Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/08/2024

2024 AGOSTI 9: IJUMAA-JUMA LA 18 LA MWAKA

Mt. Teresa Benedikta wa Msalaba
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Nah 2:1-3, 3:1-3, 6-7

Tazama juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda uziondoe nadhiri zako; kwa maana Yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali. Kwa maana Bwana anairudisha fahari ya Yakobo, kama fahari ya Israeli; maana watekao nyara wamewateka, na kuyaharibu matawi ya mizabibu yao. Ole wake mji wa damu! Umejaa mambo ya uongo na unyang’anyi; mateka hayaondoki. Kelele za mjeledi, kelele za magurudumu yafanyayo kishindo; na farasi wenye kupara-para, na magari ya vita yenye kuruka-ruka; mpanda farasi akipanda, na upanga ukimeta-meta, na mkuki ukimemetuka; na wingi wa waliouawa, na chungu kubwa ya mizoga; mizoga haina mwisho; wanajikwaa juu ya mizoga yao. Nami nitatupa uchafu uchukizao juu yako, kukufanya uwe mchafu, nami nitakufanya kuwa kitu cha kutazamwa kwa dharau. Hata itakuwa, wote wakutazamao watakukimbia, wakisema, Ninawi umeharibika; ni nani atakayeuhurumia? Nikutafutie wapi wafariji?

Wimbo wa Katikati. Kumb 32: 35-36, 39, 41

1. Maana siku ya msiba wao imekaribia,
Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka.
Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake,
Atawahurumia watumwa wake.

(K) Naua mimi, nahuisha mimi.

2. Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye.
Wala hapana Mungu mwingine ila mimi;
Naua Mimi, nahuisha mimi,
Nimejeruhi, tena naponya. (K)

3. Nikiuona upanga wangu wa umeme,
Mkono wangu ukishika hukumu,
Nitawatoza kisasi adui zangu,
Nitawalipa wanaonichukia. (K)

Injiili. Mt 16:24-28

Wakati huo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. Amin, nawaambieni, Pana watu katika hawa wasimamao hapa, ambao hawataonja mauti kabisa, hata watakapomwona Mwana wa Adamu akija katika ufalme wake.

TAFAKARI.

TUMFUATE YESU KWA UAMINIFU: Lengo la kufanya Agano na Mungu lilikuwa kupata ulinzi na mafanikio katika ufuasi wetu. Unabii wa Nahumu unaweka wazi utimilifu wa maagano hayo, uaminifu wa Mungu kwa kuwaadhibu adui za wale wanaomwamini. Tunaishi katika mifumo iliyojaa maadui katika ngazi zote. Kama tumeshikamana na Mungu kwa kuishi kiaminifu imani na viapo vingine vyenye lengo la kudumisha imani, ikiwa ni pamoja na wale wanaofanya viapo na kuhitimisha, “Ee Mwenyezi Mungu nisaidie.” Tutende kadiri ya maagano na viapo hivyo, nasi tutaonja baraka na ulinzi wa Mungu. Injili inaweka wazi mbele yetu kuwa watakaodumu waaminifu katika ufuasi machoni mwa dunia wanaweza kuonekana kama wanapoteza, lakini mbele ya Mungu uaminifu katika ufuasi ni uwekezaji wa uhakika. Yesu ametuweka wazi kuwa malipo yatatokana na utendaji wetu! Wale wachache tunaowaona kuwa wanapoteza, ndio hao ambao Bwana amesema hawataonja mauti kabisa, hata watakaposhuhudia ufalme wa Mungu ukisimama. 

SALA: Ee Yesu utusaidie tufanye maamuzi ya kukufuata Wewe bila kuhesabu gharama.