Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 12/07/2024

2024 JULAI 12: IJUMAA-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Yohane Gualberti Abate
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 14:2-9

Bwana anasema: Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie,” Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo tutakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng’ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni.Efraimu atasema,” Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, han nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Wimbo wa Katikati. Zab 51: 3-4, 8-9, 12-13, 17

1.   Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.

(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

2. Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni, Nawe utanijulisha hekima kwa siri, Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi, Unioshe nami nitakuwa mweupe kuliko theluji. (K)

3. Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako, Wala roho yako mtakatifu usiniondolee. (K)

4. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa changu kitazinena sifa zako. (K)

Injili. Mt 10:16-23

Yesu aliwaambia mitume wake: “Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwamwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

TAFAKARI

YESU, MUNGU PAMOJA NASI: Yesu, ni nafsi ya pili ya Mungu iliyoshuka duniani kukutana na mwanadamu ili kumuokoa katika hila zote na vifungo vya shetani. Neno la Mungu akatwaa mwili, akakaa kwetu! Hilo linajidhihirisha wazi katika masomo yetu ya leo. Nabii Hosea anawahubiria watu kuwa, Mungu atakuwa nao nyakati zote mithili ya baba mwenye huruma na upendo tele na tena kama umande wenye kuleta ustawi wa mazao na chanzo cha mafanikio katika jamii yote. Lakini Bwana Yesu anatahadharisha kuwa safari hiyo ya wokovu, inaambatana na msalaba ambao ni chanzo cha wokovu huo tunaouendea. Hivyo, anatuhasa kuwa wavumilivu kwani haitoshi namna ulivyoianza safari yako, namna unavyoienenda safari hiyo, ila zaidi ni namna utakavyoimaliza safari hiyo ndiyo wito tunaouona katika injili kuwa; mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Kwa hali ya kawaida ubinadamu wetu, tunakumbwa na hofu na mashaka ya namna tunaweza kuibuka washindi katika dhiki hizi. Ndiposa tunaalikwa kwa imani kutambua nguvu na uweza wa Mungu ambaye anaambatana nasi siku zote.

Sala: Ee Yesu, utujalie kutambua kuwa wakati tutakapofariki ndiyo mwisho wa mapambano yetu. Amina