Kumbukumbu
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4
Mt. Didas Wa Sevila, Mtawa (1400-1463)
Utume: Didas alizaliwa Hispani. Alitaka kujiunga na padre mtakatifu aliyeishi upweke. Baada ya miaka kadhaa aliingia utawa wa Mt. Fransisko, akawa bruda. Aliheshimiwa sana kwa moyo wake wa sala, bidii zake katika kutekeleza wajibu wake. Bruda Didas alijitolea kwa moyo kuwauguza wagonjwa na wengine walipona kwa miujiza.
SOMO 1: Flm 1:7-20
Nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. Kwa hiyo, nijapokuwa nina ujasiri katika Kristo kukuagiza likupasalo; lakini, kwa ajili ya upendo nakusihi, kwa kuwa ni kama nilivyo, Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo; ambaye zamani alikuwa hakufai, bali sasa akufaa sana, wewe na mimi pia; niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe. Na kama amekudhulumu, au unamwia kitu, ukiandike hicho juu yangu. Mimi Paulo nimeandika kwa mkono wangu mwenyewe, mimi nitalipa. Sikuambii kwamba nakuwia hata nafsi yako. Naam, ndugu yangu, nipate faida kwako katika Bwana; uniburudishe moyo wangu katika Kristo.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 146:7-10
“1. Bwana huishika kweli milele,
Huwafania hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula,
Hufungua waliofungwa.
(K) Heri ambaye Mungu wa Yakobo ni msaada wake.
- Bwana huwafumbua macho waliopofuka,
Bwana huwainua walioinama,
Bwana huwapenda wenye haki,
Huwahifadhi wageni. (K) - Huwategemeza yatima na mjane,
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi kwa kizazi. (K)”
INJILI: Lk 17:20-25
Yesu alipoulizwa na Mafarisayo, Ufalme wa Mungu utakuja lini? Aliwajibu akawaambia, Ufalme wa Mungu hauji kwa kuuchunguza; wala hawatasema, Tazama, upo huku, au, kule, kwa maana, tazama, ufalme wa Mungu umo ndani yenu. Akawaambia wanafunzi, Siku zitakuja mtakapotamani kuona siku moja katika siku zake Mwana wa Adamu, msiione. Tena watawaambia, Tazama, kule! Tazama, huku! Msiondoke mahali mlipo, wala msiwafuate; kwa kuwa, kama vile umeme umulikavyo toka upande huu chini ya mbingu hata upande huu chini ya mbingu, ndivyo atakavyokuwa Mwana wa Adamu katika siku yake. Lakini kwanza, hana budi kupata mateso mengi, na kukataliwa na kizazi hiki.
TAFAKARI
KADIRI DUNIA INAVYOZUNGUKA: Katika zama zote, imekuwa ni jambo rahisi na la kawaida kufikiri kwamba maisha yanaendelea tu kama kawaida na kuacha kuona kabisa au kuwaza kuhusu kazi ya Mungu na ahadi zake. Kwa watu walio wengi kila kitu kinaonekana kuwa cha kawaida kabisa, duka limejaa vitu vipya, madaktari wanafanya utabibu wao, barua pepe uliyotumwa imepokelewa, na makampuni yako tayari kwa biashara na wewe. Mambo yanaendelea tu kama kawaida. Lakini tusifikiri kwamba Mungu amesahau. Siku moja iwe ni hivi karibuni au baadae, hasira au utukufu wa Mungu vyote vitaonekana. Ufalme ule ambao umekuwa ukikua taratibu kama punje ya haradali katika parokia au kanisa, katika jumuiya ndogo ndogo, au katika chama cha kitume, utukufu huo utaonekana waziwazi, na ukweli kuhusu Mungu utajulikana na wote. Wito wetu siku ya leo ni kuwaendea wote ambao hawaujui upendo na huruma ya Mungu. Tuwasaidie wajiandae kwa ujio wake.
SALA: Ee Bwana utujalie tuone dalili chache za ufalme wako katika maisha yetu ya kila siku ili tujipatie hekima.