Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 25/08/2024

2024 AGOSTI 25: DOMINIKA YA 21 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yos 24: 1-2a, 15-18b

Yoshua aliwakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida yao; na wakahudhuria mbele za Mungu. Yoshua akawaambia watu wote, Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng’ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana. Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine; kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao. Basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana; maana yeye ndiye Mungu wetu. 

Wimbo wa Katikati. Zab 34: 2-3, 16-23

1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekeve wasikie wakafurahi.

(K) Onjeni, mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

2. Macho ya Bwana huwalekea wenye haki,
Na masikio yake hukielekea kilio chao.
Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya,
Aliondoe kumbukumbu lao duniani. (K)

3. Walilia, naye bwana akasikia,
Akawaponya na taabu zao zote.
Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo,
Na waliopondeka roho huwaokoa. (K)

4. Mateso ya mwenye haki ni mengi,
Lakini Bwana humponya nayo yote.
Huihifadhi mifupa yake yote,
Haukuvunjika hata mmoja. (K)

5. Uovu utamwua asiye haki,
Nao wamchukiao mwenye haki watahukumiwa.
Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake,
Wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao. (K)

Somo 2. Efe 5: 21-32

Hali mnanyenyekeana katika kicho cha Kristo. Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili. Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo, vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo. Enyi waume, wapendeni wake zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo, bali liwe takatifu lisilo na mawaa. Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe. Maana hakuna mtu anayechukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa. Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja. Siri hiyo ni kubwa; ila mimi nanena habari ya Kristo na Kanisa.

Injili. Yn 6: 60-69

Watu wengi miongoni mwa wanafunzi wa Yesu waliposikia, walisema, Neno hili ni gumu, ni nani awezaye kulisikia? Naye Yesu akafahamu nafsini mwake ya kuwa wanafunzi wake wanalinung’unikia neno hilo, akawaambia, Je! neno hili linawakwaza? Itakuwaje basi, mmwonapo Mwana wa Adamu akipaa huko alikokuwako kwanza? Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima. Lakini kuna wengine miongoni mwenu wasioamini. Kwa maana Yesu alijua tangu mwanzo ni nani wasioamini, naye ni nani atakayemsaliti. Akasema, Kwa sababu hiyo nimewaambia ya kwamba hakuna mtu awezaye kuja kwangu isipokuwa amejaliwa na Baba yangu. Kwa ajili ya hayo wengi miongoni mwa wanafunzi wake wakarejea nyuma, wasiandamane naye tena.  Basi Yesu akawaambia wale Thenashara, Je! ninyi nanyi mwataka kuondoka? Basi Simoni Petro akamjibu, Bwana! twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele. Nasi tumesadiki, tena tumejua, ya kuwa wewe ndiwe Mtakatifu wa Mungu.

TAFAKARI

NENO LA MUNGU LITASIMAMA HATA KAMA YOTE YATAPITA
Hekima ya mwanadamu inatengeneza mazingira yake na kujitahidi kumleta mwenyezi Mungu aenee katika mazingira hayo. Haya huonekana pale tunaposhindwa kumwelewa Mungu katika changamoto fulani fulani za maisha. Tunajikuta mara nyingi tunapoteza imani au kuwa na udhaifu kiimani pale mambo yamekwama. Badala ya kumweka Mungu katika nafasi ya kwanza yaani kuwa chanzo, mratibu na mwisho wa yote tuyafanyayo, tunamweka Yeye kama pambo la kuthibitisha kile tunachokifikiria. Katika muktadha wa kiimani tunapaswa kumtanguliza Mungu mbele. Neno lake lapaswa kupewa kiapo mbele. Neno lake lapaswa kusimama daima hata kama linapingana na matakwa au mawazo yetu.
“Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima”. Maneno haya Kristo ni ya msingi na yanakuja baada ya kuona mwitikio wa watu juu ya fundisho lake kuhusu chakula cha uzima. Tangu aya ya 26 ya sura ya sita ya Injili ya Yohane Kristo alinuia kuwaondoa wafuasi wake kutoka katika fikara za kimwili ili kuupokea ujumbe wa kiroho aliotuletea wanadamu. Mara nyingi tunafungwa na fikara na matamanio ya kimwili na kujidanganya tunaifuata vyema imani yetu. Mara nyingi tunahusisha mambo ya kidunia na misingi ya kiimani na kujikuta tunayaweka mambo ya kiimani katika nafasi ya pili, au kuyachukulia kama kitu kinachothibitisha tu mambo ya kimwili.
Kristo anasema: “mwili haufai kitu.” Hii haimaanishi kuudharau mwili. Mwili unabaki katika umuhimu wake na ulazima wa kumwelezea mwanadamu. Msisitizo ni kuwa muunganiko wetu na Mungu katika hali ya kiroho. Roho ndiyo inayotuunganisha na Mungu na hivyo kutupatia uzima. Hatuunganiki na Mungu kwa kumwelewa katika ustadi wa akili zetu za kimwili bali katika unganiko la ndani la kiroho. Unganiko hilo ndilo mazingira mahsusi ya kumfanya mmoja kuweza kuuelewa ujumbe wa ukombozi uletwao na Kristo. Ujumbe huo ni ujumbe wa kiroho, ujumbe ambao ukipokelewa katika namna sahihi unakuwa na tija kubwa katika maisha ya mwanadamu ndani ya jamii. Ujumbe huo unapopokelewa vyema utamjenga mtu katika ukomavu wa kiutu.
“Bwana! Twende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.” Pale tunapokosa kuona maana ya maisha, kuona mwanga mbele tuwe na ujasiri kujikabidhisha kwa Kristo kwa kuona hakuna namna nyingine ya kutustawisha kiroho na kimwili bali kubaki katika Yeye. Kutaniko letu na Kristo ni kutaniko la kiroho na hivyo ujasiri huo hauji bure kama tusipompokea Kristo kiroho. Ni wajibu kwetu kuona namna tunavyomtafuta Kristo. Tunaweza kutumia akili na ujuzi wetu kumwelewa Kristo na kumwelezea kwa maandiko mbalimbali lakini bado asiingie mioyoni mwetu.
Hili linaweza kujithibitisha kwa namna tunavyotenda katika maisha. Changamoto nyingi za kimaisha ambazo mwanadamu anakutana nazo zinashawishi kurudi nyuma na kumwacha Kristo. Wapo wengine wanaotamani hata kutumia nguvu za giza. Namna hizi ni kishawishi cha kutaka kurudi nyuma na kumwacha Kristo. Kristo anamuuliza kila mmoja moyoni: “Ninyi nanyi mwataka kuondoka?” Namna hii pia inajitokeza katika jamii ya Waisraeli wakati wakiwa mbele za Mungu huko Shekemu. Yoshua aliwaandaa katika namna ya kiroho ili kufanya maamuzi ya maisha. Aliwakumbusha historia yao na juu ya mkono wa Mungu wenye nguvu uliowakomboa kisha akawapa uchaguzi: “Nanyi kama mkiona vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia… lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana”.
Je, amfundisho ya imani yanakuwa magumu sana kwetu? Tunavutwa na miungu ya fedha, madaraka, umaarufu na utajiri ambayo tuliitumikia zamani. Lakini tunakumbushwa namna miungu hiyo ilivyotuingiza katika majanga. Tumepoteza ndugu zetu na marafiki sababu ya kiburi na ubinafsi wetu, tumeua dhamiri za watu, tumenyang’anya haki za watu. Tulitawaliwa sana na maelekeo ya mwili ambao haufai kitu. Maisha yetu kiroho yalikuwa mfu. Kwa ujumla utumishi wetu kwa miungu hiyo umetuingiza katika maangamizi ya utu wetu. Lakini tunashukuru tumeletewa neno la uzima kwa njia ya Kristo. Hivyo uchaguzi ni wako: kumtumikia Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo na kupata uzima wa milele au kurudi kwenye miungu ya zamani na kuingia katika kifo.
Swali la Kristo kwa Mitume wake linatufundisha pia uimara unaohitajika katika mafundisho ya Kanisa. Si kwa sababu watu fulani wameondoka au wameshindwa kuelewa fundisho letu ndipo tulegeze ukweli wa mafundisho yetu. Neno la Mungu linapaswa kusimama milele. Ni onyo la kuepuka kuineza imani kwa kutafuta kuongeza idadi ya wafuasi tu bila kuangalia kiwango cha imani katika kundi. Namna hii itafananishwa na makundi ya ushabiki wa kidini ambayo huangalia tu kuongezeka idadi ya waamini bila kujali ustawi wa malengo msingi ya kiimani yaani makuzi ya kiroho na kutunza amani, ukweli, haki na huruma. Leo hii kwa namna fulani tunaona kuingiliwa kwa misingi ya kiimani na mambo ya kidunia. Watu ulimwengu huu wanatamani misingi ya kiimani iwe kama bendera inayofuta upepo wa mwendo wa dunia. Tuliombee Kanisa kusudi libaki aminifu katika kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na kuongozwa nayo.
Moja ya maeneo ambayo yanapotoshwa na upepo wa kidunia na kuharibu maana yake ya kiroho ni maisha ya ndoa. Ujumbe anaoutoa Mtakatifu Paulo katika Somo la pili juu ya utii na upendo kama misingi katika maisha ya familia huwa unageuzwa mara nyingi ili kutoa auheni za kidunia hata kama huaribu makusudio ya kiroho. Tunashuhudia leo hii jinsi ambavyo dhana ya upendo na utii inavyochakachuliwa. Watu wengi wanatafuta kuhalalisha madai ya uhuru na usawa si kadiri ya namna ya kiroho bali katika mivuto na vionjo vya kibinadamu. Matokeo yake ni kuvunjika kwa ndoa nyingi. Sasa tujiulize, nini maana ya uhuru au usawa katika namna ya kiroho? Je, utii katika namna ya kiroho humfanya mmoja kuwa mtwana na mwingine mtumwa? Je, dhana ya upendo inaeandana vipi na usawa wa kweli?
Neno la Mungu limeweka wazi kwamba yote yafanyike katika namna ya “kunyenyekeana katika Kristo.” Fumbo la Msalaba linatufundisha maana hiyo ya kuonesha utii na upendo katika namna ya uhuru kamili. Hii ni namna ya kuifuata njia ya Kristo, yaani kusikiliza sauti yake katika maisha ya familia. Utii na upendo ndani ya familia unapaswa kupata msingi wake katika Kristo. Katika maisha ya familia ya mwanadamu, iliyo kitovu cha maisha ya undugu, tunapaswa kumfuata Kristo. Maarifa na ujuzi wa kiulimwengu hutulazimisha kuamisha mawazo yetu kutoka huko na matokeo yake huwa ni kuharibu familia. Jamii ya leo imekuwa mwalimu na muelekezaji wa familia ya mwanadamu lakini imempeleka katika maangamizi. Mwaliko wa Yoshua katika somo la kwanza pia unapata nafasi hapa. Familia ya mwanadamu inaulizwa njia ya kufuata: je! Ni kusikiliza sauti ya Dunia na kuendelea kuiharibu familia aua kuisikiliza sauti ya Kristo inayotupeleka katika maisha ya uzima wa milele?

SALA: Ee Mungu utuwezeshe kudumu katika kusadiki maneno yako.