Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 08/08/2024

2024 AGOSTI 8: ALHAMISI -JUMA LA 18 LA MWAKA

Mt. Dominiko, Padre
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Yer 31:31-34

Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda. Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana. Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.

Wimbo wa Katikati. Zab 51: 12-15, 18-19

1. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.

(K) Ee Mungu, uniumbie moyo safi.

2. Unirudishie furaha ya wokovu wako; Unitegemeze kwa roho ya wepesi. Nitawafundisha wakosaji njia zako, Na wenye dhambi watarejea kwako. (K)

3. Maana hupendezwi na dhabihu, au ningeitoa, Wewe kuridhi sadaka ya kuteketezwa. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjia; Moyo uliovujika na kupondeka,
Ee Mungu, hutadharau. (K)

 

Injili. Mt 16:13-23

Yesu alienda pande za Kaisaria-Filipi, akawauliza wanafunzi wake akasema, Watu hunena Mwana wa Adamu kuwa ni nani? Wakasema, Wengine hunena u Yohane Mbatizaji, wengine Eliya, wengine Yeremia au mmojawapo wa manabii. Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani? Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiye Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai. Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali baba yangu aliye mbinguni. Nami nakuambia, Wewe ndiwe Petro, na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu; wala milango ya kuzimu haitalishinda. nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lolote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lolote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni; Ndipo alipowakataza sana wanafunzi wake wasimwambie mtu yeyote ya kwamba yeye ndiye Kristo. Tangu wakati huo Yesu alianza kuwaonya wanafunzi wake ya kwamba imempasa kwenda Yerusalemu, na kupata mateso mengi kwa wazee na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuwawa, na siku ya tatu kufufuka. Petro akamchukua akaanza kumkemea, akisema, hasha, Bwana, hayo hayatakupata. Akageuka, akamwambia Petro, Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, Bali ya wanadamu.

TAFAKARI. 

MIOYO YETU IWE TAYARI, ILI MUNGU AANDIKE SHERIA YAKE NDANI YAKE:  Ni kwa mapendo ya ajabu Mungu anajifunga na wanadamu kwa njia ya agano lake. Agano ni makubaliano ya pande mbili. Hili la leo ni Mungu anakuja kwetu kutaka kujifunga nasi, ili awe Mungu wetu atulinde na kututunza katika njia ya imani. Maagano yaliyotangulia, hati zake zilikuwa nje ya mioyo ya walifanya agano. Tofauti na maagano yote, hili ambalo nyakati zake ni timilifu, amesema ataandika na kutia sheria zake ndani ya mioyo yetu. Tuitoe mioyo yetu ili Mungu atupe miongozo sahihi ya maisha, tupate kuwa salama. Injili itatutaka tukiri imani kwa Mungu tunayemwamini. Leo, sisi tunaomfuata Kristo anataka tutamke waziwazi kuwa yeye ni nani katika maisha yetu. Tukumbuke kuwa imekua rahisi kusema wengine wanasemaje kuhusu Yesu. Tutamke wazi lile lililoandikwa katika mioyo yetu ambalo ni Imani, ituwezeshe kusema kuwa, “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu aliye hai.” Imani yetu ndiyo msingi wa Kanisa. Tuwe imara, tusiyumbe katika imani.

SALA: Ee Bwana Yesu utujalie ujasiri wa kukukiri wewe waziwazi.