Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 28/08/2024

2024 AGOSTI 28: JUMATANO-JUMA LA 21 LA MWAKA

Mt. Augustino, Askofu na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 1

Somo 1. 2 Thes 3: 6-10, 16-18

Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu. Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote. Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndiyo mwandiko wangu. Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.

Wimbo wa Katikati. Zab 128: 1-2. 4-5

1. Taabu ya mikono yake hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.

(K) Heri kila mtu amchaye Bwana.

2. Tazama, atabarikiwa hivyo, yule amchaye Bwana.
Bwana akubariki toka Sayuni,
Uone uheri wa Yerusalemu siku zote za Maisha yako. (K)

Injili. Mt 23:27-32

Yesu alisema, Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mmefanana na makaburi yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu, na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani mmejaa unafiki na maasi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.

TAFAKARI

UKRISTO NI KUISHI UFUASI, KIELELEZO KWA WENGINE: Ukristo na ufuasi wetu ni mwaliko wa kuishi maisha ya nidhamu kulingana na mafundisho ya imani ya Kanisa Katoliki. Kanisa limeandaa utaratibu wa utendaji ambao muumini akifuata atafikia mafanikio. Tunashuhudia miongoni mwa wakristo, watu wanaoishi bila utaratibu unaoeleweka. Kwa upande wa maisha ya kiroho: hawasali, hawapokei sakramenti, hawaendi kwenye jumuiya wala Kanisani. Tunashuhudia watu wanaokaa bila kazi na wanataka kula na kufurahia maisha. Neno la Mungu linatuhimiza kurudi katika nidhamu na kutenda kwa unyofu wote. Bwana wetu Yesu Kristo anaendelea kuangazia juu ya swala la unafiki akishutumu utendaji usioruhusu mabadiliko wala maendeleo ya kiroho. Watendaji hao wamefananishwa na makaburi ambayo kwa nje huonekana safi na mengine yemejengwa kwa mawe ya thamani, ila kilichoko ndani ni mifupa isiyo na thamani, uchafu na uozo. Yesu anahimiza unyofu wa ndani katika utendaji wa kila siku. Tukatize mnyororo huo wa unafiki kwa kuwa watu wenye haki hasa kwa wanyonge.

SALA: Ee Bwana Yesu utujalie undani wetu wa moyo uonekane katika hali yetu ya nje.