Kumbukumbu ya Hiyari
Nyeupe
Mt. Stanislausi Kostka, Mnovisi (1550-1568)
Utume: Alizaliwa Poland, na wazazi wa jamaa bora. Stanislaus na ndugu yake walienda Viena (Austria) wapate kujifunza kwa Mayesuiti. Stanislaus alimwita Bikira Maria mama yake, na hakukosa kusali rozari. Aliingia shirikani na kuanza malezi ya kiroho katika novisiati, aliugua sana akafa mwaka 1568.
SOMO 1. Tit 3:1-7
Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote. Maana hapo zamani sisi nasi tulikuwa hatuna akili, tulikuwa waasi, tumedanganywa, huku tukitumikia tamaa na anasa za namna nyingi, tukiishi katika uovu na husuda, tukichukiza na kuchukiana. Lakini wema wake mwokozi wetu Mungu, na upendo wake kwa wanadamu, ulipofunuliwa, ulituokoa; si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na roho mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 23: 1b-6
“1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza.
Huniuisha nafsi yangu.
(K) Bwana ndiwe mchungaji wangu.
- Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake,
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana Wewew upo pamoja nami,
Gongo lako na fimbo yako vyanifariji. (K) - Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa wetesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K) - Hakika wema na Fadhili zinanifuata
Siku zote za Maisha Maisha yangu;
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)
“
INJILI: Lk 17:11-19
Ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, Yesu alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya. Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali, wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu! Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria. Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.
TAFAKARI
PEMBEZONI MWA MAISHA: Wakoma kumi walipiga kelele wakiomba Yesu awarehemu. Pembezoni mwa maisha yetu, kwa mbali kidogo wanasimama wahitaji ambao Yesu anawapenda. Utafanya nini ili uwafikie watu hao? Wako watoto wa mitaani wanasimama katika makutano, kwenye taa za barabarani na katika vijiji vyetu maisha yanawakokota bila huruma. Wako makahaba katika miji yetu ambao ujana wao umeharibiwa hawana tena cha kufanya. Wako wakimbizi wasio na kazi ya kufanya. Wako wasio na makazi wametupwa mbali na nyumba zao, na kuzuiliwa na kanisa. Sauti ya kilio chao inasikika wazi kabisa, “Wakristo mturehemu…” Inawezekana ikawa rahisi tukaendelea na biashara zetu kama kawaida. Inawezekana tunaendelea na shughuli zetu za kila siku, wakati wako wengi wanaishi maisha ya kusikitisha, maisha ya umasikini na mateso. Kwa sababu kuna mahitaji makubwa na rasilimali ni chache, waamini tunapaswa kuomba maongozi ya mwenyezi Mungu na kumtegemea Yeye mwenyewe. Tafuta njia ya kuwasaidia iwe ni kupitia kanisa au wewe binafsi.
SALA: Bwana nisaidie kuona mahitaji ya wale wanaoteseka.