; pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendwa hivyo. Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang’anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo. Basi msiutupe ujasiri wetu, kwa maana una thawabu kuu. Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi. Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, yeye ajaye atakuja, wala hatakawia. Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.
WIMBO WA KATIKATI. Zab. 37: 3-6, 23-24, 39-40
Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana
Umkabidhi Bwana njia yako pia umtumaini
Naye atafanya;
Ataitokeza haki yako kama nuru,
Na hukumu yako kama adhuhuri. (K)
Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake.
Ajapojikwaa hataanguka chini,
Bwana humshika mkono na kumtegemeza. (K)
Wokovu wa wenye haki u na Bwana,
Yeye ni ngome yao wakati wa taabu.
Naye Bwana huwasaidia na kuwaopoa,
Huwaopoa na wasio haki na kuwaokoa,
Kwa kuwa wamemtumaini Yeye. (K)
INJILI. Mk 4:26-34
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi; akawa akilala na kuondoka, usiku na mchana, nayo mbegu ikamea na kukua, asivyojua yeye. Maana nchi huzaa yenyewe; kwanza jani, tena suke, kisha ngano pevu katika suke. Hata matunda yakiiva, mara hupeleka mundu, kwa kuwa mavuno yamefika. Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani? Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake. Kwa mifano mingi ya namna hii alikuwa akisema nao neno lake, kwa kadiri walivyoweza kulisikia; wala pasipo mfano hakusema nao; lakini akawaeleza wanafunzi wake mwenyewe mambo yote kwa faragha.
TAFAKARI
KUMJUA MUNGU HUJA TARATIBU: Nakumbuka wakati nikiwa mdogo nilipokuwa naenda kanisani, nilikuwa naangalia jinsi watu wakubwa walivyokuwa wakifanya ishara ya msalaba na nilikuwa nawafwatisha ili nami nielewe japo nilikuwa nakosea hadi nilipokuja kujikuta nimeshaweza kufanya ipasavyo bila kugundua ilikuwa lini hasa. Masuala ya kiimani ndivyo yalivyo, kuna wakati unajikuta Mungu anajifunua kwako kwa namna usiyoijua. Kristo amesema, huyu mkulima wakati amelala ile mbegu inaendelea kuota asivyojua. Nasi hali kadhalika, kuna mambo Mungu anayafunua kwetu kwa namna ambayo sisi hatuwezi kugundua. Kama tunavyoamini, kuwa Sakramenti ni ishara wazi ionekanayo ya neema isiyoonekana. Hiyo neema isiyoonekana inafanya kazi ndani yetu.
Sala: Yesu mwema tuwezesha tukuze imani yetu vyema.