UKUU KATIKA UNYENYEKEVU WA KRISTO Kiongozi ni mmoja kati ya wanajamii ambaye ameaminiwa na jamii nzima kwa ajili ya kutoa dira, maelekezo na kuamrisha kwa ajili ya manufaa ya jamii nzima. Hakuna jamii inayokosa kiongozi na ikiwapo jamii hiyo basi huwa katika hali ya vurugu, ukosefu wa amani na utengano mkubwa kati ya mtu na mtu. Kiongozi huwekwa na wenzake si kwa ajili ya kujitanua na kuonesha ukuu wake bali kwa ajili ya kutumikia jamii yake na kuifanya kuwa bora zaidi. Katika uwanda wa demokrasia kiongozi hupewa uwezo wa watu wote na hivyo utendaji wake unapaswa kuakisi maana hiyo. Uwezo wa wanajamii unakusanywa na kujidhihirisha katika nafsi ya huyu anayechaguliwa. Hapa ndipo tunaiona maana ya neno demokrasia ikiwakilisha “uwezo au nguvu ya umma.” Kiongozi asiyetenda kudhihirisha ukweli huu anapingana na demokrasia hata kama amechaguliwa kwa demokrasia. Dominika hii tutafakari juu ya ukuu katika unyenyekevu wa Kristo, tunu ambayo ni muhimu kwa ajili ya kuwa kiongozi bora. Kiongozi bora ni yule aliye mfano wa Kristo ambaye amekuja si kwa ajili wa kutumikiwa bali kwa ajili ya kutumikia na kuitoa nafsi yake kuwa fidia kwa wote (rej. Mt 20:28) Kristo alikuwa anaanza kuwaelekeza wanafunzi wake kuelekea safari ya Yerusalemu ambako atapata maswahibu mbalimbali hadi kifo kwa ajili ya wokovu wetu. Aliona hiyo ni sehemu muhimu ambayo wanapaswa kuielewa ili kuwa viongozi wa kiroho wa watu. Kinyume chake wanafunzi wake hawakumwelewa. Wao wakizongwa na mawazo ya kibinadamu walibaki kushindana nani atakuwa mkubwa kati yao. Ni ipi tabia ya kiongozi bora kadiri ya mpango wa Mungu? Huyu ni yule anayekuwa “mtumishi wa wote.” Katika hali ya kawaida haya ni Mapinduzi ya kifikra kuhusiana na dhana ya uongozi. Hii ni kwa sababu mara nyingi watu wengi wananuia uongozi si kwa ajili ya kutumikia bali kutumikiwa na kujitanua wao binafsi kiutawala na kutafuta faida binafsi za kiuchumi. Namna hii ni kuichakachua maana halisi ya uongozi. Kristo anaifunua namna ya uongozi katika hali ya kujinyenyekeza kwa hatua mbalimbali. Wakati wa karamu ya mwisho aliwaosha miguu mitume wake na kuwaambia: “Ikiwa mimi niliye Bwana na Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo hivyo kutawadhana miguu ninyi kwa ninyi” (Yn 13:14). Hapo ndipo ulipo ukuu wa uongozi katika Kristo, yaani kujinyenyekeza na kujishusha katika namna ya utumishi. Ukuu wa namna ya kidunia unabadilisha maana ya uongozi. Kristo anatuelekeza leo huku akiwa amembeba mtoto mdogo kwamba: “mtu akimpokea mtoto mmoja wa namna hii kwa jina langu, anipokea mimi; na mtu akinipokea mimi, humpokea, si mimi, bali yeye aliyenituma.” Tuangalie umuhimu wa nafasi ya mzazi kwa mtoto na mategemeo ya mtoto kutoka kwa mzazi wake. Mtoto anaona wazi uwepo wake unawezeshwa na mzazi wake na mzazi anajisikia daima kupasika kumhudumia mtoto wake kwa mahitaji yote; anapasika kumfanya awe katika hali njema daima. Ni mfano muafaka wa namna kiongozi anavyopaswa kuwa mbele ya watu anaowaongoza. Ni katika hali ya kujiweka kama mtumishi ndipo tu utaweza kutimiza vema majukumu yako kama kiongozi. Mzazi hujisikia daima yu mtumishi kwa mtoto wake. Maelekeo haya ya kibinadamu hutufanya tuutafute uongozi si kwa ajili ya kutumikia wengine bali kutumikiwa na kuendelea kustawi katika ubinafsi wetu. Watu wengi wanatafuta madaraka na wakati mwingine kupitia njia za kidemokrasia lakini tutambue kuwa malengo hayo kama hayalengi katika ukweli wa kiuongozi ni kikwazo na kinyume na mpango wa Mungu. Waraka wa Mtakatifu Papa Yohane Paulo wa pili unatuambia: “Demokrasia ya kweli inakuwepo pale tu Taifa linapoongozwa na sheria katika misingi ya kweli ya dhana juu ya ubinadamu” (Centesimus Annus, n. 46). Uongozi wa kimabavu na namna za kumkandamiza mwanadamu mwenzako hupingana na mpango wa Mungu na huo si wito wa Mungu kwetu kwa ajili ya kuwa viongozi kwa ajili ya wengine. Hali ya kuitikia uongozi kadiri ya mpango wa Mungu inahitaji mtu mwadilifu kama tunayemsikia katika somo la kwanza. Uadilifu ni hali ya kuendana na matakwa ya Mungu; kuzitafuta njia zake na kuzishika katika maisha ya kila siku. Jamii ya mwanadamu mambo leo inakinzana na uadilifu huu. Zaburi ya 15 inamwelezea mtu mwadilifu katika ujumla wake kam mtu aliye karibu na Mungu, yu mkamilifu, ni mtu wa haki, ni mkweli, asiyesingizia, asiye mtendea mwenzake mabaya na asiye sengenya. Zaburi inaendelea kumpamba mwadilifu ikimwelezea kuwa ni yeye asiyechanganyana na wasio mcha Mungu, huwaheshimu wacha Mungu na mwenye msimamo. Pia ni mpinga rushwa na kamwe hatafuti kunyonya mwenzake. Sifa hizi ndizo zinapaswa kumpamba kiongozi bora na zitamuelekeza kutenda kadiri atakavyo Mungu. Mmoja anapotokea kunuia kupokea nafasi ya uongozi kadiri ya mapenzi ya Mungu hukumbana na ukinzani. Huu ni uthibitisho wa utawala wa dhambi katika jamii yetu. Kiongozi mwadilifu huonekana kuwa ni kikwazo kwa wale wanaotaka kupindisha taratibu na kutumia mianya ya uovu ili kujikusanyia zaidi na kuunyanyasa ubinadamu hasa walio wanyonge zaidi. Mmoja anapobaki katika uadilifu iwe ni sehemu za kazi, katika uwanja wa siasa, katika familia na wakati mwingine hata ndani ya Kanisa upinzani huwa mkubwa kama anaokumbana nao mwenye haki anayeelezewa katika somo la kwanza. Huyu atasukiwa ajali za namna nyingi ili hali tu aangamizwe na kutoweka na waovu waendelee kustawi katika uovu wao. Jamii inaonekana kana kwamba inabariki uongozi mbovu ambao unampora mwanadamu utu wake. Sisi Wakristo tunaitwa kupiga hatua moja mbele zaidi na kujivika namna ya Kristo ambayo hujionesha si katika mabavu na kutafuta kutumikiwa bali katika unyenyekevu. Tunapaswa kuwa taa inayoangaza jamii na kuitoa jamii katika giza. Mtume Yakobo anatupatia tahadhari kuwa vita magomvi na tamaa vinatoka katika tamaa zetu za kibinadamu. Tamaa hizi zinauua utu wetu na kutufanya kutenda kinyume na ubinadamu wetu. Anashangaa kwa kuuliza: “vita vyatoka wapi, na mapigano yaliyoko kati yenu yanatoka wapi?” Tunaona jinsi uchu wa ukuu na madaraka, uchu wa utajiri unavyouangamiza ubinadamu. Tunatenda mambo ya kuchukiza na yanayoondoa maana ya hadhi yetu. Hivyo anatukumbusha tujivike hekima itokayo kwa Mungu ambayo ni “safi, tena ni ya amani, ya upole, tayari kusikiliza maneno ya watu, imejaa rehema na matunda mema, haina fitina, haina unafiki.” Mahangaiko ya masikini, malalamiko ya mjane na kilio cha yatima kinamjia kila mmoja wetu leo hii. Wewe na mimi katika nafasi zetu mbalimbali za kijamii tunapewa fursa ya kuongoza na kuwafariji hawa wanaotafuta faraja. Mwaliko tunaopewa leo ni kumfuasa Kristo katika njia yake; si kukalia nafasi uliyonayo kwa ajili ya kutawala na kujitukuza binafsi bali tuitumie katika kumtukuza Mungu. Tunamtukuza Mungu pale tunapotimiza wajibu wetu kama itakiwavyo. Huo ndiyo wito wetu wetu Wakristo wa kuwa wa mwisho na kuwatumikia wote. Katika unyenyekevu wetu huo wa kikristo ndipo ilipo nguvu na ukuu wa Mungu.
SALA: Ee Bwana utujalie tutambue kwamba cheo ni dhamana na ukubwa ni utumishi.
|