SHERIA YA KRISTO INAJENGA UTU MPYA Sheria ni taratibu ambazo jamii fulani mahsusi hujiwekea kwa ajili ya ustawi wa jamii husika. Taratibu hizi zinapaswa kuwa na lengo la kumbadili mtu na kumjenga kadiri ya roho ya sheria husika na hivyo kuendana na jamii au kundi lililojiwekea sheria hizo. Mmoja anapobaki katika kutekeleza sheria bila mabadiliko kutoka ndani anageuka kuwa ni mtumwa wa sheria husika. Hivyo, ni jambo jema na la kufaa kuangalia mafaa ya sheria unayowekea. Kwa maneno mengine sheria haiwezi kupata maana kamili au sifa za sheria kama hainuii katika kumjenga mtu mmoja mmoja kiutu kwa ufanisi wa jamii nzima. Moja ya tabia ya sheria kadiri ya tafsiri ya Mtakatifu Thomaso wa Akwino ni kuwa kitu kinachoeleweka na kuleta maana (ratio ordinatio). Kitu kinachoeleweka na kueleta maana kitamjenga mtu na kumtambulisha haiba yake huku kikimtofautisha na watu wengine. Masomo ya Dominika ya leo yanatuletea mbele yetu dhana ya sheria. Sheria hii inayozungumziwa ni sheria ya Mungu ambayo kwayo sisi wanadamu tunajitambulisha kuwa wana wa Mungu. Mungu ni muumbaji wetu. Yeye ndiye asili yetu na ametujengea kanuni za kuutambulisha utu wetu. Utii wetu kwa sheria zake ni uhakikisho wa kujitambulisha haiba yetu barabara. Neno la Mungu linatoa maelekezo matatu. Kwanza ni “sikiliza.” Mungu anatuagiza kusikiliza amri zake, yaani kuifungua mioyo yetu na kuijaza hekima yake ndani mwetu. Kusilikiza kunatufanya kulipokea neno lake na kulifanya kuwa chachu ya utendaji wetu. Pili ni “mzitende.” Tendo la kusikiliza na kujimithilisha na maagizo au mapenzi ya Mungu kwetu linatupeleka katika utendaji. Utandaji huo ndiyo unatutambulisha na kutuingiza katika kundi la wana wa Mungu. Tatu tunaonywa tukiambiwa “msiongeze …wala msilipunguze.” Ni angalizo kuepa kuweka hekima zetu za kibinadamu, kuweka maoni yetu bali kuyadhihirisha maisha katika upendo wa Mungu. Ni kuepuka kishawishi cha kuichakachua sheria ya Mungu kwa kubadili maana ya uwepo wetu na kuingiza fikra za kibinadamu. Sheria ya Mungu inatutambulisha katikati ya watu wengine. Sheria yake inayotujenga katika haki, upendo, amani na upatanisho wa kweli ni salama kwa jamii ya wanadamu. Hivyo, tungalipo hapa duniani tunapaswa kuepa kupelekeshwa na upepo na maelekeo ya ulimwengu huu, vinginevyo hatutatofautiana na watu wengine na utume wetu wa kuukomboa ulimwengu utakosa mashiko. Amri za Mungu ni hazina ya hekima yake kwetu na nyenzo ya kutunyanyua kati ya mataifa. Hii ni nguvu kwetu ya kuwa na ushawishi wa kuijenga vema jamii ya mwanadamu. Hizi hutufanya tuwe karibu zaidi na Mungu na kuidhihirisha haki yake kwa mataifa yote. Utii wa sheria ya Mungu unamfanya mmoja kutimiza yaliyo mapenzi Mungu. Mtakatifu Alfonso Maria de Liguori aliandika haya yafuatayo: “Wakati yale tuyatakayo sisi yanapokutana au kuendana na yale anayoyataka Mungu, hapo ndipo upendo wa Mungu unajitambulisha kwetu sio kama amri kutoka nje bali huwa kwetu yale ambayo tunayataka na furaha yetu, katika Mungu na pamoja na Yeye tunapewa uwezo wa kumpenda jirani, hasa wale ambao hatufuraishwi nao.” Utii kwa amri za Mungu hutufanya tujiweke chini ya mapenzi ya Mungu na kuyaoanisha matakwa yetu yaendane na yale ya Mungu. Hivyo sheria za Mungu zinanuia kuturandanisha na Mungu na kutenda kadiri ya mapezi yake. Upendo huu unapokuwa ndani mwetu ndiyo ibada yetu ya sifa kwa Mungu. Ibada hiyo ni matendo yetu mema katika maisha ya kawaida, matendo ambayo yanatuunganisha na Mungu na jirani zetu. Injili inatuonesha jinsi Kristo alivyokwaruzana na Mafarisayo na Waandishi. Kristo hakusita kuwaonesha upungufu wao ambao ni “kuheshimu kwa mdomo ila mioyo yao iko mbali na Yeye… wanamwabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu.” Kristo alitaka kuwaondoa gizani na kuona mwanga utakaowaonesha iliyo sheria ya kweli ya Mungu. Kwanza wanapaswa kuiona sheria ya Mungu kama nyenzo kuwa karibu na Mungu, yaani kumweka Mungu ndani kabisa katika mioyo yao. Namna hii inamfanya mwanadamu amsikilize Mungu kutoka ndani ya nafsi yake, yaani anaruhusu mabadiliko katika nafsi yake na kumfanya Mungu kuwa sababu ya utendaji wake wote. Mitume walionekana kufanya unajisi kwani walitenda si kadiri ya sheria. Kristo anatoa fundisho mahsusi kuhusu unajisi. “Hakuna kitu kilicho nje ya mtu ambacho kikimwingia chaweza kumtia unajisi, bali vile vimtokavyo, ndivyo vimtiavyo unajisi mtu yule.” Mitume wanashutumiwa kwa kula kitu najisi au kichafu kwa sababu ya kutofuata sheria. Lakini sheria hiyo inakosa ladha au usafi wake hauwezi kupata nguvu kama anayeshiriki chakula hicho anaendelea kujitambulisha kwa matendo machafu kama vile ulafi, chuki n.k. Sheria inapomwingia mwanadamu kama tulivyoeleza hapo juu anapaswa kuisikiliza na kuitenda. Tumesisitiza pia sheria hiyo inategemewa kumbadilisha mwanadamu. Hivyo utii wa sheria si utekelezaji wa nje tu: kwamba nimefanya ibada au nimetoa zaka au nimesali kabla ya kula au kulala au kufanya shughuli yoyote. Utii wake unaonekana katika mwitikio wa ndani na mabadiliko yanayozingatia roho ya sheria husika. Sala yangu bila kutoa matokeo chanya ya matendo yangu ni bure. Unajisi wangu unatokana na uhasi wangu wa ndani. Ingawa nimeonekana kufuata sheria lakini utu wangu wa kale wa dhambi bado haujabadilika. Bado sijakua katika utii wangu kwa Mungu, upendo wangu kwa jirani n.k. Ingawa ninasali au kutenda lolote kwa kumwomba Mungu lakini ni kwa maneno tu. Napoteza ile maana ya sala kwamba ninamuunganisha Mungu katika yote na kumfanya Yeye wa kwanza. Bado naendelea kubaki katika ufisadi wangu, umbea na kusimanga wengine. Nakosa kuwatendea haki wengine na kujilimbikizia mali na madaraka. Hayo ndiyo yanifanyayo kuwa najisi mbele ya Mungu. Matendo maovu kama uasherati, wivu, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi na upumbavu ni uthibitisho wa kutobadilika kutoka ndani ya moyo wa mtu kunakonuiwa na sheria ya Mungu. Namna hii inatuwezesha kuona juhudi za kutoitii sheria za Mungu na kuisikiliza ya mwanadamu. Mtume Yakobo anatuhitimishia Tafakari yetu kwa maneno haya: “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu ni hii, kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na Dunia pasipo mawaa.” Maneno haya maridhawa yanaelezea kwa muhtasasi maana ya sheria ya Mungu na matokeo yake kwetu. Huku ni kukua kiutu na kumtukuza Mungu kwa maisha yako yote. Mwenyezi Mungu hatuelekezi katika dini ya maadhimisho na sadaka za alatareni tu bali katika maadhimisho na dini inayomwilika katika matendo ya upendo kwake na kwa wanadamu wenzetu hasa walio wahitaji zaidi. Haya yote yanatuhitaji kujivua utu wetu wa kale na kujivika Sheria ya Kristo inayotujenga katika utu mpya ambao hujidhihirisha katika matendo ya upendo, mshikamano, upatanisho na msamaha, unyenyekevu, kuhudumiana katika Kristo na katika ujumla wake kuustawisha undugu wetu katika Kristo Yesu.
SALA: Ee Mungu utujalie tukuabudu kwa moyo na roho.
|