Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 14/08/2024
2024 AGOSTI 14: JUMATANO-JUMA LA 19 LA MWAKA
Mt. Maximilian Maria Kolbe Shahidi
Rangi: Nyekundu
Zaburi: Juma III
Somo 1. Eze 9: 1-7; 10: 18-22
Mungu alilia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, “Waamuru wale wanaousimamia mji wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake cha kuangamiza mkononi mwake.” Na tazama, watu sita wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba. Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu Yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Bwana akamwambia, “Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, ukatie alama katika vipaji vya nyuso vya watu wanaougua na kulia kwa sababu ya machukizo yote yanayofanyika kati yake”. Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, “Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige! Jicho lenu lisiachilie; wala msione huruma; waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote mwenye hiyo alama; tena anzeni katika patakatifu pangu. “Basi wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba. Akawaambia, “Itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa. Haya, enendeni. “Wakaenenda, wakapigapiga katika mji. Kisha huo utukufu wa Bwana ukatoka pale juu ya kizingiti cha nyumba, ukasimama juu ya makerubi. Nao makerubi wakainua mabawa yao, wakapaa juu kutoka katika dunia machoni pangu, hapo walipotoka nje, nayo magurudumu yakawa kando yao; wakasimama mahali pa kuingilia pa mlango wa upande wa mashariki wa nyumba ya Bwana; na utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. Huyu ndiye kiumbe hai niliyemwona, chini ya Mungu wa Israeli, karibu na mto Kebari; nikajua ya kuwa hao ni makerubi. Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, na kila mmoja alikuwa na mabawa manne, na mifano ya mikono ya mwanadamu ilikuwa chini ya mabawa yao. Na mfano wa nyuso zao, ni nyuso zile zile nilizoziona karibu na mto Kebari; kuonekana kwao na wao wenyewe; kila mmoja walikwenda mbele moja kwa moja. |
Wimbo wa Kati. ” Zab 113: 1-2, 3-4, 5-6″
1. Aleluya. (K) Utukufu wa Bwana ni juu ya mbingu. 2. Toka maawio ya juu hata machweo yake 3. Ni nani aliye mfano wa Bwana, |
Injili. Mt 18: 15-20
Yesu aliwaamba wanafunzi wake: “Ndugu yako akikukosa enenda ukamwonye, yeye na wewe peke yenu; akikusikia, umepata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja naye tena mtu mmoja au wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa maaifa na mtoza ushuru. Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia ya kwamba wawili wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na baba yangu aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikakati yao.” |
TAFAKARI
TUBAKIE KATIKA UTUKUFU WA MUNGU KWA UTENDAJI WETU: Unabii wa Ezekiel, unatualika kutafakari utendaji wetu. Utendaji makini unatuweka katika utukufu wa Mungu ulio juu ya mbingu. Utendaji mbovu, humfanya Mungu auondoe utukufu wake kati yetu; na badala yake tunaingia katika taabu na mateso yaani maisha ya utumwa. Unabii huu ni mwaliko wa kuyatathmini maisha ya kila siku ili tuweze kufanya marekebisho kabla Mungu hajatuondolea utukufu wake na kutuacha na mahangaiko na mateso kutokana na mahusiano mabaya. Kristo anaweka mbele yetu njia ya kwenda kufanya tathmini na kujirekebisha ili kudumisha utukufu wa Mungu. Kuna msemo kuwa, “Kukosa ni ubinadamu, ila kusamehe ni hali ya kimungu.” Katika jamii tunayoishi, kuna migogoro mingi inayohitaji kusuluhishwa. Leo tumepewa mwongozo na Bwana, kwanza ni nafasi ya waliogombana kutafutana wenyewe, pili kuhusisha watu wa karibu walio na nia ya kusimamia ukweli, kisha Kanisa. Anayekataa kupatanishwa anapoteza sifa ya kuwa mfuasi wa Bwana aliyejua kusamehe. SALA: Ee Bwana tunaziombea jumuiya zetu fadhila ya kusameheana. |