Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 24/08/2024

2024 AGOSTI 24: JUMAMOSI-JUMA LA 20 LA MWAKA

MT. BARTOLOMEO, MTUME
Rangi: Nyekundu

Zaburi: Tazama sala ya siku

Somo 1. Ufu 21:9-14

Malaika alinijia akanena nami, akisema, “Njoo huku, nami nitakuonyesha yule Bibiarusi, mke wa Mwanakondoo.” Akanichukua katika Roho mpaka mlima mkubwa, mrefu, akanionyesha ule mji mtakatifu, Yerusalemu, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mwenyezi Mungu; mwenye utukufu wa Mungu, na mwangaza wake ulikuwa mfano wa kito chenye thamani nyingi kama kito cha yaspi, safi kama bilauri; ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu, wenye milango kumi na miwili; na katika ile milango malaika kumi na wavili; na majina yameandikwa ambayo ni majina ya kabila kumi na mbili za Waisraeli. Upande wa mashariki milango mitatu; na upande wa kaskazini milango mitatu; na upande wa kusini milango mitatu; na upande wa magharibi milango mitatu. Na ukuta wa mji ulikuwa na misingi kumi na miwili, na katika ile misingi majina kumi na mawili ya wale mitume kumi na wawili na Mwana-Kondoo.

Wimbo wa Katikati. Zab 145:10-13, 17-18

1. Ee Bwana, kazi zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wako,
Na kuuhadithia uweza wako.

(K) Wacha Mungu wataunena utukufu wa ufalme wako, Ee Bwana.

2. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na ufalme wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)

3. Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye Fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu. (K)

Injili. Yn 1:45-51

Filipo alimwona Nathanaeli, akamwambia, “Tumemwona yeye aliyeandikiwa na Musa katika torati, na manabii, Yesu, mwana wa Yusufu, mtu wa Nazareti.” Nathanaeli akamwambia, “Laweza neno jema kutoka Nazareti?” Filipo akamwambia, ‘Njoo uone.” Basi Yesu, akamwona Nathanaeli anakuja kwake, akanena habari zake, “Tazama, Mwisraeli kweli kweli, hamna hila ndani yake. Nathanaeli akamwambia, “Umepataje kunitambua?” Yesu akajibu, akamwambia, “Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona.” Nathanaeli akamjibu, “Rabi, wewe u Mwana wa Mungu, ndiwe Mfalme wa Israeli.” Yesu akajibu, akamwambia, “Kwa sababu nilikuambia, ‘Nilikuona chini ya mtini,’ waamini? Utaona mambo makubwa kuliko haya.  Akawaambia, “Amini, amin, nawaambia, Mtaziona mbingu zimefunguka na malaika wa Mungu wakikwea na kushuka juu ya Mwana wa Adamu.”

TAFAKARI

TWENDE KWA YESU: Mtakatifu Barthalomeo Mtume, ni mmoja wa wale aliowachagua Kristo akawaweka wawe misingi ya Kanisa ili lifundishe utakatifu. Leo tumeambiwa, mji huo mtakatifu wa mbinguni una milango kumi na miwili, mitatu kila upande. Huu ni mwaliko wa kuona jinsi Mungu anavyotupenda, na hakusudii tuteseke tukitafuta mlango. Wingi wa milango ni miito mitakatifu anayotuitia Mungu. Kwa kuishi miito hiyo kikamilifu kulingana na mafundisho ya mitume tutafika mbinguni. Mtume Bartalomeo leo anakuwa mfano kwetu baada ya kumfuata Kristo hakugeukia yale aliyokuwa ameyaacha. Wale mitume waliacha mengi kweli wakabakia na moja la kumsikiliza Kristo na alipowatuma wakatimiza vema majukumu ya wito wao. Bwana wetu Yesu Kristo ametuambia kuwa, yeye ndiye njia ya kwenda kwa Baba. Tuwapeleke watu wote kwa Yesu kama alivyofanya mtume Filipo kwa kumpeleka Nathanael (Barthalomeo) na Bwana akampa utume. 

SALA: Mtakatifu Barthalomeo Mtume utuombee tuutimize vyema utume wetu.