Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 11/08/2024

2024 AGOSTI 11: DOMINIKA YA 19 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Juma III

Somo 1. 1 Fal 19: 4-8

Eliya yeye mwenyewe aliendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. Akajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko Baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule, maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.

Wimbo wa Katikati. Zab 34: 2-9

1. Nitamhimidi Bwana kila wakati wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.

(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.

2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)

3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)

4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)

Somo 2. Efe 4: 30-5:2

Msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. Hivyo mfuateni Mungu, kama watoto wanaopendwa; mkaenende katika upendo, kama Kristo naye alivyowapenda ninyi; tena akajitoa kwa ajili yetu, sadaka na dhabihu kwa Mungu, kuwa harufu ya manukato.      

Injili. Yn 6: 41-51

Wayahudi walimnung’unikia Yesu kwa sababu alisema, Mimi ni chakula kilichoshuka kutoka mbinguni. Wakasema, Huyu siye Yesu, mwana wa Yusufu, ambaye twamjua babaye na mamaye? Sasa asemaje huyu, Nimeshuka kutoka Mbinguni? Basi Yesu akajibu, akawaambia, Msinung’unike ninyi kwa ninyi. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho. Imeandikwa katika manabii, Na wote watakuwa wamefundishwa na Mungu. Basi kila aliyesikia na kujifunza kwa Baba huja kwangu. Si kwamba mtu amemuona Baba, ila yeye atokaye kwa Mungu; huyo ndiye aliyemwona Baba. Amin, amin, nawaambia, Yeye aaminiye yuna uzima wa milele. Mimi ndimi chakula cha uzima. Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kishukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akile wala asife. Mimi ndimi chakula chenye uzima kilichoshuka kutoka mbinguni; mtu akila chakula hiki, ataishi milele. Na chakula nitakachotoa mimi ni mwili wangu, kwa ajili ya uzima wa ulimwengu.  

TAFAKARI

UWEPO WA KRISTO KATI YETU NI HAKIKA YA KUUPATA UZIMA WA MILELE
Mwanadamu anao uhakika kwamba hataishi milele. Ipo siku ataiacha Dunia hii, ipo siku ya kifo chake. Pamoja na uhakika huu hakuna anayeipokea habari hii kwa furaha au kwa kujiamini. Kifo hakizoeleki. Katika hali ya kawaida mwanadamu anahangaika ili kuulinda uhai wake. Hakuna mwanadamu awe tajiri au maskini anayeweza kuudharau uhai wake. Katika hali hii unapotokea ujumbe wa kupatiwa uzima wa milele kwa hakika utapokewa kwa shahuku kubwa. Masomo ya dominika ya leo hasa somo la Injili linamwonehsa Kristo kama mkate wa kumpatia mwanadamu uzima wa milele. “Mimi ndimi chakula chenye uzima, kilichoshuka kutoka mbinguni”. Ni muhimu kuitafakari kauli hii na kuelewa maana ya ndani ya chakula hicho na uzima anaoupokea mwanadamu.
Ugumu katika kulipokea na kulielewa fumbo la umwilisho unawafanya Wayahudi kupingana na Kristo. Wanashindwa kumpokea Yeye kama mkate ushukao kutoka mbinguni. Tangu kuzaliwa kwake Wayahudi walionesha upinzani juu ya asili yake kutoka kwa Mungu. Tujikumbushe jinsi Mfalme Herode alivyokuwa na shingo ngumu katika kuamini kuzaliwa kwa Kristo baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa Mamajusi wa Mashariki. Hayo ndiyo yanayowakilishwa na ulimwengu wa leo ambao kwa kutawaliwa na mkuu wa ulimwengu huu unashindwa kuuona ukuu wa Mungu na nafsi yake katika maisha yetu. Imani yetu katika Kristo inakosa mashiko na pengine tunakosa ushawishi wa kiimani katika kuiinua jamii ya mwanadamu inayoangamia. Dominika ya leo tunagutushwa kuyapokea mafundisho ya Kristo katika imani. Ujio wake ambao unanuia kuufunua ukarimu wa Mungu kwetu uongozwe na ufunuo wa Roho Mtakatifu ili kwa njia yake tumjongee Kristo kwa imani kuu tukitarajia kuupata uzima wa milele.
Uwezo wa Mungu ndiyo unatuwezesha kulipokea na kuliamini neno lake. “Hakuna awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; name nitamfufua siku ya mwisho.” Huu ni utendaji wa Roho Mtakatifu ndani mwetu. Hii inawezekana kwa mmoja kuikana nafsi yake, kuepuka mawazo yake ya kibinadamu na kujiweka chini ya Mungu ili kufundishwa na kuelekezwa na Yeye. Roho Mtakatifu anatupeleka kwa Kristo ambaye ameshuka kutoka mbinguni na hivyo kuwa kitabu kwetu cha kuusoma ujumbe wa Mungu na kuufuata kwa ajili ya uzima wa milele. Utendaji wa Roho Mtakatifu ndani mwetu unahitaji utayari wetu wa kujifunua na kumruhusu aingie ndani mwetu. Pili kutega masikio na kuisikiliza sauti yake na tatu kutoa ushirikiano katika maongozi yake.
Kristo anakitofautisha chakula anachokitoa Yeye na ile mana waliyokula Waisraeli jangwani. “Baba zenu waliila mana jangwani; wakafa. Hiki ni chakula kichukacho kutoka mbinguni, kwamba mtu akila wala asife.” Sehemu hii ya maandiko matakatifu inaonesha mara moja undani wa mwaliko wa Kristo. Waisraeli waliipokea mana jangwani kwa sababu ya shibe ya kimwili, shibe ambayo haikuwaondoa katika mwisho wa mwanadamu wa kifo cha kimwili. Walikula na kushiba kama watu wengine na wakati wao ulipofika waliiaga dunia hii. Chakula cha Kristo ni cha kiroho, ni kile ambacho kinatupatia uzima utakaodumu hata baada ya maisha ya ulimwengu huu. Uzima huo umeelezewa na wataalamu mbalimbali wa kiroho kuwa ni uwepo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.
Dhambi inamuondoa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Na mwanadamu anayeishi bila uwepo wa Mungu ni sawa na mfu. Hii ni kwa sababu Mungu ni uwepo wa ukamilifu kwa mwanadamu. Mwaliko wa Kristo katika Injili ya Mathayo ya kutafuta ukamilifu (rej. Mt 5:48) unanuia kutufikisha katika hali ya uzima. Uwepo wa Mungu ni uzima kwani katika Yeye yote yanatendeka katika ukweli wote. Ubandia wa maisha unatokomezwa na uwepo wa Mungu. Kazi ya uumbaji iliyofanywa kwa ukamilifu iliharibiwa na mwanadamu kwa sababu ya dhambi. Hiki ndicho chanzo cha mauti. Mafarakano, magomvi, maswahibu mbalimbali; uovu na mambo yasiyofaa hutawala. Mambo haya humfanya mwanadamu kukata tamaa na kutouonja kabisa uwepo wa Mungu au kutokuona maana ya uwezo wa Mungu katika maisha yake.
Ekaristi Takatifu ni chakula kinachotupatia nguvu na uzima unaodumu kwa ajili ya utume wa kuujenga utu mpya wa mwanadamu. Utume huu unapaswa kuwa ni wa kudumu. Nabii Elia alialikwa na Mungu katika somo la kwanza kula chakula anachopewa kwa ajili ya utume ulioko mbele yake. “Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu.” Ndivyo nasi tunavyoalikwa na Kristo katika utume wa kuijenga upya jamii ya mwanadamu. Mara nyingine tunaingia katika hali ya kukata tamaa kutokana na ukinzani wa ulimwengu. Mara ngapi tunasema: “Basi! Sasa inatosha?” Ni nyakati ambazo tunaona giza mbele, hatuoni matumaini. Nyakati nyingi tunaingia katika namna ya kutouona uwepo wa Mungu au maana ya uwezo wake kwetu sisi wanadamu. Tunaitwa kumjongea Kristo katika Ekaristi Takatifu ili kwa njia yake tufike Horebu, mlima wa Mungu.
Wema wa Mungu unatualika kuwa na utegemezi kwake. Yeye ndiye anayempatia kila mmoja wetu utume wake mahsusi. Anafahamu uwepo wa vikwazo vya ulimwengu huu ambavyo ni kazi ya mwovu shetani. Anafahamu kwa hakika shetani hapendi ufalme wake uenee; ndiyo maana anaweka ndani mwetu roho ya kukata tamaa. Lakini mithili ya Nabii Elia Mungu anatuwekea mkate na gudulia la maji ili kututuliza na kutupatia nguvu. Ujio huu wa Mungu unajifunua katika Yesu Kristo anayejiweka kwetu kuwa chakula cha uzima wa milele; si chakula ambacho kinakidhi haja ya kimwili bila kutuhakikishia uzima wa milele, bali ni chakula kinachokidhi haja ya kiroho na kutupatia uzima wa kimungu ambao ni wa milele ndani mwetu. Ni wazi katika hali ya kibinadamu huwa tunaingia katika namna ya kukata tamaa kama Elia. Tunapotegemea zaidi vipaji vyetu, karama na uwezo wetu bila kumweka mwenyezi Mungu mbele. Bado tunampokea kama Yeye aliyewapatia mana waisraeli jangwani. Katika Kristo anatupatia zawadi ya nafsi yake ambayo inatupatia uzima wa milele.
Uzima anaotupatia Kristo unatutambulisha sisi wakristo katika matendo tofauti na watu wa ulimwengu huu. Matendo yanayotupeleka katika kifo cha kiroho ni yale yanayodadavuliwa na mtume Paulo katika somo la pili ambayo ni “uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano.” Matendo hayo yanapotendeka hayadhihirishi uwepo wa Mungu na kamwe hayatupeleki katika uzima wa milele. Tufanyapo uchaguzi wa matendo hayo katika uhuru wetu wa kibinadamu ni sawa na kuendelea kuitegemea mana ambayo mwisho wake ni mauti. Hivyo tunapoimarika kiimani tunaelekea kuutumia vyema uhuru wetu. Namna hiyo inatuunganisha na Kristo na hivyo kuupata uzima wa milele. Katika namna hiyo ya pili tunakuwa katika kufadhiliana sisi kwa sisi, katika huruma na kusameheana. Matendo hayo mema yanatufanya tuendelee kuuonja upendo wa Mungu katika wenzetu na kuishi kindugu.

SALA: Ee Bwana Yesu utulishe kwa Mwili wako ili tupate uzima wa milele.