IJUMAA: JUMA II
RANGI: NYEUPE
KUMBUKUMBU
Mt. Fransisko wa Sale, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
SOMO 1. Ebr 8:6-13
Kuhani wetu sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora. Maana kama lile la kwanza lingalikuwa halina upungufu, nafasi isingalitafutwa kwa lile la pili. Maana, awalaumupo, asema, Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nami nitawatimizia nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda agano jipya; halitakuwa kama agano lile nililoagana na baba zao, katika siku ile nilipowashika mikono yao niwatoe katika nchi ya Misri. Kwa sababu hawakudumu katika agano langu, mimi nami sikuwajali, asema Bwana. Maana hili ndilo agano nitakaloagana na nyumba ya Israeli baada ya siku zile asema Bwana; nitawapa sheria zangu katika nia zao, na katika mikono yao nitaziandika; nami nitakuwa Mungu kwao, nao watakuwa watu wangu. Nao hawatafundishana kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake, akisema, Mjue Bwana; kwa maana wote watanijua, tangu mdogo wao hata mkubwa wao. Kwa sababu nitawasamehe maovu yao, sitazikumbuka tena. Kwa kule kusema, Agano jipya, amelifanya lile la kwanza kuwa kuukuu na kuchakaa ki karibu na kutoweka.
WIMBO WA KATIKATI. Zab. 85:7, 9-13
Ee Bwana,utuonyeshe rehema zako,
Utupe wokovu wako.
Hakika wokovu wake u karibu na wamchao,
Utukufu ukae katika nchi yetu.
(K) Fadhili na kweli zimekutana.
Fadhili na kweli zimekutana,
Haki na amani zimebusiana.
Kweli imechipuka katika nchi,
Haki imechungulia kutoka mbinguni. (K)
Naam, Bwana atatoa kilicho chema,
Na nchi yetu itatoa mazao yake.
Haki itakwenda mbele zake,
Nayo itazifanya hatua zake kuwa njia. (K)
INJILI. Mk 3: 13-19
Yesu alipanda mlimani, akawaita aliowataka mwenyewe; wakamwendea. Akaweka watu kumi na wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya kutoa pepo. Akawaweka wale Thenashara; na Simoni akampa jina Petro; na Yakobo, mwana wa Zebedayo, na Yohane nduguye Yakobo, akawapa jina la Boanerge, maana yake, wana wa ngurumo; na Andrea, na Filipo, na Bartholomayo, na Mathayo, na Tomaso, na Yakobo wa Alfayo, na Tadayo, na Simoni Mkananayo, na Yuda Iskariote, ndiye aliyemsaliti.
TAFAKARI
WITO HAULAZIMISHWI: Leo tunaona Kristo anawateua mitume wake 12 kwa kazi ya kuinjilisha, anapowaita hawalazimishi, anawaacha wawe huru, tunaona hata mmoja wao anakuja kumsaliti. Kila mmoja wetu katika maisha yake ameitiwa utume fulani Yer 1:5 “kabla sijakuumba nalikujua, kabla hujatoka tumboni mwa mama yako nalikutakasa…” Kitendo cha Yesu kuwateua hawa wachache 12 ni wazi kuwa, hili wanaloenda kulifanya lilishakusudiwa tangu awali, leo hii ni muda tu umefika. Nasi tujitathimini, je, tunaishi lile ambalo kwalo tuliumbwa? Au tumeshasaliti utume au wito wetu! Tujue tutadaiwa kama tutaishi sivyo.
Sala: Mungu tupe neema ya kutambua wito wetu na kuitikia ipasavyo.