Januari 25 Leave a comment

JUMATANO: JUMA II
RANGI: NYEUPE
SIKUKUU
KUONGOKA KWA PAULO MTUME

SOMO 1. Mdo  22:3-16

Paulo aliwaambia makutano, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihada kwa Mungu kama nyinyi nyote mlivyo leo hivi; Nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwauwa, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake. Kama kuhani mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe.
Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Nikaanguka chini, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi. Na wale waliokuwa pamoja nami waliiona ile nuru, lakini hawakuisikia ile sauti ya yule aliyesema nami. Nikasema, Nifanye nini, Bwana? Bwana akaniambia, Simama, uingie Dameski, na huko utaambiwa habari za mambo yote yaliyoamriwa uyafanye. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski. Basi mtu mmoja, Anania, mtauwa kwa kuifuata sheria, aliyeshuhudiwa wema na Wayahudi wote waliokaa huko, akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Basi sasa, unakawilia nini? Simama, Ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake.

WIMBO WA KATIKATI. Zab.  117:1-2

Aleluya!
Enyi mataifa yote, msifuni Bwana,
Enyi watu wote, mhimidini.

(K) Enendeni ulimwenguni mwote,
mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe.


Maana fadhili zake kwetu sisi ni kuu,
Na uaminifu wa Bwana ni wa milele. (K)

INJILI. Mk 16:15-18

Yesu alionekana na wale kumi na mmoja, akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihuburi Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya.

TAFAKARI

MABADILIKO YANAWEZEKANA: Kanisa leo linasherehekea sikukuu ya kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, huyu ndiye aliyejulikana kama Sauli, alikuwa anaogopeka sana na aliwatesa sana Wakristo wa kwanza ili wamuasi Mungu, hakulipenda Kanisa. Lakini Kristo kwa mpango wake anamtokea na kumjaza neema ya kumbadilisha kwa kazi yake, kama somo la kwanza lilivyoeleza. Injili imeeleza juu ya utume waliokabidhiwa mitume ambao ndio pia Paulo alikabidhiwa. Tukubali kubadilika, tusipende kung’ang’ania tabia mbaya, tuone kuwa Mungu anapenda mabadiliko yenye mahusiano mazuri na yeye. Wapo Wakristo wenye tabia ambazo sizo na ukitaka kuwashauri ili wabadilike wanajitetea kuwa Mungu kawaumba hivyo, kitu ambacho si kweli.

Sala: Mtakatifu Paulo tuombee kwa Mungu ili tuweze kukubali mabadiliko ya mienendo yetu mibaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *