Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/10/2024
2024 OKTOBA 26: JUMAMOSI: JUMA LA 29 LA MWAKA
Mt. Evaristo, Papa na Shahidi
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I
SOMO 1. Efe 4:7-16
Kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. Hivyo husema, alipopaa juu aliteka mateka, akawapa wanadamu vipawa. Basi neno hilo, ‘Alipaa,’ maana yake ni nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini, za nchi? Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa; juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. Naye alitoa wengine kuwa mitume; na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti; na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo. Tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 122: 1-5
1. Nalifurahi waliponiambia, (K)”Nalifurahi waliponiambia, 2. Ee Yerusalemu uliyejengwa 3. Ushuhuda kwa Israeli, |
INJILI. Lk 13:1-9
Wakati huo walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, “Je! Mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu, ukawaua mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia, Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo.” Akanena mfano huu; “Mtu mmoja alikuwa na mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia mtunzaji wa shamba la mizabibu, ‘Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu, nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu?’ Akajibu akamwambia, ‘Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.’” |
TAFAKARI
KUHUSU MAISHA NA KIFO: Yesu anakanusha mawazo yaliyokuwa yakizagaa katika wakati wake kwamba ajali, au ukatili wa kibinadamu ni hukumu ya Mungu hasa kwa wadhambi. Kwa nini basi wengine wanakufa na wengine wanaishi? Yesu hakujibu swali hili badala yake anawaeleza kila mmoja hitaji lake la kufanya toba. Siku hizi ziko familia zinazoonja machugu ya kufiwa kutokana na ajali za barabarani, ndege, na majanga kama mafuriko, vimbunga, na ukatili unaofanywa na wanadamu wenzao. Watu hao wanashawishika kuuliza; Kwa nini haya yanatupata? Kwa nini katika familia yetu na sio kwa wale? Kana kwamba unataka watu wote wapatwe na yale unayopata wewe ndipo utaridhika. Na inawezekana tukapata wakati mgumu kuelewa nini sababu ya mateso haya yote na kwa nini tunapoteza ndugu zetu bila sababu. Yesu anatuonesha jibu la pekee yaani neema ya Mungu. Akajibu akamwambia, ‘Bwana, uuache mwaka huu nao, hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La, usipozaa, ndipo uukate.’” SALA: Bwana Yesu, utujalie moyo wa toba ili tuweze kubadilika na hivyo kuzaa matunda istahilivyo. |