Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 21/07/2024

2024 JULAI 21: DOMINIKA YA 16 YA MWAKA

Rangi: Kijani
Zaburi: Tazama Sala  ya Siku

Somo 1. Yer 23: 1-6

Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! asema Bwana. Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana. Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka. Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana. Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi. Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama; na jina lake atakaloitwa ni hili Bwana ni haki yetu. 

Wimbo wa Katikati. Zab 23:1-6

1. Bwana ndiye mchungaji wangu,
Sitapungukiwa na kitu.
Katika malisho ya majani mabichi hunilaza,
Kando ya maji ya utulivu huniongoza,
Huniuhisha nafsi yangu.

(K) Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu.

2. Huniongoza katika njia za haki kwa ajili ya jina lake,
Naam, nijapopita kati ya bonde la uvuli wa mauti,
Sitaogopa mabaya,
Kwa maana Wewe upo pamoja nami,
Gongo lako la fimbo yako vyanifariji. (K)

3. Waandaa meza mbele yangu,
Machoni pa watesi wangu.
Umenipaka mafuta kichwani pangu,
Na kikombe changu kinafurika. (K)

4. Hakika wema na fadhili zitanifuata
Siku zote za maisha yangu,
Nami nitakaa nyumbani mwa Bwana milele. (K)

Somo 2. Efe 2: 13-18

Katika Kristo Yesu, ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga. Naye akiisha kuuondoa ule uadui kwa mwili wake; ndiyo sheria ya amri zilizo katika maagizo; ili afanye hao wawili kuwa mtu mpya mmoja ndani ya nafsi yake; akafanya amani. Akawapatanisha wote wawili na Mungu katika mwili mmoja, kwa njia ya msalaba, akiisha kuufisha ule uadui kwa huo msalaba. Akaja akahubiri amani kwenu ninyi mliokuwa mbali, na amani kwao wale waliokuwa karibu. Kwa maana kwa yeye sisi sote tumepata njia ya kumkaribia Baba katika Roho mmoja.

Injili. Mk 6: 30-34

Mitume walikusanyika mbele ya Yesu; wakampa habari za mambo yote waliyoyafanya na mambo yote waliyoyafundisha. Akawaambia, Njoni ninyi peke yenu kwa faragha; mahali pasipokuwa na watu, mkapumzike kidogo. Kwa sababu walikuwako watu wengi, wakija, wakienda, hata haikuwapo nafasi ya kula. Wakaenda zao faragha mashuani, mahali pasipokuwa na watu. Watu wakawaona wakienda zao, na wengi wakatambua, wakaenda huko mbio kwa miguu, toka miji yote, wakatangulia kufika. Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi.  

TAFAKARI

BIDII KATIKA UTUME
Mwenyezi Mungu amemuumba mwanadamu na kumpatia cheo kikubwa sana. Kitabu cha mwanzo kinaelezea majukumu ya mwanadamu katika kazi yote ya uumbaji. Mwenyezi Mungu alisema: “Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi, na kuitiisha…” (Mw 1:28). Mwanadamu amepewa jukumu la kuiratibu dunia hii; kuifanya jamii ya mwanadamu na uumbaji wote kuweza kuuonja wema wa Mungu.Hivyo, shughuli zetu na wajibu mbalimbali katika ulimwengu wa leo zinapaswa kuufunua uso wa Mungu kwa mwanadamu na uumbaji wote. Sisi wanadamu tunapaswa kujibidiisha katika utume wetu kwa nafasi mbalimbali tukitambua kwamba asili yake ni Mungu na Yeye ndiye ameweka nia fulani kusudi kupitia wewe au mimi katika utumishi wangu ulimwengu uendelee kuwa mahali pazuri.
Uzembe, kutokujali na kuyatupilia pembeni makusudi ya Mungu katika uumbaji hakumuachi salama mwanadamu. Hali hii hutuweka katika dosari mbili: kwanza tunakuwa wezi na kukosa uaminifu katika kazi ya Mungu na pili tunaiharibu kazi ya uumbaji anayotupatia mwenyezi Mungu.Somo la kwanza linatuonesha hali hiyo katika sura ya wachungaji waovu. “Ole wao wachungaji wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana”. Hii inawakilisha wale wanaopewa majukumu kuiratibu jamii lakini wanaishia kujiwekezea na kujinenepesha wao wenyewe. Ni Ukumbusho kwetu kuwa nyajibu zozote tuzipokeazo katika jamii ni kwa ajili ya ustawi wa jamii nzima. Hakuna nafasi yoyote anayokasimiwa mtu kwa ajili yake binafsi, bali ni kwa ajili ya jamii nzima.
Mwanadamu anapomuondoa Mwenyezi Mungu katika utume wake hutawaliwa na ubinafsi. Nafasi ya Mungu kama Baba wa uumbaji wote huondolewa na nia yake njema ya kuvistawisha vyote itafutiliwa mbali. Sauti yake kamwe haitosikiwa na kila mtendaji atajitengenezea taratibu zake. Hali hii huleta athari mbalimbali kwa wale anatarajiwa kuwahudumia. Kwanza ni “kutawanya kundi.” Ubinafsi unaleta mgawanyiko kati ya watu na wakati mwingine unamtenga mtu na uumbaji wote. Hivyo hujenga uadui kati ya mtu na mtu na matumizi mabovu ya utajiri wa ulimwengu. Hakuna atakayeweza kuisikia sauti ya anayelia kutaka msaada.
Athari ya pili ni “kuwafukuza” kondoo. Hii ni katika kuwanyang’anya haki zao kama raia wa jamii ya mwanadamu; kuwanyang’anya haki zao kama wana wa Mungu. Tamaa ya mwanadamu inaingia na matokeo yake kuupora uhuru wa mwingine. Tendo la kufukuza kwa ufupi linaonekana katika kuufuta uwepo wa ndugu yako katika uso wa dunia. Kwa upande wa uumbaji wote hujidhihirisha katika maangamizi ya “ekolojia” nzima bila kujali uhifadhi wake. Mwanadamu anaingia katika uovu wa kumgeuza mwanadamu mwenzake kuwa chombo chake cha kumtendea kazi kwa kuwa utu na heshima yake katika jamii ya mwanadamu imepotea. Ndiposa matendo kama rushwa, kuporana haki, dhuluma na kudhalilishana yanapostawi.
Athari ya tatu ni “kutokuwatazama kondoo.” Hii ni kutokuwajali na kuwapatia mahitaji yao ya msingi. Uzembe na kuuzia uwepo na umuhimu wa wale wanaokuzunguka huifunua hali hii ya kutowatazama kondoo. Hali hii inaonekana katika jamii ya leo kiuchumi, jamii ambayo haimtazami mtu katika utu wake bali katika huduma yake ambayo kipato na kumkuza mmoja kiuchumi. Misemo kama “mkono mtupu haulambwi” huchochea hali hii. Macho yetu yamefumbwa kiasi cha kushindwa kuwaona wahitaji kama wagonjwa na maskini. Tunavutika zaidi kuwaangalia wale ambao watatujaza na kutuneemesha kiuchumi au kutupatia umaarufu wa kisiasa.
Injili ya leo inatoa njia ya kupambana na hali hiyo na kuifafanua zaidi sehemu ya pili ya somo la kwanza, yaani kutuonesha haiba ya wachungaji wema. Kristo anaitimiza kauli ya Mungu anayosema kwa kinywa cha nabii Yeremia akisema: “Tazama siku zitakuja… nitakapomchipushia Daudi chipukizi la haki; naye atamiliki ufalme, atatenda kwa Hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi”. Kwanza hali hiyo inaonekana katika kazi za mitume ambao waliotumwa na Kristo kama tulivyoona Dominika iliyopita. Uaminifu katika utume na kulitekeleza neno la Kristo ndiko kuliwawezesha kupata ufanisi huo. Ni ukumbusho kwetu kubaki waaminifu na kutekeleza yote kadiri ya mapenzi ya Mungu.
Kristo anaendelea kujionesha Yeye mwenyewe kama mfano bora wa Mchungaji Mwema. “Naye aliposhuka mashuani, akaona mkutano mkuu, akawahurumia; kwa sababu walikuwa kama kondoo wasio na mchungaji; akaanza kuwafundisha mambo mengi”. Mambo matatu yanajitokeza hapa. Kwanza ni kuona, yaani kutambua uwepo wa walio na uhitaji wa huruma ya Mungu. Hali ni kinyume na wachungaji waovu waliojifikiria wenyewe. Tendo la kuona linadhihirisha utayari wa kutoka ndani ya nafsi yake na kuutambua uwepo wa mmoja aliye pembeni yako na siyo kutambua tu bali kuwa tayari kuitazama hali yake.
Kristo alipowaona katika hatua ya pili aliwahurumia. Tendo la huruma linaonesha moyo ulioona maswahibu, mahangaiko au mateso ya moyo mwingine. Hii ni hatua ambayo inauunganisha moyo mmoja na moyo mwingine. Hii ni tabia ya kimungu. Hatua hii humfanya mmoja kufikiri, kuteseka na kuiishi hali ya mwingine. Ndilo analokumbusha Baba Mtakatifu Fransisko juu ya umuhimu wa mchungaji kuwa na harufu ya kondoo. Shida zao kuwa ni sehemu yako. Hii hutupeleka katika hatua ya tatu ambayo ni kufanya kitu; kutenda ili kuiondoa hali mbaya inayomsonga jirani yako. Yeye anayeona huruma habaki katika hali ya kuona huruma tu bali anatenda. Kinyume chake anaweza kuonekana anakebehi hali ya mwingine. Pia tendo la kuona huruma kama hali ya kimungu hudhihirisha uwepo wa uwezo wa kukirekebisha kile kilichosababisha hali mbaya.
Moja ya sumu kubwa inayosababisha utendaji mbovu wa utume wetu ni upendeleo katika jamii ya wanadamu. Watendaji wengi huingia katika dhambi hiyo kwa kuwabagua watu kadiri ya vipato vyao, rangi zao, dini zao au hata makabila yao. Undugu wetu wa kibinadamu unapata ufa kwa sababu ya migawanyiko hiyo ya kijamii. Kwetu Wakristo hali hiyo ni kinyume na namna yetu. Sote tunafanyika kuwa wana wa Mungu na tumekombolewa na Damu Azizi ya Kristo. Mtume Paulo anakumbusha akisema: “Katika Kristo Yesu, Ninyi mliokuwa mbali hapo kwanza mmekuwa karibu kwa damu yake Kristo. Kwa maana Yeye ndiye amani yetu, aliyetufanya sisi sote tuliokuwa wawili kuwa mmoja; akakibomoa kiambaza cha kati kilichotutenga”.

SALA: Ee Bwana Yesu tunakuomba utujalie moyo wa toba.