Jumatano: Juma la I la Mwaka
Rangi: Nyeupe
Mtakatifu: Antoni wa Misri
SOMO 1. Ebr 4:1-5, 11
Ikiwa ikaliko ahadi ya kuingia katika raha yake, na tuogope, mmoja wenu asije akaonekana ameikosa. Maana ni kweli, sisi nasi tumehubiriwa Habari Njema vile vile kama hao. Lakini neno lile lililosikiwa halikuwafaa hao, kwa sababu halikuchanganyika na imani ndani yao waliosikia. Maana sisi tulioamini tunaingia katika raha ile; kama vile alivyosema, kama nilivyoapa kwa hasira yangu, hawataingia rahani mwangu ; ijapokuwa zile kazi zilimalizika tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Kwa maana ameinena siku ya saba, mahali fulani hivi, Mungu alistarehe siku ya saba, akaziacha kazi zake zote; na hapa napo, Hawataingia rahani mwangu. Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha ile, ili kwamba mtu ye yote asije akaanguka kwa mfano uo huo wa kuasi.
WIMBO WA KATIKATI. Zab. 78: 3-4, 6-8
“Mambo tuliyoyasikia na kuyafahamu,
Ambayo baba zetu walituambia,
Tukiwaambia kizazi kingine
Sifa za Bwana na nguvu zake.
(K) Msiyasahau matendo ya Mungu.
Wasimame na kuwaambia wana wao,
Wamwekee Mungu tumaini lao,
Wala wasiyasahau matendo ya Mungu,
Bali wazishike amri zake. (K)
Wasiwe kama baba zao,
Kizazi cha ukaidi na uasi,
Kizazi kisichojitengeneza moyo,
Wala roho yake haikuwa amini kwa Mungu. (K)”
INJILI. Mk 2: 1-12 au (Mt. 19: 16-26)
Wakati ule, Yesu aliingia tena Kapernaumu. Ikasikiwa ya kwamba Yesu alikuwa nyumbani. Wakakusanyika watu wengi, isibaki nafasi hata mlangoni; akawa akisema nao neno lake. Wakaja watu wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne. Na walipokuwa hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo; na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza. Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako. Na baadhi ya waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu? Mara Yesu akafahamu rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri hivi mioyoni mwenu? Vyepesi ni vipi, kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende? Lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo akamwambia yule mwenye kupooza), Nakuambia, Ondoka, ujitwike godoro lako, uende nyumbani kwako. Mara akaondoka, akajitwika godoro lake, akatoka mbele yao wote; hata wakastaajabu wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Namna hii hatujapata kuiona kamwe.
TAFAKARI
DAIMA TUSHIRIKI HURUMA YA MUNGU: Hawa watu tuliosikia katika Injili ambao walimwonea huruma huyu mwenzao aliyekuwa amepooza, wanatualika mimi na wewe tushiriki huruma ya Mungu kwa kuwasaidia wale wanaohitaji msaada wetu. Tumeona jinsi walivyohangaika hadi kutoboa dari, ni wazi walihitaji nyenzo nyingi hadi mhusika akapata hii huruma ya Mungu, vitu kama ngazi kwa ajili ya kupanda juu ya paa, nyundo ya kung’olea misumari ili kutoa bati, kamba ya kumshushia mgonjwa nk, yote hii ni mahangaiko kwa ajili ya huyu mgonjwa na hatujaelezwa kama ni ndugu yao au la, lakini kwa maelezo ya haraka haraka huenda hawakuwa na undugu naye. Tunaalikwa kumpenda mwanadamu mwenzetu bila kujali kama tuna undugu naye au la! Tuko ambao hata kama tunatoa msaada ni kwa wale tu ambao tuna undugu nao wa karibu na tena tunatoa kwa masharti na mipaka fulani, tukiona inatuletea usumbufu tunaacha. Tunatoa tu ile misaada milaini, myepesi, isiyochukua muda mwingi au gharama kubwa.
Sala: Tunaomba tujaliwe kipaji cha kutoa misaada kwa wahitaji bila kujibakiza.