Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/10/2024
2024 OKTOBA 21: JUMATATU: JUMA LA 29 LA MWAKA
Mt. Ursula
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma I
SOMO 1. Efe 2:1-10
Mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini Mungu, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda; hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na Kristo; yaani mmeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu. Ili katika zamani zinazokuja audhihirishe wingi wa neema yake upitao kiasi kwa wema wake kwetu sisi katika Kristo Yesu. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu; wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu. Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende matendo mema, ambayo tokea awali Mungu aliyatengeneza ili tuenende nayo. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 100
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; (K) Ndiye aliyetuumba, na sisi tu watu wake. 2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; 3. Ingieni malangoni mwake kwa kushukuru 4. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema; |
INJILI. Lk 12:13-21
Mtu mmoja katika mkutano alimwambia Yesu, “Mwalimu, mwambie ndugu yangu anigawie urithi wetu.” Akamwambia, “Mtu wewe, ni nani aliyeniweka mimi kuwa mwamuzi au mgawanyi juu yenu?” Akawaambia, “Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo.” Akawaambia mithali, akisema, “Shamba la mtu mmoja tajiri lilikuwa limezaa sana; akaanza kuwaza moyoni kwake, akisema, ‘Nifanyeje? Maana sina pa kuyaweka akiba mavuno yangu.’ Akasema, ‘Nitafanya hivi; nitazivunja ghala zangu, nijenge nyingine kubwa zaidi, na humo nitaweka nafaka yangu yote na vitu vyangu. Kisha, nitajiambia, Ee nafsi yangu, una vitu vyema vingi ulivyojiwekea akiba kwa miaka mingi; pumzika basi, ule, unywe, ufurahi.’ Lakini Mungu akamwambia, ‘Mpumbavu wewe, usiku huu wa leo wanataka roho yako! Na vitu ulivyojiwekea tayari vitakuwa vya nani?’ Ndivyo alivyo mtu ajiwekeaye nafsi yake akiba, asijitajirishe kwa Mungu.” |
TAFAKARI
ULAFI: Yesu anatutahadharisha kuhusu tamaa ya kuwa na mali. Ulafi unafuatilia chombo alichoazima mtu, ulafi unafuatilia shilingi tulishoshiriki kuitafuta, ulafi unafuatilia dakika moja tuliyofanya kazi, ulafi unafuatilia hata hundi tuliyoandika kuwasaidia wahitaji. Yesu anatuongoza katika njia ya ukarimu jambo ambalo ni adimu siku hizi. Tajiri tuliyemsikia katika mfano wa Bwana wetu Yesu Kristo anakufa kabla hajatumia kile alichojiwekea akiba. Tunapojiandaa kwa kustaafu, tunapojiandaa kwa maisha kabla ya kifo, ni jambo la hekima. Lakini kupuuzia maisha baada ya kifo ni janga. Kama tukijilimbikizia mali kusudi tujinufaishe mwenyewe, pasipokuwa na lengo la kuwasaidia wengine, tutaingia katika umilele mikono mtupu. Yesu anatupatia changamoto ya kufikiri na kutafakari mbele zaidi ya ulimwengu huu, mbele zaidi ya malengo ya hapa duniani, na kuyatumia yale aliyotupatia Mungu kwa ajili ya ufalme wake. Imani, ukarimu, na utii ni njia ya kujitajirisha kwa Mungu. SALA: Ee Bwana utuepushe na tamaa ya kujilimbikizia mali. |