Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 02/10/2024

2024 OKTOBA 2: JUMATANO-JUMA LA 26 LA MWAKA

Malaika Walinzi
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Tazama Sala ya Siku

SOMO 1. Kut. 23:20-23 au (2. Tim 3: 14-17)

Bwana asema hivi: Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. itunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makosa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; nami nitawakatilia mbali.

WIMBO WA KATIKATI. Zab. 91: 1-6, 10-11 (K) 11

Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini.

(K). Amekuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.

Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;

Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri,

Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote

INJILI. Mt. 18: 1-5, 10

Wanafunzi wakamwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, ye yote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na ye yote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi; Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika wao mbinguni siku zote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.       

TAFAKARI

ULINZI NI WA MUHIMU KWETU: Tunaona kila mahali, viongozi mashuhuru huwa wanalindwa kwa ulinzi mkali na silaha nzito. Lakini pamoja na hayo yote, kuna wakati ulinzi huo bado unaonekana kutokuwa salama. Tarehe 13/7/2024 nchini Marekani, Taifa lenye ulinzi wa hali ya juu duniani, kuna kijana kwa jina Thomas Matthew Crooks, wakati rais mstaafu Dolald Trump akiwa katika kampeni zake za kuwania uraisi mjini Pennslvania, kijana alimfyatulia risasi kwa mbali ambazo zilipelekea rais mstaafu Donald Trump kuumia sikio lake la kulia, mtu mmoja kufariki na wengine kujeruhiwa. Nimetoa mfano huu ili sote tuweze kuelewa kuwa, ulinzi wetu wa kibinadamu bado sio wa kuaminika. Yesu katika injili anasema, watoto wadogo ulinzi wao unatokana na malaika wa Mbinguni, hivyo tuwe kama watoto. Leo tunapowaheshimu malaika walinzi, kila mmoja wetu anaye, basi tujitahidi tusiwaangushe, tuwatumie vizuri. Wao wanahusika kutoa mrejesho kwa Mungu, tushirikiane nao wasije wakarudi kwa Mungu mikono mitupu, wanatuombea na kutulinda. Wataumia sana kama hatutaenda Mbinguni, tuwe wasikivu kwao kama watoto wanavyokuwa wasikivu kwa wazazi/walezi wao.

Sala: Enyi Malaika walinzi, mtuombee ili daima tuwe wasikivu kwenu.