Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 22/07/2024
2024 JULAI 22: JUMATATU-JUMA LA 15 LA MWAKA
Mt. Maria Magdalena
Rangi: Nyeupe
Zaburi: Juma 4
Somo 1. Wim 3:1-4
Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, nalimtafuta nisimpate. Nikasema,Haya, niondoke nizunguke mjini, katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, nikamwona mpendwa wa nafsi yangu. |
Wimbo wa Katikati. Zab 63:1-5, 7-8
1. Ee Mungu, Mungu wangu, nitakutafuta mapema, (K) Nafsi yangu inakuonea kiu ee Bwana. 2. Ndivyo nilivyo kutazama katika patakatifu, 3. Ndivyo nitakavyokubariki maadamu ni hai; Kwa jina lako nitaiinua mikono yangu. 4. Maana wewe umekuwa msaada wangu, |
Injili. Yn 20:1-2, 11-18
Siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalena alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simon Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walipomweka. Lakini Mariamu alikuwa akisimama karibu na kaburi, nje yake, analia. Basi akilia hivi, aliinama na kuchungulia ndani ya kaburi. Akaona malaika wawili, wenye mavazi meupe, wameketi, mmoja kichwani na mmoja miguuni, hapo ulipolazwa mwili wake Yesu. Nao wakamwambia, Mama, unalilia nini? Akawaambia, Kwa sababu wamemwondoa Bwana wangu, wala mimi sijui walikomweka. Naye akiisha kusema hayo,akageuka nyuma, akamwona Yesu amesimama, asijue ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, Mama, unalilia nini? Unamtafuta nani? Naye, huku akidhania yakuwa ni mtunza bustani, akamwambia, Bwana, ikiwa umemchukua wewe, uniambie ulipomweka, nami nitamwondoa.Yesu akamwambia, Mariamu. Yeye akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Raboni! (yaani, Mwalimu wangu). Yesu akamwambia, Usinishike; kwa maana sijapaa kwenda kwa Baba. Lakini enenda kwa ndugu zangu ukawaambie, Ninapaa kwenda kwa Baba yangu naye ni Baba yenu, kwa Mungu wangu naye ni Mungu wenu. Mariamu Magdalena akaenda, akawapasha wanafunzi habari ya kwamba, Nimemwona Bwana, na ya kwamba amemwambia hayo. |
TAFAKARI.
KRISTO APATE NAFASI MOYONI MWAKO: Maria Magdalena ni mmoja wa wadhambi waliotambua kwa kusamehewa, Kristo alimtendea makuu katika maisha yake na akampenda kwa moyo wake wote. Ni bayana kuwa Maria Magdalena alipenda kuwa alipokuwa Kristo andelee kuonja na kufurahia upendo na huruma yake ya Kimungu. Hilo lilimsukuma kufuatana na Kristo katika utume wake hapa duniani, hata alipouawa aliwahi penye kaburi la Kristo asubuhi na mapema kukiwa bado na giza. Alikuwa wa kwanza kugundua kuwa kaburi la Kristo halikuwa katika hali yake ya kawaida, aliwapa taarifa Simoni Petro na Mwanafunzi ambaye Kristo alimpenda. Hakujua nini kilichotokea kwamba mwili wa Kristo haupo kaburini, alilia kwa kumkosa Mpendwa wa moyo wake. Ni kwa Upendo huo Kristo anamkirimia zawadi ya kuwa Mtume wa kwanza wa ufufuko. Kwa Maisha ya Mtakatifu Maria Magdalena tunajifunza kujitoa kweli kwa Kristo kama mpendwa wa moyo wa nafsi, tuungane naye muda wote. Tunaweza fanya hivyo kwa kupenda kusoma, kutafakari, kuyaishi Maandiko Matakatifu na Mafundisho ya Kanisa. Sala: Ee Bwana utuwezeshe kuutafakari utakatifu wako siku zote za maisha. |