Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 23/08/2024
2024 AGOSTI 23: IJUMAA-JUMA LA 20 LA MWAKA
Mt. Rosa wa Lima
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma IV
Somo 1. Eze 37: 1-14
Mkono wa Bwana ulikuwa juu yangu, naye akanichukua nje katika roho ya Bwana, akaniweka chini, katikati ya bonde; nalo limejaa mifupa; akanipitisha karibu nayo pande zote; na tazama, palikuwa mifupa mingi katika ule uwanda! Nayo, tazama, ilikuwa mikavu sana. Akaniambia, “Mwanadamu, je, mifupa hii yaweza kuishi? Nami nikajibu, “Ee Bwana Mungu, wajua wewe.”. Akaniambia tena, “Toa unabii juu ya mifupa hii, uiambie, Enyi mifupa mikavu, lisikieni neno la Bwana. Bwana Mungu aiambia mifupa hii maneno haya; Tazama, nitatia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi. Nami nitatia mishipa juu yenu, nami nitaleta nyama iwe juu yenu, na kuwafunika ngozi, na kutia pumzi ndani yenu, nanyi mtaishi; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana.” Basi nikatoa unabii kama nilivyoamriwa; hata nilipokuwa nikitoa unabii, palikuwa na mshindo mkuu; na tazama, tetemeko la nchi, na ile mifupa ikasogeleana, mfupa kwa mfupa mwenziwe. Nikatazama, kumbe! Kulikuwa na mishipa juu yake, nyama ikatokea juu yake, ngozi ikaifunika juu yake, lakini haikuwamo pumzi ndani yake. Ndipo akaniambia, “Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana Mungu asema hivi; njoo kutoka pande za pepo nne, ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi.” Basi nikatabiri kama alivyoniamuru; pumzi ikawaingia, wakaishi, wakasimama kwa miguu yao, jeshi kubwa mno. Kisha akaniambia, “Mwanadamu, mifupa hii ni nyumba yote ya Israeli; tazama, wao husema, ‘Mifupa yetu imekauka, matumaini yetu yametupotea; tumekatiliwa mbali kabisa.’ Basi tabiri, uwaambie, Bwana Mungu asema hivi; Tazama, nitafunua makaburi yenu, na kuwapandisha kutoka katika makaburi yenu enyi watu wangu, nami nitawaingizeni katika nchi ya Israeli. Nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapoyafunua makaburi yenu, na kuwatoa ninyi katika makaburi yenu, enyi watu wangu. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, nanyi mtaishi, nami nitawawekeni katika nchi yenu, nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, nimesema hayo, na kuyatimiza asema Bwana.” |
Wimbo wa Katikati. Zab 107: 2-9
1. Wasema hivi waliokombolewa na Bwana, (K) “Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema. 2. Walitanga-tanga jangwani katika njia ya nyika; 3. Wakamlilia Bwana katika dhiki zao, 4. Na wamshukuru Bwana kwa Fadhili zake, |
Injili. Mt 22:34-40
Mafarisayo waliposikia ya kwamba amewafumba kinywa wale Masadukayo, walifanya shauri pamoja. Mmoja wao, mwanasheria, akamwuliza, akimjaribu; “Mwalimu, katika torati ni amri ipi iliyo kuu?” Akamwambia, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote. Hii ndiyo amri iliyo kuu, tena ni ya kwanza. Na yapili yafanana nayo, ni hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Katika amri hizi mbili hutegemea torati yote na manabii.” |
TAFAKARI
TUTOE MAJIBU SAHIHI YA UTUME WETU: Unabii wa Ezekiel umeambatana na swali, Je, mifupa mikavu yaweza kuishi? Ametoa jawabu kuwa “Wajua wewe.” Hata sisi sidhani kama kuna mtu mwenye jawabu sahihi kuwa mifupa mikavu yaweza kuishi. Lakini tukishirikiana na neema ya Mungu yote yatawezekana. Jukumu letu ni kutoa unabii, na Mungu anatenda kupitia utume wetu. Wako watu, ambao tunawaona kama mifupa mikavu, yako mambo tumeyakatisha tamaa kama kuwa na mifupa mikavu – tukatoe unabii juu ya uwezo wa Mungu. Lengo la malezi ya Kikristo ni kumpatia mlelewa mwanga wa kuweza kutoa jawabu sahihi wakati wa changamoto za maisha. Katika unabii wa Ezekiel, yeye alipoulizwa swali gumu juu ya mifupa mikavu kuishi alisema, “Wewe wajua.” Kwa leo hii mmoja wetu angeulizwa swali hilo jawabu lake lingekuwa “HAPANA” alama ya mkato wa tamaa. Leo hii wako watoto, vijana, wanajumuiya na waamini wasioweza kutoa jawabu sahihi kuhusu misingi ya imani yetu. Tukazie malezi na Mungu apewe nafasi ya kwanza katika maisha na shughuli zetu. SALA: Ee Bwana tuwezeshe kuwa na majibu sahihi katika changamoto mbalimbali tunazokutana nazo. |