Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/10/2024
2024 OKTOBA 1: JUMANNE-JUMA LA 26 LA MWAKA
Mt. Teresia wa Mtoto Yesu, Bikira
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma II
SOMO 1. Ayu 3:1-3, 11-17, 20-23
Ayubu alifunua kinywa chake, na kuilaani siku yake. Ayubu akajibu, na kusema; naipotee mbali ile siku niliyozaliwa mimi, na ule usiku uliosema, mtoto mume ametungishwa mimba. Mbona si kufa mimi tokea mimbani? Mbona nisitoe roho hapo nilipotoka tumboni? Mbona hayo magoti kunipokea, au hayo maziwa, hata nikanyonya, maana hapo ningelala na kutulia; ningelala usingizi; na kupata kupumzika; pamoja na wafalme na washauri wa dunia, hao waliojijengea maganjoni; au pamoja na wakuu wenye dhahabu, waliozijaza fedha nyumba zao; au, kama kuzikwa mimba iliyoharibika, nisingekuwako; kama wachanga wasiouona mwanga kabisa. Huko waovu huacha kusumbua; huko nako hao waliochoka wapumzika. Mbona yeye aliye mashakani kupewa mwanga, na hao wenye uchungu rohoni kupewa uhai; ambao wangojea mauti, lakini hawayapati; na kuyachimbulia zaidi ya kutafuta hazina iliyositirika; ambao wafurahi mno, na kushangilia watakapoliona kaburi? Kwa nini mtu aliyezibiwa njia kupewa mwanga, ambaye Mungu amemzingira kwa ukigo? |
WIMBO WA KATIKATI. Zab 88: 2-8
1. Bwana, Mungu wa wokovu wangu, (K) Maombi yangu yafike mbele zako, Ee Bwana. 2. Maana nafsi yangu imeshiba taabu, 3. Miongoni mwao waliokufa nimetupwa, |
INJILI. Lk 9:51-56
Ilikuwa, siku za kupaa kwake zilipokuwa karibu kutimia, Yesu aliukaza uso wake kwenda Yerusalemu; akatuma wajumbe kutangulia mbele ya uso wake; wakaenda wakaingia katika kijiji cha Wasamaria, ili kumtengenezea mahali. Lakini wenyeji hawakumkaribisha kwa vile alivyouelekeza uso wake kwenda Yerusalemu. Wanafunzi wake Yakobo na Yohane walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize? Akawageukia akawakanya, wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine. |
TAFAKARI.
KUDUMU KATIKA MPANGO WA MUNGU NA KUKWEPA MOYO WA KISASI: Katika Injili tunajifunza mambo mawili yaani kudumu katika mpango wa Mungu na kukwepa moyo wa kisasi. Ingawa Yesu alijua kwamba atakumbana na mateso na kifo huko Yerusalemu, lakini aliyakaza macho yake kwenda huko. Namna hiyo ya kuchukua maamuzi inapaswa kuwa ndio tabia ya wakristo. Pale Mungu anapotupatia jambo la kufanya, tutembee kwa ujasiri kuelekea lengo hilo pasipo kuangalia ni matokeo gani mabaya tutakumbana nayo. Yakobo na Yohane walitaka kulipiza kisasi kwa vijiji vile ambavyo vilikataa kumkaribisha Yesu. Pale tunapojisikia tumekataliwa au kutendewa ubaya kwa kawaida tunajisikia vibaya na kutamani kulipa kisasi. Wakati mwingine tunafikiri jinsi ya kuwanyamazisha watu au makundi ya watu kwa kutumia njia mbali mbali au kwa kufuata mawazo mabaya ya watu fulani. Tukumbuke jambo moja kwamba hukumu na kisasi ni cha Mungu, kamwe usifikirie kutumia nguvu au mamlaka tuliyonayo katika kulipiza kisasi. SALA: Ee Mungu utuepushe na moyo wa kisasi. |