Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 01/09/2024
2024 SEPTEMBA 2: JUMATATU-JUMA LA 22 LA MWAKA
Mt. Yusto, Askofu na Mtawa
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 2
Somo 1. 1 Kor 2:1-5
Ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima. Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa. Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi. Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu, ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 119:97-102
1. Sheria yako naipenda mno ajabu, (K) Sheria yako, Ee Bwana, naipenda mno ajabu. 2. Ninazo akili kuliko wanafunzi wangu wote 3. Nimeiepusha miguu yang una kila njia mbaya, |
Injili. Lk 4:16-30
Yesu alienda Nazareti, hapo alipolelewa; na siku ya sabato akaingia katika sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, akasimama ili asome. Akapewa chuo cha nabii Isaya, akakifungua chuo, akatafuta mahali palipoandikwa. Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Akakifunga chuo, akamrudishia mtumishi, akaketi; na watu wote waliokuwamo katika sinagogi wakamkazia macho. Akaanza kuwaambia, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu.” Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake. Wakasema, “Huyu siye mwana wa Yusufu?” Akawaambia, “Hapana shaka mtaniambia mithali hii, ‘Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako mwenyewe.’” Akasema, “Amin, nawaambia ya kuwa, hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.” Wakajaa ghadhabu wote waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo. Wakaondoka wakamtoa nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu yake, wapate kumtupa chini; lakini yeye alipita katikati yao, akaenda zake. |
TAFAKARI
TUJENGEKE KATIKA HEKIMA YA KIMUNGU, IMANI: Bwana Yesu anahubiri nyumbani kwao Nazareti lakini mahubiri yake hayakupokelewa kwa hamasa kwa sababu ya watu kukosa imani na kudharau mambo ya Kimungu. Bila shaka wanamwona Yesu kama mtoto wa Maria na Yosefu lakini hawakutilia maanani bado kuwa alikuwa ni Mwana wa Mungu. Kuendelea kuwafundisha, Kristo anatoa mfano wa zamani za Elisha ambapo kulikuwa na wagonjwa wengi wa ukoma lakini ni Naamani tu ndiye aliyetakaswa kwa sababu ya imani yake. Watu wanakosa imani na kumdharau Mungu aliyejifanya mwanadamu na hivyo wanashidwa kuiona miujiza na mema aliyokuwa akiyatenda ikiwa ni pamoja na kuponya wagonjwa, viwete nk. Mtakatifu Paulo anawaandikia Wakorintho akiwakumbusha kuwa hakuwahubiria akitumia hekima ya wanadamu bali katika nguvu za mwenyezi Mungu. SALA: Tumwombe Mungu atujalie hekima ya kuupokea ujumbe wake. |