Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/08/2024

2024 AGOSTI 19: JUMATATU-JUMA LA 20 LA MWAKA

Mt. Yohane Eudes, Padre
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma IV

Somo 1. Eze 24:15-23

Neno la Bwana linanijia tena, kusema, “Mwanadamu, tazama, ninakuondolea kwa pigo moja tunu, mteule wa macho yako; walakini hutaomboleza wala kulia, wala yasichuruzike machozi yako. Ugua, lakini si kwa sauti ya kusikiwa; usifanye matanga kwa ajili yake yeye aliyekufa; jipige kilemba chako, ukavae viatu vyako, wala usiifunike midomo yako, wala usile chakula cha watu.”  Basi nalisema na watu asubuhi; na jioni mke wangu akafa; nami nalifanya asubuhi kama nilivyoagizwa. Watu hao wakaniambia, “Je, hutaki kutuambia maana ya mambo haya kwetu, hata umefanya kama vile ufanyavyo.” Nikawaambia, “Neno la Bwana, lilinijia kusema, Uwaambie nyumba ya Israeli, Bwana Mungu asema hivi, angalieni, nitapatia unajisi patakatifu pangu, fahari ya uwezo wenu, mahali pa kutamaniwa na macho yenu, ambapo roho zenu zinapahurumia; na wana wenu na binti zenu, mliowaacha nyuma, wataanguka kwa upanga. Nanyi mtafanya kama mimi nilivyofanya; hamtaifunika midomo yenu, wala kula chakula cha watu. Na vilemba vyenu vitakuwa juu ya vichwa vyenu, na viatu vyenu miguuni mwenu; hamtaomboleza wala kulia; lakini mtafifia katika maovu yenu, na kuugua kila mtu pamoja na mwenziwe. Basi ndivyo Ezekieli atakavyokuwa ishara kwenu; ninyi mtatenda sawasawa na yote aliyoyatenda yeye; litakapokuja jambo hili, ndipo mtakapojua ya kuwa mimi ndimi Bwana Mungu.

Wimbo wa Katikati. Kum 32:18-21

“1. Humkumbuki mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau. Bwana akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake.

(K) Umemsahau Mungu aliyekuzaa.

2. Akasema, nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio Imani ndani yao. (K)

3. Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu;
Wamenikasirisha kwa ubatili wao;
Nami nitawatia wivu kwa wasio watu,
Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. (K)”

Injili. Mt 19:16-22

Mtu mmoja alimwendea Yesu akamwambia, “Mwalimu, nitende jambo gani jema, ili nipate uzima wa milele?” Akamwambia, “Kwani kuniuliza habari ya wema?  Aliye mwema ni mmoja.  Lakini ukitaka kuingia katika uzima, zishike amri.” Akamwambia, “Zipi?” Yesu akasema, “Ni hivi, Usiue, Usizini, Usiibe, Usishuhudie uongo, Waheshimu baba yako na mama yako, na, Mpende jirani yako kama nafsi yako.” Yule kijana akamwambia, “Haya yote nimeyashika; nimepungukiwa na nini tena?” Yesu akamwambia, “Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate.” Yule kijana alipolisikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.

TAFAKARI

NEEMA YA MUNGU ITUDUMISHE KATIKA WITO WETU: Miito yetu inakabiliwa na changamoto nyingi, lakini tusife moyo Mungu anatupatia kila aina ya msaada. Alipoitwa Ezekiel alikuwa na mashaka ila Mungu alimwahidia msaada na ulinzi. Katika kutekeleza wito na utume anakumbana na changamoto, lakini katika simulizi la somo la leo anaambiwa asichuruzike machozi wala kulia! Maisha ya nabii huyu tumeambiwa yawe ni ishara kwetu, tunapokumbana na changamoto tusife moyo wala tusikate tamaa, tumtegemee Mungu; atatufanikisha. Kijana wa mfano katika injili ya leo, pamoja na bidii binafsi alizokuwa nazo katika kushika amri na maagizo, “Haya yote nimeyashika,” bado ameshindwa kukamilisha wito wake kwa sababu ya yale aliyojishikamanisha nayo, kama mali akajiona hawezi kuiacha na kuingia katika ufuasi kamili wa Yesu. Je, sisi ni nini kinachotufanya tushindwe katika ufuasi wetu?

SALA: Ee Mungu utupe neema ya kumfuata Yesu wakati wote.