Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 20/07/2024

2024 JULAI 20: JUMAMOSI-JUMA  LA 15 LA MWAKA

Mt. Apolinari
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

Somo 1. Mik 2:1-5

Ole wao wakusudiao mambo maovu, na kutenda mabaya vitandani mwao! Kunapopambazuka asubuhi huyafanya, kwa sababu ya katika uwezo wa mikono yao. Nao hutamani mashamba, na kuyashika; na nyumba pia, nao huzichukua; nao humwonea mtu na nyumba yake, naam, mtu na urithi wake. Basi Bwana asema hivi,”Angalia, nakusudia jambo baya juu ya jamaa hii, ambalo hamtazitoa shingo zenu, wala hamtakwenda kwa kiburi; kwa maana ni wakati mbaya. Siku hiyo watatunga mithali juu yenu, na kuomboleza kwa maombolezo ya huzuni nyingi, na kusema, ‘Sisi tumenyanganyiwa kabisa! Yeye analibadili fungu la watu wangu; jinsi anavyoniondolea hilo! Awagawia waasi mashamba yetu.” Kwa hiyo hutakuwa na mtu atakayeitupa amba kwa kura katika mkutano wa Bwana.

Wimbo wa Katikati. Zab 10:1-4, 7-8, 14

1.   Ee Bwana, kwa nini wasimama mbali?
Kwani kujificha nyakati za shida?
Kwa kiburi chake asiye haki
Mnyonge anafuatiwa kwa ukali;
Na wanaswe kwa hila zizo hizo walizoziwaza.

(K) Usiwasahau wanyonge, ee Bwana.

2. Maana mdhalimu hujisifia tamaa ya nafsi yake,
Na mwenye choyo humkana Bwana na kumdharau.
Mdhalimu kwa kiburi cha uso wake
Aseme, Hatapatiliza.
Jumla ya mawazo yake ni, hakuna Mungu. (K)

3. Kinywa chake kimejaa laana,
Na hila na dhuluma.
Chini ya ulimi wake kuna madhara na uovu,
Hukaa katika maoteo ya vijiji.
Mahali pa siri humwua asiye na hatia,
Macho yake humvizia mtu duni. (K)

4. Umeona, maana unaangalia madhara na jeuri,
Uyatwae mkononi mwako.
Mtu duni hukuachia nafsi yake,
Maana umekuwa msaidizi wa yatima. (K)

Injili. Mt 12:14-21

Mafarisayo walitoka wakafanya shauri juu ya Yesu jinsi ya kumwangamiza. Naye Yesu hali akiyafahamu hayo akaondoka huko; na watu wengi wakamfuata; akawaponya wote, akawakataza wasimdhihirishe; ili litimie neno lililonenwa na nabii Isaya, akisema, Tazama, mtumishi wangu niliyemteua; mpendwa wangu, moyo wangu uliyependezwa naye; nitatia roho yangu juu yake, naye atawatangazia Mataifa hukumu. Hatateta wala hatapaza sauti yake; wala mtu hatasikia sauti yake njiani. Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima, hata ailetapo hukumu ikashinda. Na jina lake Mataifa watalitumainia.

TAFAKARI.

AMANI NI TUNDA LA HAKI NA UTUNZAJI WA UUMBAJI: Haki kama thamani ni kanuni ya maadili ya kila mtu ambaye anaamua kuishi akimpa kila mmoja kile kinacholingana na halali yake. Haki ni adili ambayo watu wote lazima watekeleze kwa njia thabiti na kutafuta manufaa yao na ya jamii. Viongozi wa dini ya Kiyahudi hawakufurahia namna Kristo alivyokuwa akihubiri habari njema ya wokovu wetu. Yesu muda wote alionesha ukaribu wake na maskini, wajane, wagonjwa na wadhambi. Alifanya hivyo akiwaonesha kuwa ni wa thamani na akiwapa heshima ya utu. Huu unapaswa kuwa ni utume wetu leo. Maskini mara nyingi wananyanyasika na wapo wachache wanaojali utu wao na kuwasaidia. Hata yeyote anayejishughulisha na mambo hayo ya maskini wanakutana na changamoto mbalimbali. Tunapaswa kutangaza haki kwa maneno na matendo yetu ambayo ni muhimu sana kupata amani na maendeleo. Wapo wengi wanaoteseka kwa sababu ya ukosefu wa haki na kwa mateso hayo hawana amani. 

Sala: Ee Bwana utuwezeshe kutambua haki na kumpa kila mmoja haki ya utu kwa manufaa ya jamii.