Masomo ya Misa Januari 30 Leave a comment

ALHAMISI: JUMA III LA MWAKA
RANGI: KIJANI
KUMBUKUMBU YA HIYARI
ZABURI: JUMA III

Mt. Yasinta, Mtawa (1640)
Habari za Mt. Yasinta zinashangaza sana kuliko masimulizi mengine kuhusu maisha ya watakatifu. Alijitoa kikamilifu katika maisha ya utawa, kisha akavunja kanuni wazi wazi hata kuwakwaza watawa wenzake. Halafu anaongoka na kuanza kuishi vizuri kitawa lakini anarudia maishayake ya zamani. Mwishowe anapona udhaifu na kupokea upya neema ya Mungu.

SOMO1. Ebr 10:19-25
Ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu, njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake; na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu; na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya; tumeoshwa miili kwa maji safi. Na tulishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu; tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri; wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 24: 1-6
Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia ya wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya miti ya maji aliithibitisha.

(K) Hiki ndicho kizazi cha wautafutao uso wako, Ee Bwana.

Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Mtu aliye na moyo safi na moyo mweupe
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili,
Wala hakuapa kwa hila. (K)

Atapokea baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

INJILI. Mk 4:21-25
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Mwaonaje? Taa huja ili kuwekwa chini ya pishi, au mvunguni? Si kuwekwa juu ya kiango? Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi. Mtu akiwa na masikio ya kusikilia, na asikie. Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa. Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa.

TAFAKARI
JAMBO JEMA SI LA KUFICHA: Mfano anaotoa Yesu leo juu ya taa kuwekwa juu ya kiango ili iwaangaze waliomo ndani, ni ujumbe kuwa jambo jema linatakiwa liwekwe hadharani ili wengine nao waweze kulifaidi na kujifunza kama watu wanavyofaidi mwanga wa taa. Kuweka taa uvunguni ni sawa na kuficha uzuri wa jema ili wengine wasifaidi. Tuko ambao hatupendi yale mema na tujuayo aliyotufunulia Mungu wengine wayafaidi, tunayaficha, hatuyaweki wazi, tunaona kuwa labda wakiyafaidi tutapungukiwa kumbe ni kinyume chake, pale unaposhirikisha mwingine jambo unalolifahamu ndipo nawe unazidi kunufaika na hata kuelewa zaidi.

Sala: Kwa ubatizo wetu tulipewa mshumaa uwakao, tudumu daima kuwa mwanga kwa wengine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *