Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/09/2024

2024 SEPTEMBA 9: JUMATATU-JUMA LA 23 LA MWAKA

Mt. Petro Claver
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

SOMO 1. 1 Kor 5:1-8

Habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye. Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo. Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwako kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo. Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu; kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu.  Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.

WIMBO WA KATIKATI. Zab 5:5-7, 12

1. Unawachukia wote watendao ubatili.
Utawaaribu wasema wasemao uongo;
Bwana humzira mwuaji na mwenye hila.

(K) Bwana, uniongoze kwa haki yako.

2. Maana huwi Mungu apendezwaye na ubaya;
Mtu mwovu hatakaa kwako;
Wajivunao hawatasimama mbele za macho yako. (K)

3. Nao wote wanaokukimbilia watafurahi;
Watapiga daima kelele za furaha.
Kwa kuwa Wewe unawahifadhi,
Walipendao jina lako watakufurahia. (K)

INJILI. Lk 6:6-11

Ilikuwa siku ya sabato nyingine Yesu aliingia katika sinagogi akafundisha; na mlikuwamo mtu ambaye mkono wake wa kuume umepooza. Na waandishi na Mafarisayo walikuwa wakimvizia, ili waone kwamba ataponya siku ya sabato; kusudi wapate neno la kumshitakia. Lakini yeye akayatambua mawazo yao, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Ondoka, simama katikati;” akaondoka akasimama. Ndipo Yesu akawaambia, “Nawauliza ninyi, Je! Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya; kuponya roho au kuangamiza?” Akawakazia macho wote pande zote, akamwambia yule mtu, “Nyosha mkono wako.” Akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena. Wakajawa na uchungu, wakashauriana wao kwa wao wamtendeje Yesu.

TAFAKARI

MWANADAMU TENDA WEMA WAKATI WOTE: Mwenyezi Mungu anawatembelea watu wake mara kwa mara akiwajulia hali, hawaachi wapweke. Siku nyingine ya Sabato, Yesu aliingia katika sunagogi, akafundisha. Mle ndani kulikuwa na mtu ambaye mkono wake ulikuwa umepooza, yaani mtu huyu alikuwa na ulemavu na mapungufu fulani ya kimsingi sana katika mwili wake. Yesu alijua mawazo ya mafarisayo na ya watu wote, akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, asimame katikati mahali ambapo kila mtu atamwona vizuri, yule mtu akaenda kusimama katikati. Yesu akawauliza swali la msingi, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuyaangamiza? Baada ya kuwatazama wote waliokuwa pale, akamwambia yule mtu aliyepooza mkono aunyooshe mkono wake, naye akafanya hivyo, na mkono wake ukawa mzima. Mwenyezi Mungu anaendelea kuwatembelea watu wake akiwafundisha, akiwaponya, akiwasamehe dhambi, akifukuza pepo na kuwaweka huru pale walipokandamizwa kwa namna mbalimbali. 

SALA: Ee Yesu utupe neema ya kutenda mema pasipo kuogopa macho na maneno ya watu.