Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/08/2024
2024 AGOSTI 31: JUMAMOSI-JUMA LA 21 LA MWAKA
Mt. Raymundi Nonnati
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. 1 Kor 1:26-31
Ndugu zangu, angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, naam, vitu ambavyo haviko, ili avibatilishe vile vilivyoko; mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu. Bali kwa yeye ninyi mmepata kuwa katika Kristo Yesu, aliyefanywa kwetu hekima itokayo kwa Mungu, na haki, na utakatifu, na ukombozi; kusudi, kama ilivyoandikwa, yeye aonaye fahari na aone fahari juu ya Bwana. |
Wimbo wa Katikati. Zab 33:12-13, 18-21
1. Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao, (K) Heri taifa ambalo Bwana aliowachagua kuwa urithi wake. 2. Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao, 3. Nafsi zetu zinamngoja Bwana, |
Injili. Mt 25:14-30
Yesu aliwaelezea wanafunzi wake mfano huu: Mtu aliyetaka kusafiri, aliwaita watumwa wake, akaweka kwao mali zake. Akampa mmoja talanta tano, na mmoja talanta mbili, na mmoja talanta moja; kila mtu kwa kadiri ya uwezo wake; akasafiri. Mara yule aliyepokea talanta tano akaenda, akafanya biashara nazo, akachuma faida talanta nyingine tano. Vile vile na yule mwenye mbili, yeye naye akachuma nyingine mbili faida. Lakini yule aliyepokea moja alikwenda akafukua chini, akaificha fedha ya bwana wake. Baada ya siku nyingi akaja bwana wa watumwa wale, akafanya hesabu nao. Akaja yule aliyepokea talanta tano, akaleta talanta nyingine tano, akisema, Bwana, uliweka kwangu talanta tano; tazama, talanta nyingine tano nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema, mtumwa mwema na uwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta mbili, akasema, Bwana, uliweka kwangu talanta mbili; tazama, talanta nyingine mbili nilizopata faida. Bwana wake akamwambia, Vema mtumwa mwema na uwaminifu; ulikuwa mwaminifu kwa machache, nitakuweka juu ya mengi; ingia katika furaha ya bwana wako. Akaja na yule aliyepokea talanta moja, akasema, Bwana, nalitambua ya kuwa wewe u mtu mgumu, wavuna usipopanda, wakusanya usipotawanya; basi nikaogopa, nikaenda nikaificha talanta yako katika ardhi; tazama, unayo iliyo yako. Bwana wake akajibu, akamwambia, Wewe mtumwa mbaya na ulegevu, ulijua ya kuwa navuna nisipopanda, nakusanya nisipotawanya; basi, ilikupasa kuiweka fedha yangu kwa watoao riba; nami nikija ningalipata iliyo yangu na faida yake. Basi, mnyang’anyeni talanta hiyo, mpeni yule aliye nazo talanta kumi. Kwa maana kila mwenye kitu atapewa, na kuongezewa tele; lakini asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang’anywa. Na mtumwa yule asiyefaa, mtupeni mbali katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. |
TAFAKARI.
TUSHIRIKIANE NA MUNGU ANAUWEZESHA UTUME WETU: Neno la Mungu linatupa mwaliko wa kujitambua asili yetu na tulivyo duni. Mungu kwa neema yake alipotuita ametuinua kwa kuweka nguvu yake ndani yetu yakuutenda utume wake. Mwito ni kuwa hakuna mwenye haki ya kujivunia mafanikio ya utume anaofanya kwani yanatokana na neema ya Mungu wala siyo juhudi na maarifa yetu. Katika utume, tuone fahari juu ya nguvu ya Mungu anayewezesha mafanikio katika Yesu Kristo. Bwana wetu Yesu Kristo aliangaza ukuu wa neema ya Mungu kwa kuwapa watu vipaji mbalimbali. Mtume Paulo alichota nguvu hiyo katika mafunuo aliyopewa na Kristo mwalimu wake, na ndiyo maana aliweza kulea jumuiya nyingi kiasi hicho. Leo hii tunaambiwa kila mmoja wetu amepewa kipaji ambacho anapaswa kukikuza kwa utendaji wake wa kila siku. Wako wengi wanaodhani mtaji mkubwa ndio utakaofanikisha maisha yao. Swali la msingi ni hili, Je, unakuza uwezo wako? Je, unavifanyia kazi vipaji ulivyokirimiwa na Mungu? Kuza vipaji vyako ili vimtumikie Mungu na jirani. SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuvitumia vema vipaji ulivyotugawia ili kukuza utume wako. |