Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/08/2024
2024 AGOSTI 20: JUMANNE-JUMA LA 20 LA MWAKA
Mt. Bernardo Abate na Mwalimu wa Kanisa
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma IV
Somo 1. Eze 28:1-10
Neno la Bwana likanijia tena, kusema, “Mwanadamu, mwambie mkuu wa Tiro, Bwana Mungu asema hivi; kwa kuwa moyo wako umeinuka, nawe umesema, ‘Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari;’ lakini u mwanadamu wala si Mungu, ujapokuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu. Tazama, una hekima kuliko Danieli; hapana neno la siri watu wawezalo kukuficha; kwa hekima yako na kwa fahamu zako umejipatia utajiri, nawe umepata dhahabu na fedha katika hazina zako; kwa hekima yako nyingi, na kwa biashara yako, umeongeza utajiri wako, na moyo wako umeinuka kwa sababu ya utajiri wako. Basi, kwa hiyo, Bwana Mungu asema hivi; kwa kuwa umeweka moyo wako kama moyo wa Mungu; basi, tazama, nitaleta wageni juu yako, watu wa mataifa wenye kutisha; nao watafuta panga zao juu ya uzuri wa hekima yako, nao watautia uchafu mwangaza wako. Watakushusha hata shimoni; nawe utakufa kifo chao waliouawa kati ya bahari. Je, Utazidi kusema mbele yake huyo akuuaye, mimi ni Mungu? Lakini u mwanadamu, wala si Mungu, mkononi mwake akutiaye jeraha. Utakufa kifo cha hao wasiotahiriwa, kwa mikono ya wageni; kwa maana mimi nimenena neno hili, asema Bwana Mungu. |
Wimbo wa Katikati. Kum 32:26-28, 30, 35-36
1. Nalisema, ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu; Isipokuwa naliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo. (K)Naua Mimi, nahuisha mimi. 2. Wasije wakasema, mkono wetu umetukuka, Wala Bwana hakuyafanya haya yote. Maana hawa ni taifa wasio shauri, Wala fahamu hamna ndani yao. (K) 3. Mmoja angefukuzaje watu walio elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa? (K) 4. Maana siku ya msiba wao imekaribia |
Injili. Mt 19:23-30
Yesu aliwaambia wanafunzi wake, “Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Nawaambia tena, ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Wanafunzi waliposikia, walishangaa mno, wakisema, “Ni nani basi awezaye kuokoka?” Yesu akawakazia macho, akawaambia, “Kwa wanadamu hilo haliwezekani;” bali kwa Mungu yote yawezekana.” Ndipo Petro akajibu, akamwambia, “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?” Yesu akawaambia, “Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli. Na kila mtu aliyeacha nyumba, au ndugu wa kiume au wa kike, au baba, au mama, au watoto, au mashamba, kwa ajili ya jina langu, atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele. Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza. |
TAFAKARI
MUNGU ANATUSHIRIKISHA MAKUU: Mungu ametuumba kwa lengo la kushiriki ukuu wake katika uumbaji. Tukipata mafanikio yoyote katika utajiri na madaraka kamwe tusijisahau na kujiita miungu. Uwezo wa Mungu wetu uko hasa katika uwezo wa kujizuia asitumie uwezo huo vibaya. Watawala wamekuwa wakisahau hilo, na hivyo wawapo madarakani, na katika mafanikio wengi wetu hujiona kama vile wamemkaribia Mungu kwa ukuu. Unabii wa leo ni onyo kuwa ulinzi na mafanikio tuliyo nayo ni zawadi ya Mungu. Tumnyenyekee. Akituondolea hivyo, tutashambuliwa kirahisi na maadui zetu; umaskini, magonjwa na uharibifu utatufika kirahisi. Bwana wetu Yesu Kristo amefafanua juu ya furaha ya wale watakaoweza kupokea wito wao kwa unyenyekevu na kumfuata kwa uaminifu. Changamoto ya injili inatualika kujitambua, hasa vilema vyetu ili tuweze kupenya katika mitego mbalimbali kama vile ngamia anavyojitambua na kupenya katika tundu la sindano na kukwepa hatari zote. Tukiacha yote kwa ajili ya Mungu, Yeye atatupatia yote. SALA: Ee Mungu utupe neema ya kudumu katika kukutegemea Wewe daima. |