Select Page

Tumsifu Yesu Kristo. Karibu Katika Masomo ya Misa 09/07/2024

2024 JULAI 9: JUMANNE-JUMA  LA 14 LA MWAKA

Mt. Veronika Giuliani, Bikira.
Rangi: Kijani

Zaburi: Juma 2

Somo 1. Hos 8:4-7, 11-13

Bwana asema hivi: Wamesimamisha wafalme, lakini si kwa shauri langu; wamejifanyia wakuu, lakini nalikuwa sina habari; kwa fedha yao na dhahabu yao wamejifanyizia sanamu, kusudi wakatiliwe mbali. Amemtupa ndama yako, Ee Samaria; hasira yangu imewaka juu yao; siku ngapi zitapita kabla ya hao kupata hali isiyo na hatia? Maana katika Israeli kimetokea hata na kitu hiki; fundi ndiye aliyekifanya, nacho si Mungu kamwe; naam, ndama ya Samaria itavunjika vipande vipande. Kwa maana wao hupanda upepo, nao watavuna tufani; nafaka haina bua; machipuko yake hayatoi masuke; hata ikiwa yatoa, wageni watayameza. Kwa kuwa Efraimu ameongeza madhabahu kwa dhambi, madhabahu zimekuwa dhambi kwake. Nijapomwandikia sheria yangu katika amri elfu kumi, zimehesabiwa kuwa ni kitu kigeni. Kwa habari za dhabihu za matoleo yangu, hutoa dhabihu ya nyama na kuila; lakini Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, na kuwapatiliza dhambi zao; watarudi kwenda Misri.

Wimbo wa Katikati. Zab 115:3-10

1.  Mungu wetu yuko mbinguni,
Alitakalo lote amelitenda.
Sanamu zao ni fedha na dhahabu,
Kazi ya mikono ya wanadamu.

(K) Enyi Israeli, mtumainini Bwana.

2.  Zina vinywa lakini hazisemi,
Zina macho lakini hazisomi,
Zina maskio lakini hazisikii,
Zina pua lakini haziskii harufu. (K)

3.   Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi,
Wala hazitoi sauti kwa koo zake
Wazifanyao watafanana nao,
Kila mmoja anayezitumainia. (K)

 4.   Enyi Israeli, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao;
Enyi mlango wa Haruni, mtumainini Bwana;
Yeye ni msaada wao na ngao yao. (K)

Injili. Mt 9:32-39

Walimletea Yesu mtu bubu mwenye pepo. Na pepo alipotolewa, yule bubu alinena, makutano wakastaajabu, wakasema,” Haijaonekana hivi katika Israeli wakati wo wote.”Lakini Mafarisayo wakasema,”Kwa nguvu za mkuu wa pepo atoa pepo.”Naye Yesu alikuwa akizunguka katika miji yote na vijiji, akifundisha katika masinagogi yao, na kuihubiri habari njema ya ufalme, na kuponya magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji. Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, “Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache. Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake.”

TAFAKARI

TUMEITWA KUENDELEZA UTUME WA KRISTO: Yesu alifukuza mapepo, aliponya wagonjwa, alifufua wafu, alisamehe dhambi na alitangaza Ufalme wa Mungu.Kristo alielewa hali mbaya waliyokuwa nayo watu wa kawaida kabisa. Hawakuwa na mtu wa kuwapa matumaini na kuwaelezea juu ya fadhila za Kimungu.Ni wajibu wa kila mkristo kutangaza Habari Njema ya wokovu wetu kwa namna ya maisha yake. Alihimiza utume waliopaswa kuuishi wanafunzi wake, uliohitaji kujitoa sadaka, kujikatalia na kufuata mfano wa Kristo. Mark Link anasema Yesu angali andika nukuu katika hili ingekuwa “Sina miguu ila miguu yako kunipeleka ulimwenguni. Sina Mikono ila mikono yako kuwafikia wahitaji. Sina ulimi bali ulimi wako kuwaambia watu ni kwa nini niliteseka na kufa kwa ajili yao.” Somo la kwanza latupa mfano mzuri wa mtu anayeitenda kazi ya Mungu, ni nabii Hosea anaendelea kuitenda kazi ya Mungu akiwaonya Waisraeli juu ya mwenendo wao wa kumwasi Mungu. Anawaalika kufanya toba na wampendeze Mungu. Ndio wito tunaoupokea kila siku ya maisha yetu. 

Sala: Ee Bwana neema yako ituwezeshe kuwafikishia watu wako habari njema ya wokovo.