Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/08/2024

2024 AGOSTI 22: ALHAMISI-JUMA LA 20 LA MWAKA

Bikira Maria Malkia
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma IV

Somo 1. Eze 36:23-28

Neno la Bwana lilinijia hivi: nitalitakasa jina langu kuu, lililotiwa unajisi katika mataifa, mlilolitia unajisi kati yao; nao mataifa watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, asema Bwana Mungu, nitakapotakaswa kati yenu mbele ya macho yao. Maana nitawatwaa kati ya mataifa, nami nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote, na kuwarudisha katika nchi yenu wenyewe. Nami nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi; nitawatakaseni na uchafu wenu wote, na vinyago vyenu vyote. Nami nitawapa ninyi moyo mpya, nami nitatia roho mpya ndani yenu, nami nitatoa moyo wa jiwe uliomo ndani ya mwili wenu, nami nitawapa moyo wa nyama. Nami nitatia roho yangu ndani yenu, na kuwaendesha katika sheria zangu, nanyi mtazishika hukumu zangu, na kuzitenda. Nanyi mtakaa katika nchi ile niliyowapa baba zenu, nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.

Wimbo wa Katikati. ” Zab 51:12-15, 18-19 “

1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

(K) “Nitawanyunyizia maji safi; Nanyi mtakuwa safi, nitawatakaseni na uchafu wenu wote.

2. Unirudishie furaha ya wokovu wako;
Unitegemeze kwa roho ya wepesi.
Nitawafundisha wakosaji njia zako,
Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa,
Wewe huridhii sadaka ya kuteketezwa.
Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika;
Ee Mungu, hutaudharau. (K)

Injili. Mt 22:1-14

Yesu aliwaambia makuhani na makutano kwa mithali, akisema, “Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi. Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja. Akatuma tena watumwa wengine, akisema, ‘Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.’  Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake; nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua. Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao. Kisha akawaambia watumwa wake, ‘Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.  Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini. Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni. Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.  Akamwambia, ‘Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa. Mfalme akawaambia watumishi, ‘Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.’ Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.”

TAFAKARI

TUPANGE SHUGULI ZETU ZIWIANE NA MPANGO WA MUNGU: Unabii wa Ezekiel ni mwaliko wa Mungu kwa mwanadamu kutafakari mpango mpana alio nao juu yetu. Kama wana wa Israeli, yawezekana wengine tumefarakana katika familia, jumuiya na kutangatanga katika imani Katoliki. Mpango wa Mungu ni kutukusanya pamoja na kutuosha ili tuweze kuwa safi kwa utumishi. Hatuwezi kumtumikia Mungu na mioyo iliyo michafu wala iliyo chakaa, tukubali atufanye wapya kwa neema zake, na tuishi kuendana na sheria zake. Kama ilivyoangazwa katika wazo kuu hapo juu, daima yatupasa kupanga shughuli zetu ziwiane na mpango mpana wa Mungu na Kanisa lake. Waalikwa katika karamu iliyoandaliwa kwa gharama kubwa, hawakupata maumivu kwa kutohudhuria kuwa mwandaaji atapata hasara, ila wameangalia maslahi yao wenyewe tu. Hao ni mfano wa waamini wengi sasa katika Kanisa. Hawaendi kwenye jumuiya, kisa tuna kazi za watu (mwajiri). Ninawahi kwenye shughuli zangu za kujipatia kipato. Wote tukiwa na udhuru, Kanisa na maisha ya mbinguni tunamwachia nani? 

SALA: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kupanga vema shughuli zetu ziendane na mpango wa Mungu.