Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 03/08/2024

2024 AGOSTI 3: JUMAMOSI-JUMA LA 17 LA MWAKA

Mt. Petro Juliani Eymardi, Padre na Mwanzilishi wa Shirika
Rangi: Nyeupe

Zaburi: Juma 1

Somo 1. Yer 26:11-16, 24

Makuhani na manabii, waliwaambia wakuu na watu wote, wakisema, mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu. Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma kuitabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia. Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu. Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu. Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia; itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia. Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana, Mungu wetu. Mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ulikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

Wimbo wa KAtikati. Zab 69: 15-16, 30-31, 33-34

1. Mungu na atufadhili na kutubariki, Na kutuangazia uso wake. Njia yake ijulikane duniani, Wokovu wake katikati ya mataifa yote.

(K) Kwa wingi wa fadhili zako unijibu, Ee Mungu

2. Mataifa na washangilie, Naam, waimbe kwa furaha, Maana kwa haki utawahukumu watu, Na kuwaongoza mataifa walioko duniani.(K)

3.  Nchi imetoa mazo yake; Mungu, Mungu wetu, ametubariki. Mungu atatubariki sisi; Miisho yote ya dunia itamcha Yeye.(K)

Injili. Mt 14:1-12

Mfalme Herode alisikia habari za Yesu, akawaambia watumishi wake, Huyo ndiye Yohane Mbatizaji; amefufuka katika wafu; na kwa hiyo nguvu hizo zinatenda kazi ndani yake. Maana Herode alikuwa amemkamata Yohane, akamfunga, akamtia gerezani, kwa ajili ya Herodia, mke wa Filipo nduguye. Kwa sababu Yohane alimwambia, Si halali kwako kuwa naye. Naye alipotaka kumwua, aliwaogopa watu, maana walimwona Yohane kuwa nabii. Hata ilipofika sikukuu ya kuzaliwa kwake Herode, binti Herodia alicheza mbele ya watu, akampendeza Herode. Hata akaahidi kwa kiapo ya kwamba atampa lo lote atakaloliomba. Naye, huku akichochewa na mamaye, akasema, nipe hapa katika kombe kichwa cha Yohane Mbatizaji. Naye mfalme akasikitika; lakini kwa ajili ya viapo vyake, na kwa ajili ya wale walioketi chakulani pamoja naye, akaamuru apewe; akatuma mtu, akamkata kichwa Yohane mle gerezani.  Kichwa chake kikaletwa katika kombe, akapewa yule kijana; akakichukua kwa mamaye. Wanafunzi wake wakaenda, wakamchukua yule maiti, wakamzika; kisha wakaenda wakampasha Yesu habari.

TAFAKARI

MAHUSIANO YETU YAMPENDEZE MUNGU: Unabii ni sauti ya Mungu anayesema na wanadamu kupitia mwanadamu. Nabii alitumwa kuwaalika watu wafanye mabadiliko, na badala ya kupokea ujumbe, wameugeuza na kuarifu uongozi kuwa Yeremia amefanya uchochezi na hivyo anastahili kufa. Nabii amejiweka mikononi mwao akiwaambia, yeye ametumwa na Mungu na kwa kuwa ameshafikisha ujumbe wa Mungu kwao, wanatakiwa kufanya mabadiliko ili kukaribisha neema za Mungu, vinginevyo wakiamua kumwua, wajue matokeo yake yatakuwa laana kwa taifa. Tuwapokee waliotumwa kwetu kwa maonyo; na tufanye mabadiliko. Sauti ya Yohane Mbatizaji ni ya kinabii, aliyetumwa kumwonya mfalme Herode. Mungu anatetea agano la ndoa kwa kuwakumbusha wote bila kujali nafasi zao kiuongozi kwa maneno, “Si halali kuwa na mke wa mwenzako.” Kati yetu wako baadhi wanaoendekeza tabia hiyo, leo wajifunze katika kisa hiki, na wamsikie Mungu akisema, “Si halali kwa yeyote kuishi maisha ya mahusiano yasiyompendeza Mungu na Kanisa lake.”

Sala: Ee Bwana utuepushe moyo mgumu ili tupate kuyashika maagizo yako.