Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 31/07/2024
2024 JULAI 31: JUMATANO-JUMA LA 17 LA MWAKA
Mt. Ignasi wa Loyola, Padre
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 1
Somo 1. Yer 15:10, 16-21
Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani. Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, ee Bwana, Mungu wa majeshi. Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi; naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu. Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu? Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao. Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana. Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, ame nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha. |
Wimbo wa Katikati. Zab 59:2-4, 10-11, 17, 18
1. Ee Mungu wangu, uniponye na adui zangu, Uniinue juu yao wanaoshindana nami. Uniponye nao wafanyao maovu, (K) Bwana alikuwa ngome yangu siku ya shida yangu. 2. Kwa maana wanaiotea nafsi yangu; 3. Ee nguvu zangu, nitakungoja wangu, Maana Mungu ndiye aliye ngome yangu. Mungu wa fadhili zangu atanitangulia, Mungu atanijalia kuwatazama adui zangu. (K) 4. Nami nitaziimba nguvu zako asubuhi, |
Injili. Mt 13:44-46
Yesu aliwaambia makutano mifano, Ufalme wa Mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Tena Ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote, akainunua. |
TAFAKARI
THAMANI YA UFALME WA MUNGU: Katika somo la kwanza Mungu anamhakikishia nabii Yeremia kuwa atakuwa naye; “maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya (Yer. 15:20).” Mungu anahidi kuwa naye kwa kuwa anayatenda ya Mungu, anawajulisha watu wa Mungu yawapasayo, wapo wanayoyasikia na kupingana nayo. Kwa hakikisho la Mungu kuwa naye, Yeremia anastawi katika ujasiri wa kutenda yale anayoyataka Mungu. Katika Injili Kristo anatufundisha ufalme wa Mungu umefanana na hazina iliyositirika katika shamba. Mtu alipoigundua hiyo hazina, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote, akalinunua shamba lile. Mwanadamu anapaswa pia kutambua kuwa Mungu yupo pamoja naye. Yaani tunapotumbua mwenye uweza wote amenisimamia tunakuwa jasiri, tunaweka matumaini yetu kwake. Tunapoweka matumaini yetu kwake ni sawa na kuitunza hazina yetu kwake kwani twajua hatuwezi lolote bila yeye. Thamani ya ufalme wa Mungu ni kuacha mengine yote; kuwaza na kuishi kadiri ya mapenzi ya ufalme huo wa Mungu. Sala: Ee Bwana neema yako iniwezeshe kuwaza na kutenda mema. Amina. |