Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 26/08/2024
2024 AGOSTI 26: JUMATATU-JUMA LA 21 LA MWAKA
Mt. Elizabeti Bishiye, Mwanzilishi wa Shirika
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 1
Somo 1. 2 Thes 1:1-5, 11-12
Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu, na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu siku zote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa hiyo twawaombea ninyi siku zote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. |
Wimbo wa Katikati. Zab 96:1-5
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, (K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake. 2. Tangazeni wokovu wake siku kwa siku. 3. Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. |
Injili. Mt 23:13-22
Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake: Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanum mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au ile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake. |
TAFAKARI
MAISHA YETU YAWE MAHUBIRI YA UTUKUFU WA MUNGU: Katika somo la kwanza, mtume Paulo anajivunia wito wake na kazi yake ya kuhubiri. Anatuhimiza nasi tuone fahari juu ya wito wetu mbali na magumu tunayokumbana nayo. Tumeitiwa utakatifu, na hivyo, yatupasa kufanya kazi kwa bidii ili kufikia hali hiyo. Maisha yana dhiki na changamoto nyingi, hizi zisifishe matumaini ya wito wetu, bali tuwe na saburi. Kama wasafiri, tuombeane na kutiana moyo ili kila mmoja afanikishe utume wake kwa kufanya yale yatupasayo kwa neema ya Mungu. Injili inatukumbusha kuwa kujisahau katika utume kutatufanya kupoteza tuzo. Utume wetu unapaswa kuwaangaza na kuwapa wengine matumaini ya kusonga mbele. Tukiishi kinyume sisi tunapotea na tunakuwa sababu ya wengine kupotea njia. Tukipofuka katika utendaji kwa kuishi kinafiki tunachanganya watu kuhusu mambo matakatifu na Mungu aliye utukufu. Tusiwe kikwazo kwa maisha yasiyompendeza Mungu, bali maisha yetu yawe kioo na mahubiri ya mafundisho ya Kristo. SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuhubiri kwa maneno na matendo yetu kama wakristo. |