Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 29/08/2024

2024 AGOSTI 29: ALHAMISI-JUMA LA 21 LA MWAKA

Kufa shahidi Yohane Mbatizaji
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer. 1: 17-19

Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao. Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii. Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.

Wimbo wa Katikati. Zab 71:1-6, 15 & 17

1. Nimekukimbilia Wewe, Bwana, Nisiaibike milele.
Kwa haki yako uniponye, uniopoe, Unitegee sikio lako, uniokoe.

K) Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa

2. Uwe kwangu mwamba wa makazi yangu, Nitakakokwenda sikuzote. Umeamuru niokolewe, Ndiwe genge langu na ngome yangu.
4 Ee Mungu wangu, uniopoe mkononi mwa mkorofi, Katika mkono wake mwovu, mdhalimu. (K)

3. Maana ndiwe taraja langu, Ee Bwana MUNGU, Tumaini langu tokea ujana wangu.
6 Nimekutegemea Wewe tangu kuzaliwa, Ndiwe uliyenitoa tumboni mwa mama yangu, Ninakusifu Wewe daima. (K)

4. Kinywa changu kitasimulia haki na wokovu wako Mchana kutwa; maana sijui hesabu yake.
Ee Mungu, umenifundisha tokea ujana wangu; Nimekuwa nikitangaza miujiza yako hata leo.

 

Injili. Mk 6:17-29

Herode mwenyewe alikuwa ametuma watu, akamkamata Yohane, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake; kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohane alimwambia Herode, “Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Maana Herode alimwogopa Yohane; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha. Hata ilipotokea siku ya kufaa, na Herode, sikukuu ya kuzaliwa kwake, alipowafanyia karamu wakubwa wake, na majemadari, na watu wenye cheo wa Galilaya; ndipo binti yake yule Herodia alipoingia, akacheza, akampendeza Herode na wale walioketi pamoja naye karamuni. Mfalme akamwambia yule kijana, Niombe lo lote utakalo, nitakupa.” Akamwapia, Lo lote utakaloniomba nitakupa, hata nusu ya ufalme wangu. Basi akatoka, akamwuliza mamaye, “Niombe nini?” Naye akasema, “Kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mara akaingia kwa haraka mbele ya mfalme, akaomba akisema, “Nataka unipe sasa hivi katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji.” Mfalme akafanya huzuni sana, lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya hao walioketi karamuni, hakutaka kumkatalia. Mara mfalme akatuma askari, akaamuru kuleta kichwa chake. Basi, akaenda, akamkata kichwa mle gerezani, akakileta kichwa chake katika kombe, akampa yule kijana, naye yule kijana akampa mamaye. Wanafunzi wake waliposikia habari, walikwenda, wakauchukua mwili wake, wakauzika kaburini.

TAFAKARI

TUUPOKEE WITO WETU NA KUFANYA KAZI KWA BIDII: Mungu ametuita kwenye wito wetu ili atutume katika mazingira tofauti tofuati. Agizo la Mungu linataka utayari wetu, naye atatupa ulinzi katika hatari zote. Mzaburi ametuangaza kuwa, kinywa chetu kinapaswa kusimulia haki ya Mungu kwa wale wanaopotosha haki kwa kutumia mamlaka yao vibaya. Mungu aliyetuita ni mwaminifu, yeye atuimarishe katika mapambano ya kurejesha haki katika familia, jumuiya, Kanisa na taifa lote ili watu wa Mungu waishi kwa furaha na ustawi wa kweli. Injili ya leo inasimulia kifodini cha Yohane Mbatizaji. Kifo chake kilitokanana utenda kazi wake alioufanyia katika mazingira magumu yaliyojaa dhuluma. Dhuluma hizi zilitekelezwa na mamlaka ya juu ya utawala – mfalme Herode. Yohane hakuogopa mamlaka ya Herode, alisimama katika ukweli daima. Leo hii katika jamii tunayoishi, kuna mambo mengi sana yanayotendeka ambayo si halali kabisa. Tunaalikwa kupaza sauti bila kuogopa magumu yatokanayo na ukweli kama alivyofanya Mt. Yohane Mbatizaji.

Sala: Ee Bwana ututie ujasiri wa kuendelea kutimiza majukumu ya wito niliochagua bila woga.