Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 18/07/2024
2024 JULAI 18: ALHAMISI-JUMA LA 15 LA MWAKA
Mt. Kamili wa Lelis, Padre
Rangi: Kijani
Zaburi: Juma 3
Somo 1. Isa 26:7-9, 12, 16-19
Njia yake mwenye haki ni unyofu; wewe uliye mnyofu wainyosha njia ya mwenye haki. Naam, katika njia ya hukumu zako sisi tumekungoja, Ee Bwana; shauku ya nafsi zetu inaelekea jina lako na ukumbusho wako. Kwa nafsi yangu nimekutamani wakati wa usiku; naam, kwa nafsi yangu ndani yangu nitakutafuta mapema; maana hukumu zako zikiwapo duniani, watu wakaao duniani hujifunza haki. Bwana, utatuamuria amani; maana ni wewe pia uliyetutendea kazi zetu zote. Bwana, katika taabu zao walikwenda kwako; waliomba maombi mengi wakati adhabu yako ilipokuwa juu yao. Kama vile mwanamke mwenye mimba anayekaribia wakati wake wa kuzaa, alivyo na utungu na kulia kwa sababu ya maumivu yake, ndivyo tulivyokuwa sisi mbele zako, Ee Bwana. Tumekuwa na mimba, tumekuwa na utungu, tumekuwa kana kwamba tumezaa upepo; hatukufanya wokovu wo wote duniani, wala hawakuanguka wakaao duniani. Wafu wako wataishi, maiti zangu zitafufuka; amkeni, kaimbeni, ninyi mnaokaa mavumbini, kwa maana umande wako ni kama umande wa mimea, nayo ardhi itawatoa waliokufa. |
Wimbo wa Katikati. Zab 102:13-19, 21
1. Wewe, Bwana, utaketi ukimiliki milele, (K) Toka mbinguni Bwana ameangalia nchi. 2. Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, 3. Kizazi kitakachokuja kitaandika hayo, |
Injili. Mt 11:28-30
Yesu aliwaambia makutano: “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi.” |
TAFAKARI
KRISTO ANATUKARIBISHA KUPUMZIKA: Baada ya meli kubwa ya Titanic kuzama, gazeti moja lilibeba picha mbili: moja upande huu na nyingine upande mwingine. Ya kwanza ilionesha upande mmoja wa meli umepasuliwa na barafu kubwa, chini yake yameandikwa maneno “Udhaifu wa mwanadamu, ukuu wa Mungu asilia.” Picha ya pili ilimuonesha abiria mmoja akiitoa nafasi yake kwenye mashua ya kuokoa maisha kwa mwanamke mmoja aliyekuwa na mtoto mikononi mwake, chini yake yaliandikwa maneno “Udhaifu wa uasilia, ukuu wa mwanadamu.” Isaya anauona ufalme wa Kusini katika hali hiyo, wenyewe ukihukumiwa bila kuwa na matumani. Kwa msaada wa Mungu unaweza ukainuka tena kutoka kaburini na ukawa hai. Kristo anatualika sote kuupokea huo msaada wake anapotualika akisema “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.” Mwanadamu anao huo udhaifu wa mahangaiko hayo muda aishipo, itakuwa mwanzo wa hekima kama akijitambua mapema na kukimbilia kwa Kristo. Sala: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kukimbilia kwako daima, katika furaha na shida. |