Jumamosi: Juma la I la Mwaka
Rangi: Kijani
Mtakatifu: Mt. Margareta wa Hungaria, Mtawa
SOMO 1. Ebr 4:12-16
Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo. Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. Basi, iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungamo yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.
WIMBO WA KATIKATI. Zab. 19: 7-9, 14
“Sheria ya Bwana ni kamilifu, huiburudisha nafsi:
Ushuhuda wa Bwana ni amini, humtia mjinga hekima.
(K) Wewe, Ee Bwana, unayo maneno ya uzima wa milele.
Maagizo ya Bwana ni ya adili, huufurahisha moyo.
Amri ya Bwana ni safi, huyatia macho nuru. (K)
Kicho cha Bwana ni kitakatifu, kinadumu milele.
Hukumu za Bwana ni kweli, zina haki kabisa. (K)
Maneno ya kinywa changu,
Na mawazo ya moyo wangu yapate kibali mbele zako,
Ee Bwana, mwamba wangu na mwokozi wangu. (K)”
INJILI. Mk 2: 13-17
Yesu alitoka, akaenda kando ya bahari, mkutano wote ukamwendea, akawafundisha. Hata alipokuwa akipita, akamwona Lawi wa Alfayo, ameketi forodhani, akamwambia, Nifuate. Akaondoka akamfuata. Hata alipokuwa ameketi chakulani nyumbani mwake, watoza ushuru wengi na wenye dhambi waliketi pamoja na Yesu na wanafunzi wake; kwa maana walikuwa wengi wakimfuata. Na waandishi na Mafarisayo walipomwona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi, waliwaambia wanafunzi wake, Mbona anakula pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi? Yesu aliposikia aliwaambia, Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi.
TAFAKARI
KAZI ZETU BILA MUNGU HAZINA MAANA: Leo tumeona Yesu anamwita mtu mwenye kazi yenye hadhi kubwa tu na anaiacha na kumfuata Yesu. Tunaloweza kujifunza hapa ni kuwa, kazi zetu na yote tufanyayo kama hayana muunganiko na Yesu ni kazi bure. Kuna watu wengine wanakuwa na kazi au shughuli fulani na zinawafanya wanamsahau Mungu, wanaona kuwa hizo kazi au shughuli ndio muhimu zaidi, wanazipa kipaumbele, wanaziabudu, wanaona ndio kila kitu. Yuko radhi hata Jumapili asiende kanisani ili tu ahakikishe anasimamia vyema kazi yake. Lawi wa Alfayo leo anatupa somo zito kuwa, Mungu apewe nafasi ya kwanza. Tusimezwe na malimwengu.
Sala: Tunaomba Bwana utupe ufahamu wa kukupa wewe nafasi ya kwanza katika maisha yetu.