Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/10/2024
2024 OKTOBA 19: JUMAMOSI: JUMA LA 28 LA MWAKA
Mt. Yohane wa Brebe na Isaaki Yog, Mapadre, na Wenzao Mashahidi/ Mt. Paulo wa Msalaba, Padre
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Tazama Sala ya Siku
SOMO 1. Efe 1:15-23
Tangu nilipopata habari za imani yenu katika Bwana Yesu, na pendo lenu kwa watakatifu wote, siachi kutoa shukrani kwa ajili yenu; nikiwakumbuka katika sala zangu, Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ufunuo katika kumjua yeye; macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo; na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo. Kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika Kristo alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho; juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote. |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 8:2-7
1. Wewe, Mungu, Bwana wetu, (K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi za mikono yako. 2. Nikiziangali mbingu zako, kazi ya vidole vyako, 3. Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu; |
INJILI. : Lk 12:8-12
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: “Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu; na mwenye kunikana mbele ya watu, huyo atakanwa mbele ya malaika wa Mungu. Na kila mtu atakayenena neno juu ya Mwana wa Adamu atasamehewa, bali aliyemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa. Na watakapowapeleka ninyi mbele ya masinagogi na maliwali na wenye mamlaka, msifadhaike kwa kuwaza maneno yenu jinsi mtakavyojibu au kusema; kwa kuwa Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kuyasema.” |
TAFAKARI.
KUKUBALI AU KUKATAA: Kumkubali Yesu kunahitaji utii kwake. Kuna wakati tunamkana Yesu tukiwa na matumaini kwamba hakuna anayejua kwamba sisi ni Wakristo. Tunagoma kuzungumzia lililo sawa, na kukaa kimya kuhusu uhusiano wetu na Mungu. Tunajifungamanisha na jamii na kuzipokea tamaduni zao kama tunu zisizo za kikristo. Kwa upande mwingine, tunamkiri Yesu pale tunapoishi maisha yaliyo na maadili safi. Tunapoishi maisha ya kumtukuza Mungu, tunapotafuta fursa ya kuwashirikisha wengine imani yetu, tunapowasaidia wahitaji na kusimamia haki, tunapokuwa na upendo, na tunapokiri uaminifu wetu kwa Kristo. Tunapotumia mali zetu kufanya kile Yesu anachotaka na sio matakwa yetu wenyewe tunamkiri Kristo. Kuzungumza mbele za watu kunaleta hofu kwa watu zaidi kuliko kitu kingine. Kwa hakika kutetea imani yetu mbele za watu kwamba sisi ni wa Kristo inaonekana inaaibisha, lakini Yesu anatuthibitishia akisema “Nami nawaambia, kila atakayenikiri mbele ya watu, Mwana wa Adamu naye atamkiri yeye mbele ya malaika wa Mungu.” Tusiogope kukiri imani yetu. SALA: Utujalie ujasiri wa kukukiri mbele za watu kuwa wewe ni Bwana na Mungu wetu. |