Kumbukumbu
Nyeupe
Zaburi: Juma 4
Mt. Martin Wa Tur, Askofu
(136-397)
Utume: Alikuwa mwanajeshi akiwa na miaka kumi na
mitano. Mwenendo wake jeshini ulielekea zaidi wa kitawa. Baadaye alikiri kuwa
yeye ni askari wa Yesu. Alibatizwa na kupewa shamba, huko akajenga monasteri,
kisha akapadrishwa. Mapadre wenzake na waamini walimchagua kuwa askofu.
Alijulikana sana kwa ajili ya mahubiri na miujiza yake.
SOMO 1: Tit 2:1-8, 11-14
Wewe nena mambo yapasayo mafundisho yenye uzima; ya kwamba wazee wawe wenye kiasi, wastahivu, wenye busara, wazima katika imani na katika upendo na katika saburi. Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema; ili wawatie wanawake vijana akili, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao; na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe. Vivyo hivyo na vijana waume uwaonye kuwa na kiasi; katika mambo yote ukijionyesha mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenyekupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Maana neema ya Mungu iwaokoao wanadamu wote imefunuliwa; nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; tukilitazamia tumaini lenye baraka na mafunuo ya utukufu wa Kristo Yesu, Mungu mkuu na mwokozi wetu; ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili yetu, ili atukomboe na maasi yote, na kujisafishia watu wawe milki yake mwenyewe, wale walio na juhudi katika matendo mema.
WIMBO WA KATIKATI: Zab 37:3-4, 18, 23, 27, 29
1. Umtumaini Bwana ukatende mema,
Ukae katika nchi, upendezwe na uaminifu.
Nawe utajifurahisha kwa Bwana,
Naye atakupa haja za moyo wako.
(K) Wokovu wa wenye haki una Bwana
2. Bwana anazijua siku za wakamilifu,
Na urithi wao utakuwa wa milele.
Hatua za mtu zaimarishwa na Bwana,
Naye aipenda njia yake. (K)
3. Jiepue na uovu, utende mema,
Na kukaa hata milele.
Wenye haki watairithi nchi,
Nao watakaa humo milele. (K)
INJILI. Lk 17: 7-10
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Ni nani kwenu mwenye mtumwa alimaye au achungaye ng’ombe, atakayemwambia mara arudipo kutoka shambani, Njoo upesi, keti, ule chakula? Je! hatamwambia, Nifanyie tayari chakula, nile; jifunge unitumikie, hata niishe kula na kunywa, ndipo nawe utakapokula na kunywa? Je! atampa asante yule mtumwa, kwa sababu ameyafanya aliyoagizwa? Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.
TAFAKARI
UJIRA WA MTUMWA: “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya.” Kila mmoja katika kipindi cha Yesu, alielewa vyema kazi ya mtumwa. Mtumwa alifanya kazi ile ambayo kwayo alinunuliwa. Bwana wake hakudaiwa kumshukuru kwa kazi aliyoifanya na wala mtumwa hakutarajia kupewa shukrani. Watu wengi wanapenda kutambulika na kusifiwa katika kila hatua wanayochukua kusaidia au kuwahudumia wengine. Utii na uaminifu ndio mwanzo na wajibu wa waamini. Pale ambapo waamini wanatafuta kusifiwa, na kupewa zawadi, wanakuwa wanajihudumia wenyewe na sio Mungu. Tuchunguze nia zetu. Tunatarajia nini pale tunapowahudumia au kuwasaidia wngine. Je! Tunatafuta kusifiwa, kuonekana, kupewa zawadi au tunawasaidia kwa sababu ni wajibu wetu na kwamba wao pia wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wanastahili kutendewa kwa heshima?
SALA: Ee Bwana utujalie tutimize wajibu wetu pasipo kungojea sifa, heshima au utukufu.