Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/09/2024

2024 SEPTEMBA 22: JUMATATU-JUMA LA 25 LA MWAKA

Mt. Pio wa Pietrelcina, Padre
Rangi: NYEUPE

Zaburi: Juma I

SOMO 1. Mit 3:27-34

Mwanangu, Usiwanyime watu mema yaliyo haki yao, ikiwa katika uwezo wa mkono wako kuyatenda. Usimwambie jirani yako, nenda, urudi halafu, na kesho nitakupa; nawe unacho kitu kile karibu nawe. Usiwaze mabaya juu ya jirani yako, ambaye anakaa karibu nawe na kujiona salama. Usishindane na mtu bila sababu, ikiwa hakukudhuru kwa lo lote. Usimhusudu mtu mwenye jeuri, wala usiichague mojawapo ya njia zake. Maana mtu mkaidi ni chukizo kwa Bwana, bali siri yake ni pamoja na wanyofu. Laana ya Bwana i katika nyumba ya waovu, bali huibariki maskani ya wenye haki. Hakika yake huwadharau wenye dharau, bali huwapa wanyenyekevu neema.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 15: 2-5

1. Ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu.
Ni mtu aendaye kwa ukamilifu,
Na kutenda haki, asemaye kweli kwa moyo wake
Asiyesingizia kwa ulimi wake.

(K) “Mtu aendaye kwa ukamilifu, atafanya maskani yake, katika kilima chako kitakatifu. “

2. Asiyemtendea mwenziwe mabaya,
Wala hakumsengenya jirani yake.
Machoni pake mtu asiyefaa hudhaauliwa,
Bali huwaheshimu wamchao Bwana.
Ingawa ameapa kwa hasira yake,
Hayabadili maneno yake. (K)

3. Hakutoa fedha yake apate kula riba,
Hakutwaa rushwa amwangamize asiye na hatia.
Mtu atendaye mambo hayo
Hataondoshwa milele. (K)

INJILI. Lk 8:16-18

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Hakuna mtu ambaye akiisha washa taa huifunika kwa chombo, au kuiweka uvunguni, bali huiweka juu ya kiango, ili waingiao wapate kuona nuru yake. Kwa maana hakuna neno lililositirika ambalo halitafunuliwa; wala lililofichwa ambalo halitajulikana na kutokea wazi. Jiangalieni basi jinsi msikiavyo; kwa kuwa mwenye kitu atapewa, na yule asiye na kitu atanyang’anywa hata kile ambacho anadhaniwa kuwa nacho.

TAFAKARI. 

TUNG’ARE KWA MWANGA WA KRISTO: Katika Agano la kale, Sehemu ya kitabu cha Mithali kinatoa ushauri wa maisha unaomsaidia mwanadamu kuishi katika mwanga kwa kuwapa watu mema ambayo ni mastahili na haki yao. Kumhudumia mhitaji kwa wakati bila usumbufu wa nenda rudi, kutowaza mabaya juu ya wengine, kuchagua moja ya njia za mtu jeuri ni chukizo kwa Bwana. Siri ya Bwana ipo katika unyoofu na huwapa wanyenyekevu neema. Kristo mwenyewe kwa unyenyekevu wake ni mwanga wa ulimwengu. Kwa mateso, kifo na ufufuko wake ametuangaza wote na kutukomboa kutoka katika giza la dhambi. Kwa maneno na matendo yake ametuonesha namna ya kuishi kama waana wa Mungu na kama mashuhuda wa ufalme wa Mungu. Baada ya kututoa katika utumwa wa ufalme wa giza na kutuingiza kwenye ufalme wa mwanga wa mwanae mpendwa inategemewa tuishi kwa kuakisi mwanga huo. Wito wetu wa ukristo unafungamanishwa na kung’ara katika mwanga wa Kristo. Hakutakuwa na maisha halisi ya ushuhuda wa kikristo kama tukiuficha huo mwanga.

SALA: Ee Bwana ufanye maisha yetu yawe mwanga wa kuwaangazie wengine wakufuate.