Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/08/2024
2024 AGOSTI 12: JUMATATU-JUMA LA 19 LA MWAKA
Mwenyeheri Isidori Bakanja, Shahidi
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III
Somo 1. Eze 1:2-5, 24-28
Siku ya tano ya mwezi, nao ulikuwa ni mwaka wa tano wa kuhamishwa kwake mfalme Yehoyakini, neno la Bwana lilimjia Ezekieli, kuhani, mwana wa Buzi, kwa dhahiri, katika nchi ya Wakaldayo, karibu na mto Kebari. Na mkono wa Bwana ulikuwa hapo juu yake. Nikaona, na tazama, upepo wa dhoruba ulitoka upande wa kaskazini, wingu kubwa sana, pamoja na moto, ukifanya duara ya nuru, na mwangaza pande zote, na katikati yake kitu kama rangi ya kaharabu, katikati ya moto huo. Kukatokea katikati yake mfano wa viumbe hai vinne. Kuonekana kwao kulikuwa hivi; walikuwa na sura ya mwanadamu. Nao walipokwenda nalisikia mshindo wa mabawa yao, kama mshindo wa maji makuu, kama sauti yake Mwenyezi, mshindo wa mvumo, kama mshindo wa jeshi; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Tena palikuwa na sauti juu ya anga lile, lililokuwa juu ya vichwa vyao; hapo waliposimama walishusha mabawa yao. Na juu ya anga, lililokuwa juu ya vichwa vyao, palikuwa na mfano wa kiti cha enzi, kuonekana kwake kama yakuti samawi; na juu ya mfano huo wa kiti cha enzi, ulikuwako mfano kama kuonekana kwa mfano wa mwanadamu juu yake. Nikaona kana kwamba ni rangi ya kaharabu, kama kuonekana kwa moto ndani yake pande zote, tangu kuonekana kwa viuno vyake na juu; na tangu kuonekana kwa viuno vyake na chini, naliona kana kwamba ni kuonekana kwa moto; tena palikuwa na mwangaza pande zake zote. Kama kuonekana kwa upinde wa mvua, ulio katika mawingu siku ya mvua, ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwa mwangaza ule pande zote. Ndivyo kulivyokuwa kuonekana kwake mfano huo wa utukufu wa Bwana. Nami nilipoona nalianguka kifudifudi. |
Wimbo wa Katikati. Zab 148:1-2, 11-14
1. Aleluya. (K) Utukufu wako unajaza mbingu na ulimwengu. 2. Wafalme wa dunia, na watu wote, 3. Na walisifu jina la Bwana, 4. Naye amewainulia watu wake pembe, |
Injili. Mt 17:22-27
Mitume walipokuwa wakikaa Galilaya, Yesu akawaambia, Mwana wa Adamu anakwenda kutiwa katika mikono ya watu, nao watamwua, na siku ya tatu atafufuka. Wakasikitika sana. Hata walipofika Kapernaumu, wale watozao nusu-shekeli walimwendea Petro, wakasema, Je! Mwalimu wenu hatoi nusu-shekeli? Akasema, Hutoa. Naye alipoingia nyumbani, Yesu alitangulia kumwuliza, akisema, Waonaje, Simoni? Wafalme wa dunia hutwaa kodi ama ushuru kwa watu gani? kwa wana wao au kwa wageni? Naye aliposema, Kwa wageni, Yesu alimwambia, Basi, kama ni hivyo, wana ni mahuru. Lakini tusije tukawakwaza, enenda baharini ukatupe ndoana, ukatwae samaki yule azukaye kwanza; na ukifumbua mdomo wake utaona shekeli; ichukue hiyo ukawape kwa ajili yangu na kwa ajili yako. |
TAFAKARI
TUTIMIZE YANAYOTUPASA KWA UTUKUFU WA MUNGU: Neno la Mungu leo linatualika kusikia sauti yake inayotuita kwenye utukufu wa mbinguni kupitia shughuli zetu katika Kanisa lake. Mzaburi anatukumbusha kuwa uumbaji na kazi za Mungu ni tangazo la utukufu wake. “Mbingu zauhubiri utukufu wa Mungu na anga laitangaza kazi ya utukufu wake (Zab 19: 1 – 4).” Japo hivyo, katika utendaji wetu mara nyingi hatuko makini katika utendaji ili utukufu huo udhihirike. Utendaji mbaya unatufanya tupoteze utukufu wa Mungu. Ezekiel ameitwa, ili atumwe kuwakumbusha watu juu ya utukufu huu wa Mungu. Injili inaweka mbele yetu safari ya Yesu kurudi katika utukufu wa Baba wa mbinguni kwa njia ya mateso. Kama ilivyodokezwa hapo juu, utendaji wetu waweza kuwa sababu ya utukufu, au kutupotezea utukufu wa milele. Kwa njia ya mateso yake anatimiza mapenzi ya Baba yake. Nasi tunaalikwa kutimiza mapenzi ya Baba yetu hata kwa njia ya mateso ikiwa ni kwa njia hiyo tutaingia katika utukufu wa Baba. SALA: Tuombe neema ya kutimiza vema wajibu wetu hata katika mazingira magumu. |