Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 19/07/2024

2024 JULAI 19: IJUMAA-JUMA  LA 15 LA MWAKA

Mt. Makrina, Bikira
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 3

Somo 1. Isa 38:1-6, 21-22, 7-8

Siku hizo Hezekia aliugua, akawa katika hatari ya kufa; na Isaya nabii, mwana wa Amosi, akaenda kwa mfalme, akamwambia, “Bwana asema hivi, tengeneza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.” Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana, akasema, “Ee Bwana, kumbuka haya, nakusihi kwamba nimekwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako.” Hezekia akalia sana sana. Kisha neno la Bwana likamjia Isaya, kusema, “Enenda ukamwambie Hezekia, Bwana, Mungu wa Daudi, baba yako, asema hivi,”Mimi nimeyasikia maombi yako, nimeyaona machozi yako; tazama, nitaziongeza siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano. Nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu. Basi Isaya akasema,”Na watwae mkate wa tini, wakauweke juu ya jipu, naye atapona.” Tena Hezekia alikuwa amesema, iko ishara gani ya kunionyesha ya kuwa nitapanda niingie nyumbani mwa Bwana?” Jambo hili liwe ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kuwa Bwana atalitimiza jambo hili alilolisema; Tazama, nitakirudisha nyuma kivuli madaraja kumi, ambayo kilishuka juu ya duara ya Ahazi kwa sababu ya jua. Basi jua likarudi madaraja kumi katika hiyo duara, ambayo limekwisha kushuka.

Wimbo wa KAtikati. Isa 38:10-12, 16

1. Nalisema, katika usitawi wa siku zangu
Nitakwenda kuingia malango ya kuzimu;
Nimenyimwa mabaki ya miaka yangu.

(K) Umeniokoa na shimo la uharibifu, ee Bwana.

2.  Nalisema, sitamwona Bwana, yeye Bwana,
Katika nchi ya walio hai;
Sitamwona mwanadamu tena pamoja na hao
wakaao duniani. (K)

3.    Kao langu limeondolewa kabisa,
Limechukuliwa kama hema ya mchungaji;
Nimekunja Maisha yangu kama mfumaji.
Atanikatilia mbali na kitanda cha mfumi;
Tangu mchana hata usiku wanimaliza. (K)

4.   Ee Bwana kwa mambo hayo watu huishi;
Na uhai wa roho yangu u katika hayo yote;
Kwa hiyo uniponye na kunihuisha. (K)

Injili. Mt 12:1-8

Wakati ule Yesu alipita katika mashamba siku ya Sabato; wanafunzi wake wakaona njaa, wakaanza kuvunja masuke, wakala, na Mafarisayo walipoona, walimwambia,” Tazama! Wanafunzi wako wanafanya neno ambalo si halali kulifanya siku ya sabato. Akawaambia, “Hamkusoma alivyotenda Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wenziwe? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaila mikate ile ya w onyesho, ambayo si halali kwake kuila wala kwa wale wenziwe, ila kwa makuhani peke yao? Wala hamkusoma katika torati, kwamba siku ya sabato makuhani hekaluni huinajisi sabato wasipate hatia? Lakini nawaambieni, kwamba hapa yupo aliye mkuu kuliko hekalu. Lakini kama mngalijua maana yake maneno haya, Nataka rehema, wala si sadaka, msingaliwalaumu wasio na hatia. Kwa maana Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.”

TAFAKARI.

MSINGI WA DINI NI UPENDO NA HURUMA MUNGU: Hezekia anatambua thamani ya Upendo wa Mungu kwa mfano wa mwanadamu anayemkimbilia Mungu katika sala na Mungu anajibu sala yake. Huyu ni tofauti na Mafarisayo walioshindwa kutambua upendo na huruma ya Mungu wakishikilia tu sheria. Walichokuwa wanafanya mafarisayo chaweza kufananishwa na mfano huu: Hebu fikiri kuwa mwanao anaadhimisha siku ya kuzaliwa kwake, unamfanyia sikukuu kubwa na akapewa zawadi nyingi, alipozifungua zawadi hizo alitunza karatasi zilizofungia zawadi na kutupa zile zawadi kwenye mashine ya kuchakata takataka. Huu mfano wa kusikitisha unatufikirisha walivyokuwa wakifanya Mafarisayo kwenye dini. Kutunza sheria ilionekana kuwa ya muhimu zaidi kuliko kuishi kwa upendo na huruma. Wafarisayo waliudhi, kwani waliibadili dini iliyokuwa nzuri kuwa kitu kibaya au cha kuchukiwa kisichokuwa na upendo ndani mwake. Waliifanya dini ionekane kuwa kitu tofauti na kile Mungu alichokitaka. Walikuwa wanatupa zawadi ya Mungu na kutunza karatasi iliyotunza zawadi. 

Sala: Ee Mungu utuwezeshe kutambua vema zawadi unazotukirimia kuzipokea na kuzitunza.